Magufuli Asema M4C ni ‘Magufuli for Change’

Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema maana na neno M4C, linalotumiwa na Chadema ni "Magufuli for Change” akimaanisha ndiye atakayeleta mabadiliko.

Dk Magufuli alitoa kauli hiyo jana katika Kata ya Nguruka, Jimbo la Kigoma Kusini mkoani Kigoma, alipohutubia mkutano wa hadhara wa kampeni ambapo aliwabeza wapinzani kuwa hawawezi kurudi kwa wananchi kuangalia shida zao.

“Mkiangalia hizi picha za wagombea, mimi nimevaa shati, mwingine amevaa suti. Sasa huyu mwenye suti anaweza kukubali kuja kupata shida na nyinyi huku?” alihoji na kuongeza:

“Wanasema M4C, mnajua maana yake?” aliuliza mgombea huyo na kujibu mwenyewe, “maana yake ni ‘Magufuli for Change’.

Katika mkutano huo, mgombea huyo alimtaka mgombea ubunge wa chama hicho katika jimbo hilo, Hasna Mwilima amwachie matatizo ya jimbo hilo ayashughulikie mwenyewe.

Matatizo yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo ni bei ya tumbaku, kukosekana kwa umeme na maji na upandishaji hadhi kituo cha afya cha Nguruka kuwa hospitali ya Wilaya ya Uvinza.

Dk Magufuli alisema kazi ya kwanza atakayompa waziri wake wa kilimo, itakuwa ni kutafuta soko la zao la tumbaku kwa mikoa ya Tabora na Kigoma ili wananchi wauze kwa bei nzuri.

“Mchagueni Hasna Mwilima ili akawawakilishe bungeni, lakini kwa matatizo haya niachieni mimi. Haiwezekani mpaka sasa Nguruka hamna umeme,” alisema mgombea huyo.

Akiwa katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, alimtambulisha mgombea ubunge wa jimbo hilo, Peter Serukamba na kuwataka wananchi kumchagua ili akashirikiane na Serikali yake bungeni.

Lakini ilipofika zamu ya mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Dk Amani Kabourou, hali ilibadilika na kutokea minong’ono ya wananchi kama ishara ya kumkataa pale alipopewa nafasi ya kuwasalimia.

Dk Kabourou alianza kuzungumzia mipango yake endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa mara nyingine, hata hivyo wananchi walisikika wakisema ‘hapana, hapana’ huku wakinyoosha mikono juu kuonyesha ishara ya kumkataa mgombea huyo.

Wakati Dk Magufuli alipojaribu kumnadi mgombea huyo, wananchi walianza tena kupiga kelele, wakisema ‘hatumtaki...’ jambo lililomfanya Dk Magufuli kutomwombea kura na kuendelea kuzungumzia mambo mengine.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company