HOTUBA YA ZITTO ALIYOITOA KIGOMA LEO BAADA YA MAPOKEZI,awasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu, uzalendo na uwajibikaji.



Leo nina furaha kubwa sana kwani baada
ya safari ndefu na yenye changamoto
nimerudi nyumbani kuwasalimu wananchi
wenzangu! Na hii si salamu za kawaida
bali nawasalimu kwa salaam za
demokrasia, uadilifu, uzalendo na
uwajibikaji.
Nawasalimu si kama mbunge bali kama
mwana wenu wa Kigoma! Na popote
niendapo najivunia kujitambulisha kama
Mtanzania; kama mwenyeji wa mkoa wa
Kigoma na zao la Ujiji.
Tuna mengi ya kujivunia kama taifa lakini
Ujiji na watu wake mna nafasi ya pekee
katika historia. Watu wa Ujiji mlipokea
harakati za kudai uhuru wa nchi yetu
mapema kabisa mapambano ya uhuru
yalipoanza. Watu wa Ujiji mlikuwa wa
kwanza kabisa kupokea mfumo wa vyama
vingi mwaka 1992. Na Jimbo la Kigoma
Mjini ilikuwa miongoni mwa majimbo ya
mwanzo kabisa kutoa mbunge wa
CHADEMA mwaka 1995. Kabla ya hapo
mlitoa madiwani wengi mwaka 1994.
Wakati Watanzania wengine wakiwa
wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu
kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa,
watu wa Ujiji, watu wa Kigoma hamkusita
kupokea mabadiliko. Wengi wamepoteza
maisha yao, wengine kazi zao na wengine
hata ndoa zao katika kupata mbegu ya
mabadiliko katika nchi yetu. Nawataka
msichoke. Wekeni nguvu mpya katika
kusimika mabadiliko kwani bado kazi ya
kuimarisha demokrasia katika nchi yetu
haijaisha na inahitaji uvumilivu,
kusameheana na kuaminiana.
Na nchi yetu Tanzania ni nchi
inayoonyesha uwezo mkubwa katika
kupendana, kuaminiana, kuvumiliana na
hata kusameheana. Na haya si maneno tu
ambayo ninayazungumza kama
mwanasiasa. Hii ni hali halisi na maisha
niliyoyaishi kwa mifano nilipokuwa
ninakua na kusoma katika shule ya Msingi
Kigoma na baadaye Shule ya Sekondari
Kigoma.
Malezi yangu yalikuwa yanaongozwa na
jamii nzima ya Kigoma. Nimekuwa
nikiwaeleza rafiki zangu niliokutana nao
kwenye masomo na kwenye siasa kwamba
nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza
nikiwa darasa la tatu. Viatu hivyo viliitwa
'asante Salim' vilivyokuwa vinatengenezwa
na Kampuni ya Bora Shoes. Vililinunuliwa
na mama Coretha Furugunya ambaye
tulikuwa tunakaa mtaa mmoja wa
Kisangani Mwanga. Mama Coretha
hakuninunulia viatu kwa sababu alikuwa
ana uwezo mkubwa, la hasha!
Alifurahishwa na matokeo yangu ya
mitihani ya darasa la pili kwenda la tatu.
Ninaamini kitendo cha mama huyu ni
ushahidi wa uungwana, upendo na hata
uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania.
Uwajibikaji kwani alichukua jukumu
kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu,
lakini aliona kuwa kama mwanajamii ana
nafasi kubwa katika kuwaendeleza watoto
wote. Jamii hii ya watu wa Kigoma
ilinifunza kuwa nikijitahidi na kukazana
kwa bidii kwenye masomo na majukumu,
nitafanikiwa. Siwezi kusahau somo hili
katika maisha yangu na ni somo hili ndilo
limenifanya nijitahidi kwa kadiri ya uwezo
wangu kuwatumikia kwa uadilifu na
mafanikio ya hali ya juu sana.
Nikiwa nimejaa matumaini haya kuhusu
wananchi wenzangu, leo nataka
niwakumbushe kwa nini kama jamii
tulichagua kufuata njia ya demokrasia.
Demokrasia ina maana pale ambapo
inatumika kuleta mabadiliko chanya
kwenye maisha ya wananchi. Maisha
yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha
mwananchi kupata huduma zake stahili
kama Elimu, Afya, Maji na miundombinu.
Demokrasia haina maana pale wananchi
wanakufa njaa kwa kukosa ajira na kukuza
umasikini. Demokrasia inahusu
maendeleo.
Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa
mkoa wa Kigoma kutoka mikoa isiyo na
miundombinu kabisa ya maendeleo
mpaka kuwa mkoa unaotumika kama
mfano kwa miradi mingi ya Maendeleo
ikiwemo Daraja la Malagarasi, Uwanja wa
ndege wa Gombe-Mahale, barabara za
lami na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa
bandari ndogo mpya na ujenzi wa kituo
cha Usafirishaji Mwandiga.
Asije mtu akasema yeye ndio kafanya
haya. Haya ni matunda ya nyinyi watu wa
Kigoma kupokea demokrasia na bila woga
kuchagua viongozi wenu bila kujali vyama
bali kwa kuangalia uwezo. Haya ni
matunda ya viongozi wenu kupaza sauti
yenu kwenye baraza la Taifa, Bunge. Haya
ni matunda ya uvumilivu wenu na uamuzi
wenu wa kutaka maendeleo. Juhudi hizi
lazima ziendelezwe kwa nguvu zote ili
kuhakikisha kuwa nafasi ya mkoa wa
Kigoma katika uchumi wa Tanzania
inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea
maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa kituo
cha biashara katika nchi za maziwa
makuu.
Lakini tukumbuke pia kuwa Demokrasia ni
Uwajibikaji. Katika kipindi cha utumishi
wangu kwenu,kutokana na malezi
niliyoyapata kutoka kwenu,nimekuwa
mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Serikali
inawajibika kwa Wananchi. Nakumbuka
wakati napambana kuhusu sheria mbovu
ya madini kuna watu hapa nyumbani
walisema 'sasa huyu kawa mbunge wa
Taifa' lakini watu wengi zaidi wakasema
tumemtuma Dodoma kusemea
Watanzania wote na sio Kigoma tu.
Tuliweza ndani ya miaka mitano kufanya
mabadiliko makubwa sana kwenye sera ya
Madini na sheria ya madini ambapo
baadhi ya mambo ambayo yalikuwa
hayafikiriki sasa yametungiwa sheria
ikiwemo Serikali kuwa na hisa kwenye
migodi, Tanzanite kumilikiwa na
Watanzania sio chini ya asilimia 50 na
kuzuia kabisa wageni kuchimba vito vya
thamani.
Uwajibikaji ulipelekea kumshinikiza Rais
kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la
Mawaziri kwa kuwafukuza mawaziri
wanane mwaka jana. Hii ilitokana sio tu
na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri
Mkuu bali pia ushiriki mkubwa wa
wananchi kupitia simu na mitandao ya
kijamii ambapo wabunge walishinikizwa
kuweka saini kwenye karatasi za kumtoa
Waziri Mkuu. Toka wakati huo kumekuwa
na utaratibu sasa ambapo wabunge
hawaoni taabu kutaka uwajibikaji waziwazi
ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za Umma.
Ni hivi jana tumeshuhudia mawaziri
wanne wamejiuzulu na kufukuzwa kazi
kutokana na kashfa ya operesheni
Tokomeza ujangili iliyoibuliwa na ripoti ya
kamati ya bunge. Mabadiliko haya ni
hatua muhimu katika kuimarisha
demokrasia yetu.
Pamoja na matunda haya mengi mazuri
lakini bado kuna changamoto katika
juhudi zetu.
Changamoto kubwa tuliyonayo wananchi
ni kukosekana kwa imani katika
demokrasia yetu.
Kutoaminiana
Ni dhahiri kuwa kutoaminiana katika nchi
yetu kumekuwa kwa kiasi kikubwa. Taarifa
za kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila
Watanzania kumi, wanane hawaaminiani.
Ni changamoto kubwa sana. Wananchi
wameacha kutuamini wanasiasa na
wanasiasa wameacha kuaminiana
wenyewe kwa wenyewe. Hivi sasa uongo
umegeuzwa kuwa ukweli na ukweli
umekuwa ni uongo. Hivi sasa ukitaka
kuwa mwanasiasa maarufu inabidi ujue
kudanganya na ukitaka kuitwa
mwanasiasa msaliti inabidi uwe msema
kweli.
Kukosekana kwa uaminifu na kuaminiana
imekuwa ni kansa katika siasa zetu.
Itachukua muda mrefu sana kujenga
demokrasia imara katika nchi yetu kama
hatutapata jibu la changamoto hii ya
kutoaminiana na kugeuza uongo kuwa
ukweli na ukweli kuwa uongo. Hivi sasa
ukweli umekuwa unatengenezwa badala
ya kutafutwa. Ni majanga! Juzi bungeni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza
shutuma kwangu kwamba sikushirikiana
na kamati maalum iliyoundwa na Bunge
kufuatilia mabilioni ya uswisi na kwamba
chini ya kiapo nilisema sina majina ya
watu wenye akaunti huko Uswisi. Huu
ulikuwa ni uongo.
Ni uongo kwa sababu niliitika wito wa
kamati hata nilipokuwa katika mafunzo ya
mgambo huko Tanga na nilikutana nao
mara nne. Ni uongo kwa sababu niliwapa
wajumbe wa Kamati Maalaum maelezo na
taarifa nyingi sana kuhusu utoroshwaji wa
fedha nje ya nchi na umiliki wa mali nje ya
nchi kinyumecha sheria.
Ni uongo kwa sababu mimi kutotaja
majina haya haina maana sina majina, bali
ni kwamba ninaheshimu utaratibu na
nimeachia vyombo husika vikamilishe
uchunguzi. Kwani mimi kama mtu binafsi
nikianza kuchukua majukumu ya taasisi
ninaweza kutia dosari harakati hizi
muhimu na hata kupelekea mchakato
mzima kuvurugika. Sitaingia mtego huu!
Lakini hatua hii ya Mwanasheria Mkuu
imenipelekea kujiuliza maswali mengi kwa
mfano uongo kama huu ulifanywa kwa
malengo gani? Na ninajikuta hata mimi
ninaingia katika hali ninayoilalamikia ya
KUTOAMINIANA.
Lakini mtambue pia kuwa kutoaminiana
kunaleta kutovumiliana. Hivi sasa kuwa na
mawazo tofauti katika vyama vya siasa au
hata asasi za kijamii ni uhaini. Lakini bila
kuenzi tofauti za mawazo hatuwezi
kujenga vyama imara wala Taifa imara.
Demokrasia imara ni zao la tofauti za
mawazo na uhuru wa mawazo. Kama
hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha
uhuru wa mawazo na tofauti za mawazo,
tutajenga Taifa lenye watu wenye kuogopa
na waliojaa woga. Wanachama
wanapoogopa uongozi ni udikteta, lakini
uongozi unapoogopa wanachama ni
demokrasia. Bila demokrasia ya uwazi na
kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta.
Lazima vyama vya siasa, viongozwe kwa
namna ile ile ambayo Taifa litaongozwa.
Demokrasia bila kuaminiana, demokrasia
bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli
Juzi nilipoingia Bungeni kwa mara ya
kwanza baada ya matukio kadhaa
yanayoendelea ndani ya chama chetu
nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu.
Wabunge wengine walidhani tutarushiana
ngumi na badala yake ikawa ni vicheko na
mazungumzo. Hii ni kwa sababu sina
chuki na mtu yeyote yule.
Mmenifunza kutojenga chuki na watu na
badala yake kuchukua kila tukio kama
changamoto ya maisha. Siasa ni
kupambanisha mawazo tofauti na
hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. Na
siasa ina misingi yake ambayo sisi
wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi.
Msingi wa siasa ni kuwa inapaswa kuleta
unafuu wa maisha ya wananchi na sio
malumbano tu ya kurushiana maneno na
kuzushiana ili kujijengea umaarufu wa
kisiasa. Siasa si kuwekeana chuki na
kuonyeshana ubabe.
Na hapo ni muhimu muelewa
wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti
ninapofuatilia mabilioni ya Uswisi
ninatafuta umaarufu, ni uongo!
Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua
posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu,
ni uongo! Kinachonisukuma kufanya vyote
hivi ni ninyi. Ninasukuwa kila
ninapowaona watoto bado wanatembea
bila viatu; kila ninapoona akina mama
wanapoteza maisha yao katika uzazi;kila
ninapoona vijana ambao hawana uhakika
wa kupata hata mlo moja kwa siku kwa
kukosa kazi; ninapoona wazee wa Kigoma
kukosa hata shilingi mia moja kununua
chai asubuhi. Ninawaona si wanaKigoma
bali mamilioni ya watanzania wakiishi
katika hali hii. Alafu nalinganisha na
taarifa tunazozipata kuhusu ufujaji na
utoroshwaji wa pesa zetu.
Hebu sasa linganisheni na ukweli kuwa
ripoti ya kimataifa iliyotolewa hivi karibuni
imeonyesha kuwa mwaka 2010 pekee,
jumla ya dola za kimarekani milioni 1315
(bilioni 1.3), yaani shilingi trilioni
2,113,930,000,000 (sh trilioni 2.1)
zilitoroshwa kutoka nchini Tanzania.
Mwaka 2011 kiasi cha dola za kimarekani
milioni 817 yani shilingi za kitanzania
zipatazo trilioni 1,315,370,000,000
(trilioni 1.3) zilitoroshwa. Ripoti hiyo
inaeleza kuwa jumla ya fedha za
Watanzania zilizotoroshwa nje ya nchi
katika miaka kumi iliyopita zilifikia dola za
kimarekani milioni 4526 (bilioni 4.5) sawa
na shilingi za kitanzania trilioni
7,286,860,000,000 (trilioni 7.3).
Nimewatajia hapa namba chungu nzima
na matrilioni na mabilioni hayaleti maana.
Lakini hii ina maana kwamba kiasi cha
pesa zilizotoroshwa katika miaka 10 pesa -
robo yake tuingeweza kujenga barabara
ya lami ya kiwango cha juu kabisa kutoka
Kigoma mpaka Dar-es-salaam!
Pesa hizi zingeweza kuajiri na kuwalipa
vizuri walimu, madaktari na wafanyakazi
wengine ili kuhakikisha tunapata huduma
bora na kutengeneza ajira bora kwa vijana
wetu. Pesa hizi zingeweza kununua
madawa muhimu na kuokoa maisha ya
maelfu ya akina mama tunaowapoteza kila
mwaka wakati wa uzazi. Pesa hizi
zingeweza kuwanunulia watanzania wote
si watoto tu angalau pea 10 ya viatu. Sasa
nikitafakari haya siwezi kuchapa usingizi
mnono na kufumbia macho utoroshwaji
wa fedha au matumizi mabaya ya fedha za
umma kwa njia ya sisi wabunge kujilipia
posho! Hapana! Nafsi yangu hainiruhusu
kukaa kimya kwa kuogopa kuitwa mbinafsi
au msaliti!
Lakini naomba niwasihi kuwa katika
nyakati kama hizi za changamoto za
kisiasa jambo la msingi kuliko yote ni
kutulia maana hakuna linalotokea bila
sababu. Licha ya kwamba kuna watu
wengi wanapaza sauti zao katika mambo
haya lakini pia kuna wengi zaidi ambao
wapo kimya lakini wana mawazo yao,
ndani na nje ya chama chetu;ndani na nje
ya Serikali na ndani nanje ya nchi yetu.
Ndio maana lazima kuibadili nchi yetu ili
kuweza kuhakikisha kila raia anakuwa na
fursa ya kutoa mawazo na fikra zake
zinakuwa huru.
Maisha ni mabadiliko; mabadiliko hayana
ukomo; mabadiliko hayazuiliki kwa sababu
bila mabadiliko hakuna ukuaji, bila
mabadiliko hakuna maendeleo.
Mabadiliko ni kiu kikubwa cha Tanzania
kwa sababu mabadiliko huleta matumaini.
Na kiu hii ni kubwa zaidi kwetu sisi vijana
wa kizazi hiki kipya. Siasa za kizazi kipya
cha viongozi ni siasa za majawabu ya kero
za wananchi. Siasa za mabadiliko ni siasa
za kujenga na kuimarisha; ni siasa za
kuaminiana na kuheshimiana hata pale
mnapopingana kimawazo. Ninataka
tujenge siasa mpya Tanzania;siasa za
mabadiliko; siasa zinazojenga matumaini
ya kweli;siasa zinazowajali na kuwajengea
uwezo wananchi wa Tanzania.
Mungu ibariki Tanzania.
Imetolewa na,
Zitto Zuber Kabwe
Ofisi ya Mbunge-Tabata D.S.M
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company