Kiongozi wa Muungano wa Upinzani nchini Syria Ahmad Jarba
Reuters
Na
Martha Saranga AminiMuungano wa Upinzani nchini Syria unasema kuwa utahudhuria tu mazungumzo ya amani jijini Geneva nchini Uswizi ikiwa rais Bashar Al Assad ataondoka madarakani.
Kiongozi wa muungano huo Ahmad Jarba amesema kuwa hawawezi kuketi katika meza moja na rais Assad au wawakilishi wake ambao anawatuhumu kusabisha umwagaji damu nchini Syria.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza William Hague ameusihi upinzani kukubali kuhudhuria mazungumzo hayo na kusisitiza kuwa rais Assad hawezi kushirikishwa kwa lolote kwa kile alichokieleza kuwa amepoteza uhalali wa kuwa kiongozi wa Syria.
Mawaziri wa Mambo ya nje kutoka nchi za Magharibi walikutana na viongozi wa muungano wa upinzani nchini Syria jumanne jijini London nchini Uingereza kujadili harakati za kurejelewa kwa mazungumzo ya amani ambayo bado hayajahamika yatafanyika lini.
Wachambuzi wa siasa za Kimataifa wanaona kuwa bado mazungumzo ya Geneva ni muhimu kwa upatikanaji wa suluhu la kisiasa nchini Syria.
Utawala wa raisi wa Syria Bashar al Assad umeendelea kulaumiwa kusababisha mauaji ya raia na kufanya mashambulizi kwa silaha zenye kemikali.