TAARIFA KWA UMMA
KUKOMA/KUSIMAMISHWA KUWA KIONGOZI KWA MWENYEKITI WA WILAYA YA BUMBULI ndugu ABDI SHEKIMWAGA
CHADEMA Kanda ya Kaskazini, inawatangazia umma wote kuwa, Ndugu ABDI SHEKIMWAGA amesimamishwa kuwa mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Bumbuli kuanzia 21 Desemba 2013.
Ofisi ya kanda, ilipokea nakala ya taarifa na miniti ya kikao kilichoketi tarehe 22 septemba 2013 kutoka kamati tendaji ya wilaya/jimbo pamoja na nakala ya barua ya tuhuma alizoandikiwa ndugu ABDI SHEKIMWAGA ili ajieleze na kujibu, ikiwemo na barua ya tarehe 12 Desemba 2013 aliyoandikiwa katibu wa mkoa kujulishwa mapendekezo na hatua za kunusuru chama dhidi ya hila mbaya zilizokuwa zinafanywa na ABDI SHEKIMWAGA. Kwa bahati mbaya sana ndugu SHEKIMWAGA alitoa maneno ya kashfa na dharau pamoja na kutumia lugha isiyofaa kwa viongozi na kuamua kugoma kujibu barua ya tuhama hizo.
Uongozi wa Kanda baada ya kupitia taarifa hizi na baada ya kufanya kikao cha pamoja na viongozi wa wilaya tarehe 21 Desemba 2013 huko wilaya lushoto mkoani Tanga, unamtangaza ndugu SHEKIMWAGA kuwa kwa kukinisuru chama dhidi ya tuhuma dhidi yake, kwa ajili ya kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, kwa ajili ya hofu na kutokuwa na imani kulikoonyeshwa na viongozi na wanachama wenzake AMESIMAMISHWA KUWA MWENYEKITI WA CHAMA KUANZIA TAREHE 21 DESEMBA 2013. Hatua hii ni ya kuzingatia pendekezo la kamati tendaji ya wilaya/jimbo kwa mujibu wa ibara ya 6.3.4 (c), “amekoma kuwa kiongozi kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa masharti ya katiba, kanuni na maadili ua chama”.
Aidha uongozi wa kanda, unaliagiza baraza la uongozi la mkoa ambayo ndio mamlaka ya nidhamu kwa wilaya/jmbo kwa mujibu wa katiba ya chama ibara ya 6.3.6 (a) sehemu (iV) kuwa ndugu ABDI SHEKIMWAGA APEWE FURSA NYINGINE TENA akiwa katika hali ya kusimamishwa uongozi kwa kuandikiwa barua tena ya tuhuma dhidi yake na apewe muda wa kikatiba kujibu ama sivyo hatua kali zichukuliwe dhidi yake.
Tuhuma hizo ni;
Kuamua kwa makusudi kuzuia na kukwamisha kazi za CHAMA, programu ya CHADEMA ni msingi. Ndugu SHEKIMWAGA ametoa maneno ya uzushi na upotoshaji kwa uwazi mbele ya viongozi wenzake na maafisa wa kanda kuwa hayuko tayari kufanya kazi ambayo yeyé aliitafsiri kuwa ina lengo la kumjengea mtu fulani mtandao ndani ya chama. Hii ni kinyume na kanuni ya maadili ya kiongozi na uendeshaji wa kazi za chama sura ya 10.1 (viii)
Ametoa lugha na matamshi yenye kuonyesha udini na ukabila mbele ya viongozi wenzake na mbele ya maafisa wa kanda kuwa kaimu katibu wa CHADEMA mkoa wa Tanga ndugu Jonathan Leonard Baweje kuwa ni Mkristo na ametokea mkoa wa Kigoma hivyo hawezi kuwa katibu wa mkoa wa Tanga kwa sababu sio muislam. Hii ni dhambi mbaya sana na ni kinyume na kanuni ya maadili ya kiongozi na uendeshaji wa kazi za chama sura ya 10.1 (iv), “Kiongozi yoyote asijihusishe na vikundi vyovyote vyenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya chama au miongozi mwa jamii kisiasa au kijamii”.
Amejitambulisha wazi mbele ya viongozi wenzake na mbele ya maafisa wa kanda kuwa yeyé yupo kundi la Zito Kabwe na atahakikisha CHADEMA inakufa Bumbuli iwapo maamuzi ya kamati kuu ya kumvua uongozi Zito Kabwe hayatabadilishwa. Kitendo hiki cha kujitengenezea makundi na upotoshaji ni kinyume na kanuni ya maadili ya kiongozi na uendeshaji wa kazi za chama sura ya 10.1. (iv), “Ni mwiko kwa kiongozi kujihusisha na upotoshaji wa maamuzi halali ya vikao vya chama”.
Amezuia kwa makusudi kazi za chama na amekuwa akifanya hujuma dhidi ya viongozi wengine ambao wamekuwa wakifanya kazi za chama. Sambamba na hili ametuhumiwa kuwa anashirikiana na wapinzani wetu CCM katika kuhujumu chama na kwa kumwaga sumu na maneno ya uongo. Kitendo hiki kimekuwa sababu ya kuzuka kwa migogoro isiyokwisha katika jimbo la bumbuli na imeendelea kuvunja moyo na kuleta mifarakano inayorudisha nyuma kazi za chama. Jambo hili ni kinyume na kununi ya maadili ya uongozi na uendeshaji wa kazi za chama sura ya 10.1 (ix), “Kiongozi asijihusishe au kushiriki na vikundi au vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake”.
Taarifa hii inaenda sambamba na ndugu ABDI SHEKIMWAGA kukabidhi vifaa vyote vya chama, ikiwemo kadi za chama mpya zipatazo 400 zenye thamani ya Tshs 600,000 ndani ya siku TATU kuanzia tarehe ya taarifa hii kwa KATIBU WA CHADEMA MKOA WA TANGA.
CHADEMA Kanda ya Kaskazini inaendelea kuonya kuwa haitavulia kabisa kuona CHAMA CHETU ambacho ni tumaini kwa Watanzania wengi kikivurugwa na watu wachache wenye hila mbaya na chafu. Aidha nitoe rai kwa WanaCHADEMA wote wa kanda ya kaskazini na Watanzania wapenda haki na kweli wasiwe na hofu yoyote na matukio haya ya kukisafisha chama maana hatuna budi kusafisha na kufukuza bundi wote waondoke.
Imetolewa leo tarehe 23 Desemba 2013
Amani Golugwa
Katibu wa CHADEMA – KANDA YA KASKAZINI.
Makao Makuu ya Kanda – Arusha, Tanzania:
Simu:
+255 754 912 914