HABARI ZETU
Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais Jakaya Kikwete na vyama vya siasa katika mazungumzo yao Ikulu, jijini Dar es Salaam Oktoba 15, mwaka huu, yamezua safari mpya na ngumu ya kuelekea katika kupata muafaka wa pamoja kuhusiana na Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Hali hiyo imedhihirika baada ya vyama vyote vya siasa nchini, vikiwamo vyenye uwakilishi na visivyokuwa na uwakilishi bungeni kukutana jana jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kuipata Katiba mpya katika mazingira ya maridhiano ya kitaifa.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na viongozi wakuu wa vyama hivyo, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Philip Mangula, kilifanyika jana chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Wengine ni Profesa Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti CUF), Dk. Willibrod Slaa (Katibu Mkuu-Chadema), Tundu Lissu (Mkurugenzi wa Katiba na Sheria-Chadema), Isack Cheyo (aliyemwakilisha Mwenyekiti wa UDP) na Nancy Mrindoko (aliyemwakilisha Mwenyekiti wa TLP).
Walikuwapo pia Khamsi Ambari (Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Zanzibar), Fahmi Dovutwa (Mwenyekiti UPDP), Mng’ong’o (NCCR-Mageuzi na Evod Mmanda (Mwanasheria kutoka CCM).
Mbatia, ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, aliliambia NIPASHE muda mfupi baada ya kikao hicho jana kuwa, kikao chao kilizingatia makubaliano yaliyofikiwa kati yao na Rais Kikwete, Ikulu.
Alisema makubaliano hayo ni pamoja na vyama vyote kukaa meza moja na kufikia maridhiano ya kutanguliza mbele maslahi ya Taifa chini ya kaulimbiu ya “Tanzania Kwanza” kabla ya kitu kingine chochote, zikiwamo itikadi na tofauti za kisiasa.
Alisema mbali na hilo, katika mazungumzo na Rais Kikwete, Ikulu, pia walikubaliana kupanua wigo zaidi wa kuboresha mchakato wa mabadiliko ya Katiba, badala ya vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi pekee kama ilivyokuwa awali.
Hiyo ni pamoja na kuwa na mchakato shirikishi usiokuwa na ubabe.
Mbatia alisema badala ya maboresho hayo kufanywa na vyama hivyo vitatu pekee, walikubaliana kushirikisha vyama vyote ambavyo ni wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ikiwamo CCM.
Vyama vingine, ambavyo walikubaliana vishirikishwe pia katika suala hilo ni vile visivyokuwa na uwakilishi bungeni, ambavyo vilihudhuria katika kikao cha jana.
Vyama hivyo ni UMD, NLD, UPDP, NRA, Tadea, Demokrasia Makini, Chausta, DP, APPT-Maendeleo, Jahazi Asilia, Sau, AFP, CCK, ADC na Chaumma.
Kwa mujibu wa Mbatia, katika kikao cha jana, vyama hivyo viliwakilishwa na UPDP.
“Ndiyo tunajadiliana. Tulichojadiliana ni kuandaa maridhiano ya kitaifa kabla ya Bunge la Katiba,” alisema Mbatia na kuongeza kuwa baada ya majadiliano hayo watatoa taarifa kwa umma walivyoafikiana.
Alisema kikao kama hicho kilifanyika pia Alhamisi ya wiki iliyopita.
Vikao hivyo vimefanyika siku sita baada ya Rais Kikwete kukutana na viongozi wa vyama sita vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, Ikulu, jijini Dar es Salaam na kukubaliana mambo makuu mawili.
La kwanza, vyama vyote vya siasa vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013, kuyawasilisha haraka serikalini ili kutafuta namna ya kuyashirikisha katika marekebisho ya sheria hiyo.
La pili, vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato mabadiliko ya Katiba ya nchi kwa maslahi mapana ya nchi na mustakabali wa taifa.
Katika makubaliano hayo, TCD kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi ulimalizika kwa pande mbili hizo kukubaliana mambo hayo.