Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa maslahi ya makampuni ya Marekani yanayotaka kuwekeza katika Tanzania hayataathiriwa na kuwepo kwa China katika uchumi wa Tanzania kwa sababu China siyo moja ya wawekezaji wakuu katika uchumi wa Tanzania kwa sasa.www.hakileo.blogspot.com
Rais Kikwete amesema kuwa miongoni mwa wawekezaji wakuu wa uchumi wa Tanzania, China inashikilia nafasi ya 10 huku Uingereza ikiwa inaongoza katika kuwekeza katika Tanzania.(P.T)
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa misaada ya maendeleo kwa Tanzania lakini siyo katika makampuni ya nchi hiyo kuwekeza katika uchumi wa Tanzania na hivyo nchi hiyo haiwezi kuwa tishio kwa
uwekezaji wa makampuni ya Marekani.
Rais Kikwete ametoa ufafanuzi huo mchana wa Jumatano, Septemba 18, 2013, wakati alipokutana katika mkutano wa kikazi na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Mahusiano ya Nje na Bajeti ya Miradi ya Maendeleo ya Bunge la Marekani mjini Washington, D.C., pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati yake.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete aliulizwa jinsi gani fedha ya Jamhuri ya Watu wa China katika uchumi wa Tanzania inavyoathiri uwekezaji wa makampuni ya Marekani.
"Napenda kuwahakikisheni kuwa hakuna athari yoyote. China inashikilia nafasi ya 10 katika uwekezaji katika nchi yetu na hivyo siyo miongoni mwa nchi zinazoongoza katika uwekezaji. Nchi ya kwanza kabisa ni Uingereza ikifuatiwa na Kenya, India na Afrika Kusini. Hizi ndizo nchi kubwa nne."
Ameongeza Rais Kikwete: "China iko zaidi katika kutoa misaada ya maendeleo ambako kwa kweli huko ni miongoni mwa nchi zinazoongoza siyo kwenye uwekezaji. Walitujengea TAZARA, wamejenga Uwanja wa Taifa, sasa wanajenga Bomba la Mafuta kutoka Mtwara hadi Dar Es Salaam, watajenga Bandari ya Bagamoyo...yote hii ni kwenye misaada ya maendeleo."
"Ni msaada wa maendeleo wa China kwa nchi yetu kama tunavyopokea misaada ya nchi nyingine na kama China inavyotoa misaada kwa nchi nyingine. Hivyo, kwa kweli hakuna tishio lolote kwa uwekezaji wa Marekani kutoka kwa Wachina katika Tanzania, sijui nchi nyingine. Kwa Marekani nadhani mtu wa kumwogopa katika uwekezaji katika Tanzania ni Uingereza."
Wakati huo huo, Rais Kikwete ametoa rambirambi kwa Serikali na Bunge la Marekani kufuatia mauaji ya watu 12 yaliyofanywa na kijana mmoja mwenye umri wa miaka 34 kwenye Kambi Moja ya Jeshi la Maji la Marekani mjini Washington, D.C.,mwanzoni mwa wiki hii.
"Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwa niaba ya nchi yangu, Serikali na mimi binafsi kutoa salamu zangu za rambirambi kufuatia tukio hili la kusikitisha sana ambako watu wasiokuwa na hatia wamepoteza maisha yao."
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.