SIKU moja baada ya vyama vinavyounda Ukawa kuomba kufanyika mdahalo utakaowajumuisha viongozi wa vyama, badala ya wagombea urais, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejitokeza na kutaka ufanyike mdahalo utakaowajumuisha wagombea urais wote, bila yeyote kukimbia.
Katika kusisitiza kauli yao, CCM imesema mgombea wake wa urais, Dk John Magufuli amekubali kushiriki mdahalo wa wagombea urais, ulioitishwa kwa pamoja na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Taasisi ya Twaweza na imemtaka mgombea wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vya CUF, NCCR – Mageuzi na NLD, Edward Lowassa kushiriki.
Pia, chama hicho kimesema utafiti wa ndani uliofanywa kwa kipindi cha siku 10 zilizopita katika majimbo 246, kati ya majimbo 269, unaonesha kwamba Dk Magufuli atapata ushindi wa asilimia 69.3.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba alipozungumza na waandishi wa habari.
Midahalo ya wagombea
January akizungumza na wanahabari jana alisema; “Wiki tatu zilizopita, CCM, na kwa hakika vyama vingine pia, ilipokea mwaliko wa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli, kushiriki kwenye mdahalo wa wagombea urais ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania kwa kushirikiana na taasisi kadhaa ikiwemo Twaweza.
“Dk Magufuli amekubali kushiriki katika mdahalo huo. Kwa msingi huo, kauli ya Ukawa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia, kwamba Ukawa inaomba mdahalo ni njia ya kuwahadaa Watanzania tu kwa kuwa mwaliko wa mdahalo ulikwishatolewa mapema kwa vyama vyote na wanaotakiwa kushiriki ni wagombea urais wa vyama.”
Katika kile kinachodhihirisha chama hicho kupania kushiriki mdahalo, January alisema CCM inafurahishwa na utamaduni wa midahalo, ambao unaanza kujitokeza katika uchaguzi nchini na inaamini midahalo ya wagombea urais ni sehemu muhimu ya kuwashirikisha wapiga kura katika mchakato wa uchaguzi na kuwasaidia waamue, nani wamchague kwa misingi ya hoja na sera na si kwa ushabiki, mihemko na propaganda.
“Mdahalo unatoa fursa ya wagombea kuulizwa maswali ya moja kwa moja na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu sera na ahadi zao, fursa ambayo hawaipati kwenye mikutano ya hadhara ya kampeni,” alisema.
January alisema; “Hatukubaliani na kauli ya Ukawa kwamba mdahalo usiwe baina ya wagombea, bali uwe baina ya wenyeviti wa vyama. Tunaamini hoja hii ni kichekesho.
“Haijawahi kutokea popote duniani kwenye utamaduni wa midahalo, kwamba wagombea wasishiriki bali watu wengine ndio wafanye midahalo kwa niaba yao.
"Tunaamini mdahalo huu, unapaswa kuwa baina ya wagombea. Wao ndio wanaoomba dhamana, wao ndio wanaopaswa kujibu maswali na kufafanua kuhusu ahadi zao.
“CCM inaamini kwamba ili mdahalo huu uwe na tija, wagombea urais wote, hasa wa vyama vikuu wawepo na washiriki.
"Mdahalo hautakuwa na maana kama mgombea mmojawapo wa vyama vikuu atatengeneza kisingizio ili asishiriki”.
Mwenendo wa kampeni
Akiwa Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January alitumia fursa hiyo ya mkutano na wanahabari kueleza mwenendo wa kampeni za Dk Magufuli, akisema utafiti unaonesha kuwa atapata ushindi wa asilimia 69.3, ingawa upo uwezekano wa asilimia hizo kupanda kiasi.
Alisema hadi juzi, Dk Magufuli alikuwa amefanya kampeni katika mikoa 12 na majimbo 94. Pia, alikuwa amefanya mikutano mikubwa ya hadhara 76 na mikutano ya barabarani 381.
Alisema mgombea huyo ambaye ni Waziri wa Ujenzi, aliyepata mafanikio makubwa katika ujenzi wa barabara za lami nchini, amekwishatembea kwa gari jumla ya kilomita 13,720 na amekutana moja kwa moja na asilimia zaidi ya 30 ya wapiga kura.
Alisema kwamba kwa kuwa mikutano ya CCM inatangazwa moja kwa moja na vituo vya redio na televisheni, wapiga kura waliopata nafasi ya kumsikia wanafikia asilimia 70.
“Tunafarijika na idadi kubwa ya watu wanaokuja kwenye mikutano ya kampeni zetu.
"Tunafarijika pia kwamba karibu Watanzania wote wanaopata fursa ya kumuona na kumsikia wamemuelewa na wamepata matumaini ya Tanzania Mpya kupitia kwake. "
Alisema kwa upande wa kampeni za ubunge, zaidi ya robo tatu ya wagombea ubunge wa CCM wamekwishazindua kampeni zao na wanaendelea vizuri, huku akiweka hadharani mpango wa Sekretarieti ya CCM kuandaa programu maalumu ya kampeni katika majimbo yenye changamoto mahsusi.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwajulisha wana-CCM kwamba viongozi na makada wengine wa CCM, waliopo madarakani na wastaafu watapita tena, jimbo kwa jimbo, nchi nzima katika siku 30 za mwisho katika jitihada za kuongeza ushindi wa CCM na Dk Magufuli,” alisema January.
Alisisitiza mwito unaoendelea kutolewa na CCM mara kwa mara wa kufanyika kwa uchaguzi wa amani na uchaguzi unaoendelea kujenga Umoja wa Kitaifa, akisema CCM inasikitishwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi, ambazo zinaashiria fujo na vurugu.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago