Ndugu zangu,
Ni rahisi kwa Rais wa Afrika kuchomoka na Mwananchi kuliko kuchomoka na Mo Ibrahim!
Naam, dola milioni tano za Mo Ibrahim hazichomokeki kirahisi isipokuwa ' zinawachomea' Marais wa Kiafrika hasa wale wenye kutenda maovu au wenye kudhamiria kuyatenda maovu kwa watu wao.
Tangu kuasisiwa kwa tuzo hiyo mwaka 2007 ni Marais watatu tu wastaafu wa Kiafrika waliochomoka na tuzo hiyo; Chissano wa Msumbiji, 2007, Festus Mogae wa Botswana, 2008 na Pedro Verona Pires wa Cape Verde, 2011.
Hakuna Rais aliyechomoka na tuzo hiyo mwaka 2009, 2010 na 2012. Wakati umefika kwa tuzo hiyo kutolewa hata kwa viongozi wa Kiafrika wasio Marais. Maana, Afrika ina viongozi wengi wenye kustahili tuzo lakini hawataki kuwa Marais.
Na mwaka huu nao hola ama patupu, hakuna Rais aliyechomoka!
Tatizo? Ni kubwa, Marais wengi Afrika hawaamini kwa dhati katika demokrasia ikiwamo Utawala Bora na kuheshimu Haki za Binadamu.
Na Botswana ni nchi ya kupigiwa mfano Afrika. Inajitahidi sana kwenye kujenga demokrasia na kuheshimu Haki za Binadamu. Si ajabu, ndio nchi ya Kiafrika ambayo haikupiga kura yake kuunga mkono maazimio ya AU dhidi ya ICC- Mahakama ya Uhalifu Duniani.
Na majuzi hapa kwa Marais wengi wa Afrika kuishupalia ICC- Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ni sawa na kusema kuwa, kuna wengi wameshashindwa kigezo cha kuchomoka na tuzo ya Mo Ibrahim wakitoka madarakani.
Maana, ICC ni moja ya dhamana kubwa kwa Waafrika kuwa viongozi wao wanaweza kuingiwa hofu ya kuwafanyia vitendo vya kihalifu. Maana, kiongozi wa Kiafrika akifunguliwa jalada kule The Haugue, basi, atasakwa na iko siku atakamatwa na kusimama kizimbani. Tumeyaona ya akina Taylor na wengine.
Ndio, kama kiongozi, ICC inatoa ujumbe kuwa, mathalan, huwezi leo ukaanzisha kikundi cha Wanamgambo na kuwatendea uhalifu raia katika nchi unayodai unaiongoza halafu ukabaki unatanua.
Popote pale utakapojificha, ICC watahakikisha ' Wanakuchomoa' na ' kukuchomeka' kizimbani ujibu mashataka ya uhalifu uliotenda.
Na hapo ndio utakuwa ' Umechomeka' kwa uhalifu wako.
Siku Njema.
Maggid.