Ripoti iliyotolewa na taasisi moja ya kimataifa kuhusu utumwa mamboleo imefichua kwamba karibu watu milioni 30 kote duniani wanaishi katika utumwa.
Ripoti iliyotolewa leo na jumuiya ya Walk Free Foundation (WFF) imesema kuwa watumwa hao ama husafirishwa kwa njia za magendo katika mipaka ya nchi mbalimbali, kulazimishwa kufanya kazi au hata huzaliwa wakiwa utumwani.
Ripoti hiyo imesema karibu nusu ya watumwa hao iko India ambayo inafuatiwa na nchi ya Mauritania huko Magharibi mwa Afrika. Imesema asilimia 4 ya raia wa Mauritania wanaishi katika utumwa. Ripoti hiyo inaitaja Mauritania kuwa ni taifa lenye utumwa mkubwa wa kurithi ambako watu walioko kwenye utumwa wanaweza kuuzwa na kununuliwa, kukodishwa na hata kutolewa kama zawadi.