HATIMAYE Serikali imekubali kuuondoa bungeni Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa mwaka 2015.
Muswada huo, ambao unapingwa na wadau wa habari, ulikuwa usomwe leo bungeni kwa mara ya pili na tatu.
Akitangaza kuondolewa kwa Muswada huo bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, alisema Serikali imetafakari na kuyakubali maoni ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ya kutaka kuendelea kuufanyia kazi muswada huo.
“Serikali imeafiki muswada huo uendelee kufanyiwa kazi hadi hapo Kamati itakapokuwa imekamilisha kazi yake ipasavyo na kuwasilisha maoni yake bungeni,” alisema.
Profesa Mwandosya alisema matarajio ni kwamba muswada huo utasomwa kwa mara ya pili na ya tatu katika Bunge lijalo.
“Muswada wa Sheria ya Upatikanaji Habari wa mwaka 2015, ulichapishwa Februari 20, mwaka 2015 na ukasomwa kwa mara ya kwanza bungeni katika Mkutano wa 19, kwa hiyo muswada huu si wa dharura kama wengine wanavyosema,” alisema
Alisema hata hivyo, Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii iliyokutana Juni 22 mwaka huu iliujadili kwa kina na kuzingatia maoni ya wadau wa tasnia hiyo muhimu ikashauri kupewa muda zaidi kwa ajili kuendelea kupata maoni zaidi ya wadau.
“Naomba kutoa ushauri kwa wadau ambao bado wanaendelea kutoa maoni kwa Kamati na wale ambao hawajatoa ushauri waendelee kufanya hivyo ili kupata Muswada ulio bora na sheria nzuri kwa maslahi ya Taifa,” alisema.
Profesa Mwandosya alisema mchakato wa kutunga sheria za nchi ni shirikishi na ni wa wazi na kwamba sheria inayokusudiwa kutungwa kila wakati huwa ni kwa manufaa ya jamii na kwa Taifa.
Wadau mbalimbali wa habari wamekuwa wakipinga kuwasilishwa kwa muswada huo bungeni kwa sasa kutokana na kutokukidhi viwango na kutozingatia maoni ya wadau.
Baadhi ya wadau hao ni pamoja na Jukwaa la Wahariri (TEF), Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Baraza la Habari la Nchi za Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISATAN), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu na Jukwaa la Katiba na baadhi ya asasi zisizo za kiraia.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago