RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein amesema mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa asilimia 90 ndiyo uliomsukuma kuchukua fomu ya kugombea tena urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM.
Aidha, ameahidi endapo atapewa tena ridhaa ya kuiongoza Zanzibar katika miaka mitano mingine, atahakikisha Zanzibar inakuwa na maendeleo na mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo za kiuchumi na utawala bora.
Aliyasema hayo jana alipozungumza na viongozi wa CCM katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa mara baada ya kukabidhiwa fomu ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar.
Alifafanua kuwa utekelezaji wa ilani ya CCM na kuwatumikia wananchi kwa uadilifu mkubwa na kuleta maendeleo ndiyo uliomshawishi kugombea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili sasa.
“Nimeamua kuchukua fomu kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM kwa sababu ya kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa ilani ya CCM kwa asilimia 90,” alisema.
Akiyataja baadhi ya mafanikio yake, alisema mara baada ya kuingia madarakani alifanya kazi kubwa kuhakikisha taasisi zinazokusanya kodi zinasimamia majukumu yake ambapo katika mwaka 2011 Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ilikuwa ikikusanya jumla ya Sh bilioni 13.5 na sasa jumla ya Sh bilioni 39 zinakusanywa kwa mwezi.(VICTOR)
Alisema makusanyo hayo yameifanya Serikali kuongeza maslahi kwa watumishi wake ikiwemo kulipa mishahara kwa wakati na viinua mgongo kwa wafanyakazi wastaafu serikalini.
Alifahamisha kwamba hatua hizo zimeufanya uchumi wa Zanzibar sasa kukua kutoka asilimia 5.2 katika mwaka 2010 na kupanda hadi asilimia 7.2 hivyo kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika ukuaji wa pato la mwananchi wa kawaida.
Aidha alisema katika utekelezaji wa malengo yake, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Abeid Amaan Karume uliopo Unguja upo katika hatua za mwisho za kukamilika kwake ambapo unatarajiwa kukabidhiwa Serikali mwezi wa Oktoba.
“Ujenzi ulikwama kwa sababu za kiufundi, lakini tumerekebisha kasoro na sasa unaendelea kwa kasi kubwa na utakapomalizika utaruhusu ndege zote kubwa kutua bila ya matatizo,” alisema.
Alisema kazi za matengenezo za kuweka taa katika Uwanja wa Ndege wa Karume Pemba zinaendelea ambapo pia upo mpango mkubwa wa kuufanyia matengenezo uwanja huo kwa kiwango cha kuruhusu ndege kubwa kutua.
Alisema Serikali yake imechukua juhudi zote kuhakikisha kisiwa cha Pemba kinapata mabadiliko makubwa ya ukuaji wa uchumi na maendeleo sambamba na yale yaliyopo Unguja.
“Nataka niwaambie wananchi kwamba kila kinachofanyika Unguja na Pemba tunafanya kwa ajili ya ukuaji na ustawi wa wananchi wake......Pemba leo imebadilika,” alisema.
Alivitaja vipaumbele vyake kama akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ikiwemo kulinda Muungano kwa nguvu zote za Serikali mbili na hatakubali kuchezewa.
Alisema Muungano ndiyo kielelezo kikubwa cha utambulisho wa Watanzania kwa hivyo unahitaji kulindwa na kamwe watu wenye nia mbaya wasipewe nafasi kuuchezea.
Aliwapongeza wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa kuhakikisha kwamba muundo wa Seriali mbili katika Muungano unaendelezwa na kuwataka wananchi kuipigia kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa kwa ajili ya maslahi ya Zanzibar.
Aidha alisema atahakikisha amani na utulivu unadumishwa katika kipindi chote na watu wenye nia ya kuleta chokochoko atawashughulikia kwa mujibu wa katiba na utawala bora.
Alisema mabadiliko makubwa yamefikiwa Zanzibar katika kipindi cha miaka mitano chini ya Serikali ya umoja wa kitaifa ambapo amani na utulivu umedumu na kutoa nafasi kwa wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo bila ya matatizo.
“Nasisitiza na kusema kwamba sina mchezo na suala la kuchezea amani na utulivu na watu watakaoleta chokochoko kwa lengo la kuleta mgawanyo wa Wazanzibari nitawashughulikia kwa mujibu wa katiba na utawala bora wala sio kwa ubabe,” alisema.
Mapema Dk Shein alikabidhiwa fomu nakala 3 za udhamini wa wanachama wa CCM kwa nafasi ya urais wa Zanzibar na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
Msaidizi wa Mkapa, Mwinyi Emmanuel Ghula anaripoti kutoka Dar es Salaam kwamba aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Patrick Chokala ametangaza nia ya kuwania tena kuteuliwa na CCM kuwania Urais wa Tanzania, akisema ana uwezo wa kuiongoza nchi na kuifikisha katika hatua nzuri kimaendeleo.
Balozi Chokala aliyepata pia kuwa mwandishi wa habari wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na kuendelea kuwa mmoja wa wasaidizi wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam.
Kwa Chokala, hii ni mara yake ya pili kujitosa kuwania urais, kwani kwa mara ya kwanza alifanya hivyo mwaka 2005 akichuana na Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, Dk Salim Ahmed Salim, John Shibuda, Dk William Shija (marehemu), John Malecela, Frederick Sumaye, Dk Abdallah Kigoda, Balozi Ali Karume na Iddi Simba.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza nia yake ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini, Chokola alisema haoni sababu ya Tanzania kutokuwa na maendeleo makubwa kwani ina kila kitu ambacho kikitumiwa kwa utaratibu kitaleta maendeleo.
“Sisi tuna kila kitu, mfano bandari pekee ya Dar es Salaam inaweza kuifanya nchi kujipatia fedha nyingi sana na kujitosheleza kuhudumia baadhi ya miradi ya maendeleo.
Kitu kinachohitajika ni kuweka miundombinu vizuri ya usafirishaji hasa mizigo inayopitia bandarini,” alisema Chokala. Akieleza vipaumbele vyake, alisema pamoja na kukuza uchumi kwa kupitia bandari, pia atasimamia vizuri sekta ya madini na uwekezaji kutokana na kuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.
Katika sekta ya utalii, alisema ataongeza jitihada za kupambana na ujangili ili kulinda rasilimali asilia ikiwemo wanyama na kuongeza idadi ya watalii kwani kupitia utalii nchi itajipatia sio tu umaarufu wa kuwa kivutio cha watalii bali sekta hiyo itaongeza fedha za kigeni.CHANZO:HABARI LEO
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago