Uhaba wa vifaa vya umeme:Muhongo agonga mwamba


  Tanesco sasa kuingiza nguzo kutoka Afrika Kusini
  Yaponda viwango vya ubora wa nguzo za ndani
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
Zile tambo za Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kubaini ufisadi katika biashara ya ‘kuingiza’ nguzo za umeme kutoka Afrika Kusini, zimefika ukomo.

Julai mwaka jana, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni, Profesa Muhongo, alisema kuna biashara haramu ya kuchukua nguzo kutoka mashamba ya ndani na kuzibadili ili zionekane zinatoka Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, nguzo hizo zilisafirishwa hadi Mombasa nchini Kenya, kisha kurejeshwa nchini zikionyesha kutoka nje ya nchi.

Biashara hiyo ilichangia ongezeko la gharama za kuunganisha umeme ambazo hata hivyo, serikali kupitia kwa Profesa Muhongo, ilitangaza kuzishusha kuanzia Januari mwaka huu.
Hata hivyo, wakati kipindi cha punguzo hilo kikielekea mwezi wa tatu sasa, NIPASHE Jumamosi imebaini kuwepo ukosefu wa vifaa vya kuunganisha umeme, zikiwamo nguzo.

Taarifa za ndani kutoka Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) zilieleza kuwapo maombi mengi ya kuunganishiwa umeme, lakini utekelezaji wake ni duni, ukitokana na ukosefu wa vifaa hivyo.

Hali hiyo imeibua utata na hisia za kuwapo hujuma zenye lengo la kufanikisha azma ya wafanyabiashara walioathirika kutokana na tamko la Profesa Muhongo bungeni.

TANESCO KUINGIZA NGUZO ZA AFRIKA KUSINI
Taarifa zilizothibitishwa na uongozi wa juu wa Tanesco, zimeeleza kuwapo mpango wa kuingiza nguzo kutoka Afrika Kusini ‘mapema iwezekavyo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchismi Mramba, alisema jana kuwa kutokana na uhaba wa nguzo uliopo, wameamua kuziagiza kutoka katika kampuni mbili za Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa Mramba, shehena ya nguzo hizo inatarajiwa kuingia nchini katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

“Tunategemea kupokea nguzo kutoka Afrika Kusini wiki ijayo, na hilo tatizo la upungufu linaloikabili shirika kwa sasa utakuwa umemalizika,” alisema.

Hata hivyo, Mramba alisema maeneo yenye mradi wa umeme ambayo yalisimama kutokana na upungufu wa nguzo, yataendelea na kazi mara baada ya kuwasili kwa shehena hiyo.

APONDA UBORA WA NGUZO ZA NDANI
Mramba alisema nguzo za umeme zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini, hazina viwango vya kutosha kukidhi mahitaji ya matumizi.

Tangu serikali ilipoanza kutekeleza ahadi ya kupunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi, uhaba wa vifaa zikiwamo nguzo umeripotiwa maeneo tofauti ya nchi.

Vituo vingi vya Tanesco vilivyopo kwenye kanda tofauti na vinavyopaswa kusambaza vifaa vya kuunganishia nishati hiyo, vinadaiwa kukabiliwa na ukosefu wa vifaa hivyo.

“Kwanza viwanda vya ndani havitoshelezi mahitaji ya nguzo nchini, ndiyo maana tunaagiza nje, lakini pamoja na kutotosheleza mahitaji, nguzo zenyewe hazina ubora unaostahili na bei yake ni ghali,” Mramba alisema.
Mramba alisema pamoja na kasoro hizo, Tanesco inawajali wazalishaji wa nguzo wa ndani kwa kutangaza zabuni kwa wazalishaji wa nchini pale zinapohitajika.

MUHONGO ASEMA HANA ALIJUALO
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu kero na hatua iliyofikiwa na Tanesco kuhusu kadhia hiyo, Profesa Muhongo, alisema hana taarifa na uagizaji huo.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Profesa Muhongo, alisisitiza, “sina jibu la kutosha, ngoja kwanza niwasiliane na viongozi wa Tanesco kisha nitakuwa na jibu la kutoa.”

Hata hivyo Profesa Muhongo alisema kamwe hawezi kuyazungumzia mambo aliyowahi kuyatolea maelezo ama ufafanuzi kuhusiana na suala hilo.

Awali, meneja wa Tanesco wa kanda ya Tegeta katika manispaa ya Kinondoni, Gipson Gihoswa, alisema wasemaji wa upungufu wa nguzo na vifaa vingine vinavyohusiana na umeme ni Makao Makuu ya shirika hilo.

Tegeta ni moja ya maeneo ambayo waandishi wa gazeti hili walifanya ziara ya kiuchunguzi, kubaini uhalisia wa tatizo lililo katika kuunganisha umeme.
 “Sehemu itakayoweza kuwapa majibu sahihi ni kwa meneja wa Tanesco mkoa wa Kinondoni Kaskazini ama makao makuu, hao watawapa majibu sahihi kuhusu ukosefu wa vifaa hivyo,” alisema Gihoswa.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company