
Simanzi na vilio jana vilitawala wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi aliyefariki dunia kwenye Hospitali ya Milpark nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu.
Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal aliwaongoza viongozi mbalimbali wakiwemo Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wastaafu, mawaziri, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dini, kuuaga mwili wa Dk Mvungi kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.
Watu wengi waliowasili katika viwanja hivyo saa 3:00 asubuhi walionekana wenye huzuni, huku wakikaa katika makundi wakizungumza kwa sauti za chinichini.
Ilipofika saa 4:00 asubuhi, mvua ilianza kunyesha na kuwalazimisha watu waliokuwa wametawanyika katika eneo hilo kuanza kutafuta sehemu ya kujificha.
Dakika tatu baadaye wakati mvua ikiendelea kunyesha, gari lililokuwa limebeba mwili wa Dk Mvungi liliwasili kwenye viwanja hivyo, kitendo kilichowafanya baadhi ya waombolezaji kuanza kutokwa machozi.
Mara baada ya mwili kuwekwa sehemu iliyokuwa imeandaliwa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Paramagamba Kabudi alipanda jukwaani kusoma historia ya marehemu.
Kabudi alisema Dk Mvungi alikuwa mtu aliyechukia rushwa na kuheshimu utawala bora, na kwamba kifo chake kimewaunganisha pamoja watu wa itikadi tofauti.
Aliongeza kuwa kutokana na uzalendo aliokuwa nao kwa nchi yake, Dk Mvungi alipomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), baada ya kumaliza elimu ya sekondari, aliendelea kuvaa magwanda hayo alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi yalipochakaa.
Aliongeza kuwa, Dk Mvungi ambaye pia alikuwa mwanasheria maarufu nchini, alishiriki kubadilisha mfumo wa masomo ya sheria vyuo vikuu baada ya kuanzisha utaratibu wa kusoma shahada ya sheria kwa miaka minne tofauti na mitatu ya awali.
"Mwaka 1998 aliitisha kikao mjini Arusha na kushawishi kubadili shahada ya sheria kutoka miaka mitatu ya awali hadi minne ya sasa," alisema.
Akizungumzia uamuzi wa Dk Mvungi kugombea kiti cha urais mwaka 2005, Kabudi alisema kwamba Mvungi hakugombea kiti hicho kwa sababu alikuwa anajua angeshinda au alikuwa anamchukia rais aliyekuwa madarakani wakati huo, bali alitaka kushiriki ndiyo maana aliposhindwa alikuwa wa kwanza kukubali matokeo.
Akiongoza misa ya kuuaga mwili wa marehemu, Padri Monsinyori Deogratius Mbiku alisema kuwa Dk Mvungi ameshakamilisha kazi yake hapa duniani, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha anatekeleza majukumu aliyopewa.
"Kila siku kamilisha wajibu wako, usiache kiporo. Wajenzi wanasema zege halilali, kwa hiyousilale bila kukamilisha wajibu wako, nani anayekwambia utaishi kesho?" alihoji Mbiku.
Viongozi watoa salamu
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia huku akionekana kuwa na huzuni nyingi, alisema familia ya Dk Mvungi inajiuliza kwa nini baba yao alikufa kwa kifo cha aina hiyo.
"Tunajua kuwa kila nafsi itaonja mauti, lakini familia ya Mvungi inajiuliza kwa nini itokee hivi?" alihoji na kuongeza kuwa kifo cha Mvungi ni mwendelezo wa matukio ya mauaji yanayofanana kwenye sekta ya sheria hapa nchini.
Alisema Profesa Jwani Mwaikusa na Wakili Michael Wambari, nao walikufa katika mazingira ya kutatanisha na kuiomba Serikali kuongeza ulinzi kwa wananchi wake.
"Hao wengine nao waliondolewa duniani kikatili na kinyama hivihivi. Ulinzi na usalama wa taifa inabidi ulindwe kwa gharama yoyote, badala ya kulalamika tutekeleze wajibu wetu," alisema.
Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, aliongeza kuwa marehemu Dk Mvungi alitumia muda wake mwingi kutetea haki za binadamu, lakini wale aliowatetea kwa kujua au kutokujua ndiyo waliotoa roho yake.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko, Jaji Joseph Warioba akizungumza kwa taabu kutokana na simanzi alisema kwamba kifo cha Dk Mvungi kimeacha pengo la zaidi ya mtu mmoja ndani ya tume hiyo, kwa sababu alikuwa na mchango mkubwa.
"Kwa hali ya kawaida inaonekana ni mtu mmoja amepotea, siyo hivyo, huyu mtu alikuwa na mchango mkubwa," alisema.
Pia aliongeza kwamba Dk Mvungi aliisaidia tume hiyo kufanya utafiti mbalimbali uliokuwa unahusu katiba na hata siku aliyovamiwa na kujeruhiwa kuna utafiti alikuwa ametoka kuumalizia.
"Kabla ya mkasa huo, Ijumaa alikuwa ameomba afanye utafiti ambao angeukabidhi Jumatatu, lakini alipoondoka ndiyo ilikuwa mwisho wa kuonana," alisema Warioba.
Aliwataka wananchi kumkumbuka Dk Mvungi kwa kupata Katiba Mpya kwa njia ya maridhiano ambayo marehemu aliitumia wakati wa uhai wake.
Makamu wa Rais
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, akiwasilisha salamu za Rais Jakaya Kikwete, alisema Dk Mvungi alikuwa msomi mahiri, mwenye mapenzi na nchi yake ndiyo maana alichaguliwa kuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kama alivyokuwa amependekezwa na chama chake.
"Ametoka wakati anahitajika sana, chama kimepoteza mwanachama wa kutumainiwa pengo lake haliwezi kuzibwa," alisema.
Msajili wa Vyama vya Siasa
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliwataka Watanzania kumuenzi Dk Mvungi kwa kudumisha utaifa na kumaliza mchakato wa Katiba Mpya kwa amani.
"Pia, tusitafute mchawi kwa kuwa tayari Serikali inafanya kazi yake, tuchukulie msiba huu kuwa ni ishara ya kutuweka pamoja," alisema.
Mkuu wa Chuo cha Bagamoyo
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UB), Profesa Costa Mahalu alisema marehemu alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa chuo hicho, hivyo wameamua kulipa jengo moja jina lake.
Profesa Lipumba
Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba alimtaja Dk Mvungi kama mpambanaji aliyetanguliza masilahi ya taifa, ndiyo maana hata aliposhindwa uchaguzi wa urais 2005 alikuwa wa kwanza kukubali matokeo.
Baada ya uchaguzi vyama vilivyoshindwa viliamua kufungua kesi ya kupinga matokeo ambapo Dk Mvungi na Dk Masumbuko Lamwai walichaguliwa kuwa mawakili wao.
"Baada ya matokeo mwenzetu alikubali matokeo, lakini sisi wengine tulijiona ni marais wachakachuliwaji...tulihangaika na ile kesi lakini ilikufa baada ya Dk Lamwai kuingia mitini," alisema.
Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema Dk Mvungi alisimamia alichokiamini bila kumwogopa yeyote na kwamba kifo chake kinawakilisha watu wengi waliofariki dunia kwa namna hiyo.
Edward Lowassa
Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa amesema kifo cha Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dk Sengondo Mvungi kimeacha pengo kubwa katika upatikanaji wa Katiba Mpya na ujengaji wa misingi ya demokrasia.
Akitoa salamu zake za rambirambi kwa Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia, alisema Dk Mvungi alikuwa mojawapo ya nguzo zilizokifanya chama hicho kuonekana kutokurupuka katika kutoa hoja za kuikosoa serikali.
"Kuondoka kwake ni pigo kubwa kwa maendeleo na uimara wa demokrasia nchini kwa kuwa alikuwa mtu mwenye mawazo ambayo yaliifanya NCCR-Mageuzi kuwa chama kisichokurupuka katika utoaji wa hoja za kuikosoa serikali," alisema Lowassa na kuongeza
Mwigulu Nchemba Akizungumza kwa niaba ya CCM, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Mwigulu Nchemba alisema nchi imekumbwa na roho ya mauaji na kwamba analaani matukio ya kutoa uhai watu wasio na hatia.
www.hakileo.blogspot.com