Ubalozi wa Marekani na Uganda watahadharisha shambulizi la ugaidi tena.

Serikali ya Uganda ipo makini kuzuia uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi kama yaliyotokea Westgate
Msemaji wa serikali ya Uganda anasema ubalozi wa Marekani unashirikiana habari za kijasusi na utawala nchini Uganda kuonya uwezekano wa shambulizi la kigaidi kama lile lililotokea kwenye jengo la Westgate nchini Kenya mwezi mmoja uliopita. Katika kujibu tukio la aina hiyo, Ofwono Opondo anasema serikali ya Rais Yoweri Museveni imeziweka katika hali ya tahadhari ya juu idara zote za usalama.

“Tumechukua hatua za ziada za usalama. Tumepeleka wafanyakazi wanaovaa sare na wasio na sare katika maeneo makuu ya serikali yenye harakati nyingi na wilaya za biashara siyo kampala peke yake, lakini kote nchini”, alisema Opondo. “Tunapeleka ilani ya tahadhari kwa umma kuwa makini hasa katika maeneo ambayo mara kwa mara yanatembelewa na watu wengi”.

Onyo la ubalozi wa Marekani limekuja takribani mwezi mmoja baada ya wanamgambo waliposhambulia eneo la Westgate lenye maduka ya kifahari nchini Kenya na kusababisha vifo vya watu 67 na majeruhi kadhaa. Kundi lenye msimamo mkali la al-Shabab la nchini Somalia lilidai kuhusika na shambulizi.

Opondo anasema maafisa waandamizi wa usalama wanatathmini hatua za kuhakikisha wamejiandaa vya kutosha kuzima mashambulizi ya aina yeyote. Anasema usalama umeongezwa katika vituo vya usafiri wa umma ambavyo vitaweza kuwa “walengwa wa karibu” kwa magaidi.

“Kwenye milango mikuu ya kuingilia ya vituo vya abiria wa umma vya taxi na mabasi kuna ukaguzi wa ziada wa watu, mizigo na magari”, alisema Opondo. “Tunashauri kwa kila mtu kutoa ushirikiano kwenye vituo vya usalama ambavyo vimewekwa, kusudi kasoro isijitokeze”.

Anasema serikali imeanzisha kampeni kwenye vyombo vya habari ikiutaka umma kuwa katika tahadhari na kuwasiliana na maafisa wa usalama juu ya harakati zozote zenye kutia shaka.


Kundi la wanamgambo wa al-Shabab

Kundi la al-Shabab tayari limedai kuhusika na shambulizi nchini Uganda wakati wa michuano ya kombe la Dunia mwaka 2010. Kundi hilo lilisema yalikuwa majibu kwa nchi hiyo kutoa msaada wa kijeshi kwa AMISOM, majeshi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia. Opondo anasema Uganda haitaondoa majeshi yake kutoka nchi hiyo iliyopo Afrika mashariki licha ya vitisho kutoka kwa al-Shabab.

Anasema idara za usalama nchini humo zimeweza kuzuia majaribio ya mashambulizi ya kundi la wanamgambo wenye silaha kutoka Somalia tangu mwaka 2010.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company