Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amefunguka na kuwaomba Watanzania kumpa kura ambazo ameziita bakora ili awacharaze viboko watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ufisadi nchini.
Lowassa ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia umati katika mkutano wa kampeni kwenye Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, mjini Morogoro.
Alisema ili kutekeleza azima yake, ni vizuri wananchi wakajitokeza kwa wingi kama Oktoba 25, mwaka huu kama walivyojitokeza jana wapige kura ili kumpa kazi ya kuwanyoosha mafisadi.
Akizungumza huku akikatizwa kutokana na kushangiliwa na umati, Lowassa alisema Serikali yake itahakikisha inawashughulikia wale wote watakaotumia vibaya fedha au madaraka waliopewa kinyume cha sheria na taratibu.
Lowassa alijiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu mwaka 2008, kama njia ya kuwajibika baada ya kuibuka kwa sakata ya serikali kuipa zabuni kampuni ya kufua umeme ya Richmond katika mazingira tata.
Sakata hilo liliibuliwa na Kamati Teule iliyoongozwa na Mbunge wa kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, baada ya kuchunguza na kuwasilisha ripoti bungeni.
Hata hivyo, baadhi ya mahasibu wake wa kisiasa wamekuwa wakimhusisha na tuhuma hizo, lakini ameshazikanusha na kuwataka wenye ushahidi kwenda mahakamani vinginevyo wafunge midomo.
Kadhalika, Lowasa ameshasema kuwa maagizo ya kuipa kampuni hiyo zabuni ya kufua Megawati 100 za umeme wa dharura yalitoka mamlaka za juu.
Mama lishe,Bodaboda
Katika hatua nyingine, Lowassa alisema kuwa atakapochaguliwa, Serikali yake itahakikisha inaanzisha benki maalum ya maendeleo kwa ajili ya mamalishe, waendesha bodaboda pamoja na wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga.
Lowassa alisema kuwa ataanzisha beki hiyo kwa kuwa ni moja ya mikakati ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo pamoja na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya biashara bila kubughudhiwa na mgambo.
Kufufua Viwanda
Kuhusu viwanda vilivyokufa katika Mkoa wa Morogoro baada ya kubinafishwa, alisema kuwa baada ya kuchaguliwa atahakikisha, anafanya utafiti wa kuviangalia upya viwanda hivyo kama vinaweza kufufuliwa na Serikali au kujengwa upya kwa ajili ya kutoa ajira kwa wakazi wa mkoa huo.
Alisema mkoa huo kwa miaka kadhaa iliyopita ulikuwa wa viwanda na wakazi wake walipata maendeleo, hivyo ni lazima asimamie kurudishwa kwa uchumi wa viwanda kwa lengo la kuwasaidia wakazi wake.
Kilimo cha Kisasa
Kuhusu kilimo, Lowassa alisema kuwa wananchi wengi wa mkoa huo wanategemea zaidi kilimo, hivyo katika utawala wake atahakikisha wanawekewa mazingira ya kulima kilimo cha kisasa pamoja na kuwapunguzia kodi ambazo zinaonekana sio rafiki kwao.
Elimu ya Bure
Kwa upande wa elimu, Lowassa alisema kuwa atakapochaguliwa, elimu itakuwa bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne na kwamba elimu itakayotolewa itakuwa bora na si bora elimu kama ilivyo sasa.
Alisema kuwa hayo yote hayatafanikiwa ikiwa wananchi hao hawatajitokeza kumpigia kura Oktoba 25, mwaka huu.
Sumaye: Msiogope
Kwa Upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, aliwataka wananchi kutotishika na vitisho vinavyotolewa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa upinzani ukiingia Ikulu kutakuwa na machafuko.
Sumaye aliahidi kuwa Serikali ya Ukawa ikiingia madarakani itahakikisha inasimamia mambo mbalimbali waliyoyaainisha kwenye ilani yao tofauti na serikali ya CCM ambayo alisema licha ya kuahidi maisha bora na kukusanya kodi za wananchi, bado hali ya maisha imeendelea kuwa mbaya siku hadi siku.
Awali, mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro kupitia Chadema, Albanie Marcus, aliomba wananchi wa Manispaa ya Morogoro kumchagua katika nafasi hiyo ili ashirikiane na Lowassa kurudisha viwanda 14 vilivyobadilishwa matumizi yake.
Alisema kuwa katika uongozi wake atahakikisha viwanda ambavyo vimebadilishwa matumizi yake vinafufuliwa na kuwa sehemu ya ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro.
Marcus alisema kuwa katika mji wa Morogoro huduma mbalimbali za kijamii zikiwamo za barabara na afya hususani kwa wanawake na watoto zimezorota na kusababisha vifo visivyo vya lazima na kuahidi kuwa wananchi wakimchagua, atahakikisha anazisimamia na zinaboreshwa.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago