Johannesburg. Mtanzania Agnes Gerald, maarufu Masogange, ameachiwa huru na Mahakama ya Kempton ya jijini Johannesburg, baada ya kulipa faini ya R30,000 (Sh4.8 milioni) kwa kosa la kubeba kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya.(hd)www.hakileo.blogspot.com
Wakati Masogange akitozwa faini hiyo mwenzake, Melissa Edward ameachiwa huru na mahakama hiyo, baada ya kukosekana ushahidi wa kumtia hatiani.
Msemaji wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai cha Afrika Kusini(Hawk), Kapteni Paul Ramaloko alisema Watanzania hao wameachiwa huru baada ya kuonekana kuwa hawakubeba dawa za kulevya, bali kemikali aina ya ephedrine.
Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa, Melissa hana hatia kwa kuwa ilionekana kuwa amemsindikiza Masogange, ambaye alimwomba amsaidie kubeba mzigo huo.
"Mahakama iliona kuwa Melissa aliombwa tu kumsaidia kubeba baadhi ya mabegi, lakini hayakuwa yake. Mizigo yote iliandikwa jina la Agness Gerald na si Melissa," alisema Kapteni Ramaloko.
Kapteni Ramaloko alisema, Melissa alijitetea kuwa hakuwa amesafiri pamoja na Masogange bali walikutana ndani ya ndege na Masogange alimwomba amsaidie kubeba mizigo hiyo, kwani ilikuwa mikubwa.
Kwa sheria za Afrika Kusini kubeba kemikali zozote ambazo zimepigwa marufuku ni kosa la jinai kisheria, hivyo mahakama iliamuru Masogange ahukumiwe kwenda jela kwa miezi 30 (miaka miwili na miezi mitano) au alipe faini ya R30, 000 (sawa na Sh4.8 milioni).
Hata hivyo, Kapteni Ramaloko alisema mdhamini wa Masogange alilipa nusu ya fedha na kwamba zinazobaki amalizie baadaye.
Alisema kutokana na kutomalizia kulipa fedha hizo ataendelea kubaki nchini humo hadi atakapomaliza kulipa nusu ya faini iliyobaki.
Masogange na mwenzake walipokamatwa na SARS ilielezwa walikuwa wamebeba dawa za kulevya aina ya
Methamphetamine, lakini Mahakama juzi ilithibitisha walikamatwa na kemikali aina ya Ephedrine, ambayo siyo dawa za kulevya.
Wakati Kamishna Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Geofrey Nzowa alipoulizwa na Mwananchi Jumamosi juzi alisema mzigo walioubeba Masogange na mwenzake haukuwa ni dawa za kulevya bali ni kemikali za dawa za kulevya, lakini Msemaji wa Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini, (SARS), Marika Muller alieleza kuwa timu ya SARS ina uhakika kuwa mabegi sita yaliyokamatwa Julai 5 ni dawa za kulevya aina ya Methamphetamine.Jana, Muller alipoambiwa kuwa Watanzania hao wameachiwa huru baada ya kulipa faini na mmoja kuachiwa huru kwa kuwa Mahakama imeridhika kuwa hazikuwa methamphetamine bali kemikali aina ya Ephedrine, alirudia tena na kueleza kuwa, mamlaka hiyo ina uhakika na kazi yake na iwapo mahakama imewaachia huru basi yeye hana la kusema zaidi.
"Kazi yetu kubwa ni kukamata mizigo haramu inayopitishwa uwanja wa ndege, kama Mahakama imeona kuwa si dawa za kulevya, hatuna la kuongeza. Kikubwa tumemaliza kazi yetu," alisema Muller kwa kujiamini.
Hata hivyo, Nzowa jana akizungumzia kuachiwa huru kwa Watanzania hao, alionyesha kushangazwa jinsi Mahakama ilivyotoa adhabu ndogo.
"Hii ni ajabu sana. Kama watu wamebeba mzigo wenye thamani ya Sh6.8 bilioni wanapigwa faini ya milioni nne, hawataogopa kufanya hiyo biashara. Hao watu ni hatari sana," alisema Nzowa.
Alipoulizwa iwapo wakirudi Tanzania wanaweza kushtakiwa, Nzowa alisema kitengo chake hakitaweza kuwashtaki tena kwa sababu wanaweza kujitetea kuwa tayari walishahukumiwa, isipokuwa Mwendesha Mashtaka aliyekuwa akisimamia kesi yao anaweza kukata rufaa.
"Iwapo Mwendesha Mashtaka wa huko akikata rufaa kwa kuona adhabu aliyopewa mhalifu huyo ni ndogo, anaweza kufanya hivyo," alisema Nzowa.
Nzowa alisema, inasikitisha kuwa wakati mapambano ya biashara hiyo yakiwa yanaendelea Tanzania, watuhumiwa hao wanaachiwa.
"Adhabu waliyopewa ni ndogo hasa wakati huu ambao Tanzania tunachafuka kwa tuhuma hizi. Lazima kitu kifanyike kubadili hali halisi hapa nchini," alisema.
Nzowa alieleza kuwa alikwenda Afrika Kusini tangu Septemba Mosi kuwahoji wasichana hao ambao hata hivyo hawakuweza kusema lolote la kuisaidia polisi.
Masogange aliandika kwa maandishi kuwa ni kweli mzigo ulikuwa wa kwake, lakini akasema mdogo wake, ambaye ni Melissa, hajui lolote na alikuwa amemsaidia.
Julai 5, mwaka huu Masogange na Melissa walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo wakidaiwa wamebeba kilo 150 zilizodaiwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye thamani ya Sh6.8 bilioni.
Dawa hizo zilizokuwa zimepakiwa katika mabegi makubwa sita, zinatajwa kuwa ni kiwango kikubwa kukamatwa katika historia ya SARS ndani ya uwanja huo unaotumiwa na mataifa makubwa duniani.Taarifa za kukamatwa kwa wasichana hao zilipamba kurasa mbalimbali za magazeti ndani na nje ya Tanzania, jambo lililosababisha Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kuchukua hatua za kuusafisha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.
Baada ya uchunguzi wa Dk Mwakyembe ambao ulibaini kuwapo mchezo mzima uliochezwa wakati Masogange na Melissa walipokuwa uwanja wa ndege.
Agosti 17 alitoa agizo la kufukuzwa kazi, Koplo Juliana Thadei, Jackson Manyoni, Yusuph Daniel Issa, Koplo Ernest na Mohamed Kalugwan.
Mwakyembe alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida mfanyabiashara ambaye hakuwa na tiketi ya kusafiri siku hiyo, baadaye alibadili mawazo hapohapo na kuamua kuondoka siku hiyo kwenda Afrika Kusini na kulipia faini ya dola 60 (Sh96, 000) ili kupata tiketi.
Pia Mwakyembe aliliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kumkamata mfanyabiashara anayedaiwa kumsaidia Masogange kusafirisha dawa za kulevya ambaye alitoweka na mabegi matatu ya dawa hizo huko Afrika Kusini:chanzo mwananchi.