Baraza la Vyama vya Siasa kujadili vurugu za wabunge

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa , Peter Kuga Mziray
Vurugu za wabunge zilizotokea wakati wa kikao cha 10 cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatimaye zimetua katika Baraza la Vyama vya Siasa ambalo limeamua kujadili suala hilo wakati wa mkutano mkuu wa baraza hilo utakaofanyika mwanzo mwa mwezi ujao.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Kuga Mziray, akizungumza na NIPASHE jana alisema mkutano huo ambao utakuwa na ajenda zaidi nane, utafanyika kwa siku mbili kuanzia Machi 5 hadi 6, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mziray ambaye pia ni Rais Mtendaji wa Chama cha APPT Maendeleo, alisema pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili hali ya mwenendo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa kutokana na vurugu zilizojitokeza wakati wa kikao cha Bunge la 10 kilichomalizika mwanzo ni mwa mwezi huu. Alisema hatua ya baraza hilo kuamua kujadili suala la mwenendo wa Bunge, inalenga kutaka vyama vyenye wabunge na visivyo na wabunge, kuweka utaratibu mzuri ambao utawafanya Watanzania kuvutiwa na vikao vya Bunge badala ya kuchukia kutokana na vurugu zilizoanza kujitokeza.

Alizitaja ajenda jingine zitakazojadiliwa kuwa ni suala la ruzuku kwa vyama vyote vya siasa, uundaji wa Tume huru ya uchaguzi, maboresho ya madaftari ya wapiga kura na kupitia kanuni za Baraza la Vyama vya Siasa.

Mapema Februari 4, mwaka huu, kulitokea vurugu Bungeni wakati Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, akiwasilisha hoja binafsi kuhusu tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam.

Kufuatia hali hiyo, Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge, ilifanya uchunguzi na kuwasilisha ripoti yake bungeni ambayo iliwatia hatiani wabunge wanne kutoka Chadema kwamba walihusika na vurugu hizo.

Wabunge hao ni Mnyika mwenyewe, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Viti Maalum, Pauline Gekul.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, wabunge hao walikutwa na hatia baada ya kamati hiyo iliyopewa kazi ya kuchunguza chanzo cha vurugu kumaliza kazi yake.

Akiwasilisha taarifa ya kamati, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hassan Ngwilizi, alisema kamati hiyo ilitumia picha za televisheni za TBC kuwatambua wabunge waliohusika na vurugu hizo na kuwabaini.

Ngwilizi alisema hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni za Bunge za 60 na 68 zinaeleza mchakato wa majadiliano bungeni huku ikitoa nafasi kwa mbunge kutoa taarifa bungeni.

Katika hoja yake, Mnyika aliitaka serikali kuchukua hatua za kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama pamoja na ushughulikiaji wa majitaka katika Jiji la Dar es Salaam.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company