WATU sita wamezama katika mwambao wa Bahari ya Hindi Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, baada ya boti yao waliyokuwa wakisafiria kuzama baada ya kupigwa na dhoruba kali ilipokuwa safarini. (HM)
Akizungumza jana muda mfupi katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi mnamo saa moja usiku ambapo watu hao walikuwa wakisafiri kwenda katika moja ya visiwa wilayani hapa.
"Kama unavyoona tupo katika jitihada za kuhangaika kutafuta miili ya watu watatu ambapo mpaka hivi sasa mida ya jioni hatujaweza kuipata na tumeamua kuahirisha kazi hii mpaka kesho tutakapoendelea tena kuwasaka, tunahisi huenda wakawa wamepoteza maisha," alisema.
Akisimulia tukio hilo, Revina Mdemo ambaye ni mmoja ya watu walionusurika katika ajali hiyo, alisema walikuwa katika safari yao ya kawaida ya kwenda Hoteli ya Las Lagoon iliyopo kisiwani, ndipo walipokumbwa na hali hiyo.
Mdemo alisema siku hiyo walianza safari muda wa saa 12 jioni, wakiwa zaidi ya abiria 6 na ndani ya boti hiyo walikuwa wamepakia jumla ya lita 3000 za maji kwa ajili ya matumizi ya hotelini hapo.
"Tulikuwa tumepakia maji lita 3000 kwa ajili ya kupeleka hotelini kwetu na pia tukabeba na watu sita ambao wengine ni wafanyakazi wa hoteli hiyo na wengine ni familia ya mmoja wa wafanyakazi wa hoteli," alisema.
Aliwataja baadhi ya watu ambao miili yao imeonekana ni Elikarano Malile mkazi wa Njombe (39), ambaye alikuwa na mke wake Hawa Mtungi (31) na mtoto wake, huku Elisandre Malile mwenye umri wa miezi minane pamoja na Robert Kyando wakiwa hawajaweza kuonekana. Chanzo: mtanzania