Baada ya Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara ((TNBC) uliofanyika tarehe 16 Desemba 2013, chini ya uenyekiti wa Mhe. Rais, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, sikutegemea kwamba Mhe. Profesa Muhongo angeendeleza mashambulizi dhidi yangu kwa sababu katika mkutano huo ambao ulikuwa na mafanikio makubwa tulifikia maamuzi ya kudumisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi, kitu ambacho nimekuwa nikipigania. Hivyo basi, kauli ambazo Mhe. Profesa Muhongo amezitoa Bungeni tarehe 19 Desemba 2013, zimenishtua na kunisikitisha sana.
Ningependa kuwaeleza Watanzania wenzangu yafuatayo.
Profesa Muhongo ni muongo
Imefika wakati wa Watanzania kubaini kwamba Mhe. Profesa Muhongo ni mtu mwenye hulka ya kusema uongo. Kwa mfano:
1. Kwenye kongamano la tarehe 8 Desemba 2013, Mhe. Profesa Muhongo alisema kwamba moja ya kazi yake, alipokuwa akifanya kazi kama mwanasayansi huko nje, ilikuwa kutabiri umuhimu wa sayansi katika uchumi wa dunia miaka 3,000 ijayo. Huu ni uongo wa mchana kweupe.
2. Mnamo Julai 2012 Mhe. Profesa Muhongo aliwaahidi Watanzania kwamba hakutakuwa na mgawo wa umeme tena. Sote tunashuhudia mgao wa umeme ukiendelea hadi sasa.
3. Mnamo mwezi Septemba 2012, Mhe. Profesa Muhongo alinukuliwa akizungumzia mikataba ianayohusiana na vitalu vya gesi akisema kwamba “baadhi ya mikataba ni ya ovyo, na inahitaji kuvunjwa” na “sitovumilia mikataba ambayo haina maslahi kwa nchi na inawanufaisha wachache”. Baada ya hapo, Mhe. Profesa Muhongo aliamrisha Bodi mpya ya TPDC kusitisha ugawaji wa vitalu vya gesi uliopangwa kufanyika mwezi huo na kupitia upya mikataba yote iliyokuwepo awali. Sasa zaidi ya mwaka umepita na Mhe. Profesa Muhongo hajarekebisha mkataba hata mmoja.
Profesa Muhongo na takwimu zake za maeneo ya madini
1. Tarehe 8 Desemba 2013, alipokuwa anajibu swali la Mhe. Tundu Lissu kuhusu ni nani anamiliki migodi ya Tanzania, Profesa Muhongo alitoa takwimu za kuonyesha kwamba mimi ninamiliki eneo kubwa mara tatu ya Dar es Salaam kupitia kampuni zangu tanzu.
2. Jumapili iliyopita mimi nilimjibu Mhe. Profesa Muhongo kwa kumueleza kwamba takwimu zake kuhusu mimi ni za uongo, na vilevile hizo alizotoa Bungeni pia ni za uongo na nilimweleza kwamba swali la Mhe. Tundu Lissu lilikuwa ni “nani anamiliki maeneo ya migodi”.
3. Katika eneo la kutafuta madini unaweza ukapata au ukakosa – ni bahati nasibu, ndiyo maana maeneo ya utafutaji yanakuwa makubwa. Vilevile wakati unatafuta madini shughuli nyingine za wananchi waliopo katika eneo hilo huwa zinaendelea, kwa mfano kilimo, makazi, uchimbaji mdogo mdogo nk. Unapopewa leseni ya mgodi inamaana kwamba tayari umeshapata bingo – madini yapo na unaanza kuchimba. Kwa mantiki hiyo maeneo ya migodi inakuwa midogo – isiyozidi kilomita 10 za mraba, na shughuli zote za wananchi katika eneo hilo zinasitishwa.
4. Sasa kwenye maelezo yangu ya Jumapili iliyopita nilitamka wazi kwamba mimi ninamiliki kwa ubia na Watanzania wenzangu mgodi mmoja tu wa uchimbaji wa madini ya Tanzanite wenye eneo lisilofikia hata kilomita moja ya mraba. Profesa Muhongo hajakanusha hili, badala yake anaturudisha Watanzania kule kule kwenye maeneo ya utafutaji badala ya migodi.
5. Siyo hilo tu. Mhe. Profesa Muhongo anafahamu kwamba kuna aina 6 za leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini. Lakini kwa makusudi kabisa Mhe. Profesa Muhongo anafananisha leseni ya Mtanzania anayetafuta au kuchimba kokoto na leseni ya mwekezaji wa kigeni anayetafuta au kuchimba urani au dhahabu. Kweli unaweza kufananisha kokoto na dhahabu?
6. Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa utafutaji madini (mineral prospecting) ndiyo msingi wa maendeleo ya sekta ya madini kwa sababu bila utafutaji hakuna ugunduzi na uendelezaji wa migodi hapa nchini. Lakini kuanzia Julai mwaka jana Waziri Muhongo alipandisha tozo za vitalu kwa asilimia kati ya 100 na 500. Matokeo yake Watanzania wengi wanarudisha leseni zao na kasi ya ugunduzi wa migodi imepungua.
7. Nia ya mtu inajionyesha siyo tu kwa yale anayosema lakini bali pia kwa yale anayoacha kusema. Sasa kama kweli nia ya Mhe. Profesa Muhongo ni nzuri, kwa nini hatoi takwimu zinazohusu gesi? Kwa mfano, kwa nini hawaambii Watanzania kwamba:
a. Eneo ambalo limeshatolewa kwa ajili ya mafuta na gesi lina ukubwa wa kilomita za mraba 243,000 ambalo ni sawa na karibu robo ya eneo la Tanzania nzima au mara 175 ya eneo la mkoa wa Dar es Salaam au eneo la mikoa 9 ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Shinyanga na Kagera.
b. Kwa nini Mhe. Profesa Muhongo hataki kuwaambia Watanzania kwamba hakuna hata mzawa mmoja anayemiliki kitalu cha kutafuta au kuchimba mafuta na gesi?
c. Kwa nini Mhe Profesa Muhongo hataki kuweka wazi kwamba vitalu vyote 27 vya gesi ambavyo vinaanzia katika mpaka wetu na Kenya hadi mpaka wetu na Msumbiji, vimegawiwa kwa wageni? Je, kugawa vitalu vyote vya gesi kwa wageni siyo hatari kwa mustakabali wa usalama wa taifa letu?
d. Lakini cha muhimu ni kwamba Watanzania wafahamu kwamba gesi ambayo imeshagunduliwa Tanzania inakadiriwa kuwa na thamani ya US$ 500 bilioni wakati dhahabu yote iliyokwishagunduliwa hadi sasa na bado haijachimbwa inakadiriwa kuwa na thamani ya US$ 60 bilioni kwa bei ya sasa ya dhahabu.
Kwanini Profesa Muhongo hawaambii Watanzania takwimu hizi?
Profesa Muhongo na kauli zake kwamba Watanzania hawawezi kushiriki katika mchakato wa mafuta na gesi