Mafungu ya rushwa urais 2015 yapangwa



MBINU na mikakati kutoka katika baadhi ya kambi za watu wanaotajwa kuwania kuteuliwa kugombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) 2015, zimeendelea kuvuja, Raia Mwema likielezwa kwamba viwango maalumu vya rushwa vimekwishawekwa na sasa kinachoendelea katika baadhi ya kambi ni kukamilisha nakisi ya fedha za rushwa inayohitajika.

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka katika baadhi ya kambi zinazotarajiwa kuingia katika kinyang’anyiro hicho cha urais, vikao vinavyopewa kipaumbele kwa sehemu kubwa ya wajumbe wake kuhongwa ni vya aina tatu, kati ya vikao vinne muhimu vya CCM katika mchakato wa kuchuja wagombea.

Kwa kuzingatia utaratibu wa vikao vya CCM, vikao vinavyohusika ni pamoja na kikao cha Kamati ya Maadili, Kikao cha Sekretariati, Kikao cha Kamati Kuu chenye wajumbe 32, Kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kinachotajwa kuwa na wajumbe 374 na mkutano mkuu wa chama hicho, wenye wajumbe takriban 3,000.

Taarifa za uhakika za hivi karibuni ambazo hata hivyo hazikubainisha wafadhili au vyanzo vya fedha hizo, zinaeleza kwamba kati ya makundi yanayopania kuweka wagombea, baadhi wamekwishapiga hesabu maalumu kuhusu viwango vya rushwa ikielezwa kwamba, angalau kila mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM amepangiwa bajeti ya shilingi milioni 10 kila mmoja wakati kwa kila mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, amepangiwa kiwango cha shilingi milioni tano huku wajumbe wa mkutano mkuu, kila mmoja akipangiwa kiwango cha rushwa ya shilingi milioni tatu.

Hata hivyo, chanzo hicho cha habari kimekejeli mipango hiyo kikieleza ya kuwa umakini zaidi utazingatiwa pindi wakati utakapowadia na udhibiti wa rushwa utakuwa wa kiwango cha juu kuliko ilivyopata kutokea katika chaguzi zilizotangulia.

Lakini kutokana na mkakati huo, na hasa kama utafanikiwa rushwa hiyo inatajwa kuweza kuwa ya kiwango kikubwa zaidi kuwahi kutumika katika kinyang’anyiro cha kupitisha wagombea wa CCM katika ngazi ya urais, huku kundi husika likijigamba kwamba 2015 ni lazima mgombea wao apitishwe na chama hicho kwa gharama yoyote.

Hali hiyo inajitokeza katika wakati ambao masuala ya kisiasa nchini yakigharimu mamilioni ya fedha, kuanzia katika uchaguzi ndani ya vyama vya siasa, uchaguzi wa kitaifa na hata uchaguzi katika chaguzi ndogo, zikiwamo za ubunge.

Kwa mfano, katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, mkoani Arusha uliofanyika baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Jeremiah Sumari, inadaiwa kwamba, CCM kilitumia takriban shilingi milioni 800 huku mmoja wa viongozi wakuu aliyekuwa akimuunga mkono mmoja wa wagombea wa ubunge katika uchaguzi huo, akitumia zaidi ya shilingi bilioni moja kando ya bajeti ya chama chake, ili kufanikisha ushindi wa huyo aliyekuwa akimuunga mkono.

Mbali na Arumeru, chaguzi nyingine zilizopata kutafuna mamilioni ya fedha ni uchaguzi mdogo wa Igunga, mkoani Tabora ambako mmoja wa wagombea kupitia chama chake alitumia bajeti ya shilingi zisizopungua milioni 800 huku wa vyama vingine wakitajwa kutumia kiwango pungufu cha hicho lakini kisicho chini ya shilingi milioni 400,000.

Wakati hali ya kujipanga kwa kutumia rushwa ili kushinda kinyang’anyiro cha uteuzi ndani ya CCM ikiwa hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Philip Mangula amekwishanukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini, mara baada ya kushika wadhifa huo, akijigamba kudhibiti majaribio yote ya rushwa ndani ya chama hicho hasa yanayolenga kujipatia ushindi katika nafasi za uteuzi.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanaamini kasi ya Mangula katika kudhibiti wimbi hilo la rushwa linalotarajiwa kuzidi mwaka 2015 ni ndogo, wakirejea ahadi yake kwamba angedhibiti waliotumia rushwa kushinda katika nafasi mbalimbali za uchaguzi wa ndani ya chama hicho. Mangula alitoa miezi sita ili kukamilisha ahadi yake hiyo lakini pamoja na miezi hiyo kupita, hakuna uamuzi ulio wishafanyika, kinyume cha ahadi yake.

Tayari viongozi mbalimbali nchini wamekwishawahi kulalamika kuhusu kuwapo kwa matumizi makubwa ya fedha katika uchaguzi kiasi cha wakati fulani Rais Jakaya Kikwete kushawishi kutungwa kwa sheria ya gharama za uchaguzi ambayo hata hivyo, imekuwa na kasoro kadhaa na utekelezaji wake haujatoa matokeo mazuri.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company