TAARIFA KWA WAANDISHI WA HABARI
Leo tarehe 6 Agosti, 2015 Profesa Ibrahim Lipumba aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Peacock, mjini Dar es Salaam na kutangaza kwamba amejizulu nafasi yake kama Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF).
Sisi kama Chama tumezipokea taarifa hizo na tunayaheshimu maamuzi yake. Ni haki yake ya kikatiba na haki ya kidemokrasia kufanya maamuzi anayoyaona yana maslahi kwake.
Bila shaka, Profesa Ibrahim Lipumba amekifanyia kazi kubwa Chama chetu katika miaka 16 ambayo alikuwa Mwenyekiti wetu, nafasi iliyomfanya awe kiongozi wetu mkuu. Kwa nafasi yake hiyo, pia ametoa mchango mkubwa katika ujenzi wa demokrasia katika nchi yetu. Tunaithamini kazi hiyo na tutaendelea kumheshimu kwa utumishi wake mkubwa kwa Chama chetu na nchi yetu. Tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ya baadaye.
Chama Cha Wananchi (CUF) ni taasisi na kinaendeshwa kitaasisi. Ndiyo maana maamuzi yake yote yamekuwa yakifanywa kitaasisi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama. Kwa msingi huo, pamoja na ukweli kwamba kuondoka kwa Profesa Lipumba katika safu ya uongozi kutaacha pengo hasa katika kipindi hichi ambacho tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, tunawahakikishia wanachama na wapenzi wa CUF na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwamba Chama hichi hakitayumba.
Katika historia yake, CUF imepita katika dhoruba na misukosuko mingi lakini mara zote kimeonesha uwezo mkubwa wa kuhimili dhoruba na misukosuko hiyo na kukabiliana na athari zake. Hatuna chembe ya wasiwasi kwamba hata mtihani huu tutauvuka na tunaamini tutaibuka tukiwa Chama imara zaidi.
Katibu Mkuu ameagiza kuitishwa kwa vikao vya dharura vya Kamati ya Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa siku ya Jumapili, tarehe 9 Agosti, 2015 ili kujadili hatua hiyo na kufanya maamuzi juu ya hatua muafaka zinazopaswa kuchukuliwa katika kipindi hiki hadi hapo Chama kitakapomchagua mwanachama mwengine kujaza nafasi hiyo ya Mwenyekiti.
Katika kipindi hiki, Chama kinawataka wanachama na wapenzi wake wote kuwa watulivu na wavumilivu na kusubiri maelekezo ya vikao vya juu vya kitaifa vya Chama.
Mwisho kabisa, tunawahakikishia wanachama wetu na Watanzania wote kwa ujumla kwamba CUF itaendelea na shughuli zake kama Chama na pia kama mshirika katika UKAWA ambayo CUF ilikuwa ni katika waasisi wake.
Tunawahakikishia wanachama wetu na Watanzania wote kwa ujumla kwamba CUF itatumia nguvu, uwezo, juhudi na maarifa yake yote kuhakikisha kwamba inaulinda UKAWA ambao unaonekana kuwa mwiba kwa CCM.
Tunatambua kwamba kuna njama na mbinu kubwa na nyingi zinazofanywa na watawala kutaka kuuvuruga na kuuhujumu UKAWA wakidhani kwamba watapata manusura.
Tumesema na tunaendelea kusema CCM mwaka huu hawana manusura.
Watanzania wameamua kuwan’goa, na watan’goka Tanzania Bara na Zanzibar kupitia sanduku la kura tarehe 25 Oktoba, 2015. Wimbi hili kubwa la mabadiliko halizuiliki tena.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAWASILIANO NA UMMA
06 AGOSTI, 2015
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago