Watu tisa wamefariki katika ajali ya Hiace kugongana na basi ,huko MWANZA.

 NA ITV
Watu tisa ambao walikuwa ni abiria wa Hiace iliyokuwa inatoka jijini Mwanza kuelekea usagara wilayani Misungwi wamekufa papo hapo baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Allys lililokuwa linatoka Arusha kuelekea Mwanza katika eneo la Buhongwa.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza kamishna msaidizi mwandamizi Valentino Mlowola amesema katika ajali hiyo watu 15 wamejeruhiwa vibaya na wamelazwa katika hospitali ya rufaa Bugando iliyopo jijini Mwanza.

ITV imetembelea majeruhi hao katika hospitali ya rufaa Bugando na kuelezwa na afisa muuguzi wa zamu Bi. Justina Thomas Bishota kwamba hali za majeruhi saba wakiwemo wanawake watatu na wanaume wanne ni mbaya kutokana na majeraha waliyoyapata sehemu mbalimbali za miili yao na kwamba madaktari wanafanya juhudi za kuwafanyia upasuaji na marekebisho mengine ili kuokoa maisha yao.

Aidha kamanda Valentino Mlowola amesema katika tukio jingine mpanda baiskeli mmoja Shilaga Thomas wa kijiji cha Lubuga wilaya ya Misungwi amekufa papo hapo baada ya kugongwa na basi la kampuni ya Bunda bus express lenye namba za usajili T.234 TZK katika eneo la Mitindo wilayani Misungwi wakati basi hilo lilipokuwa likielekea Musoma kutoka Dodoma.

Ameongeza kwamba abiria wengine 41 wa basi la Lukumani ambao walikuwa wakisafiri kutoka Bariadi kuja jijini Mwanza wamenusurika kifo baada ya basi hilo kupinduka katika kijiji cha Mikoroshoni wilayani Magu kutokana na kupasuka tairi la mbele.
www.hakileo.blogspot.com
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company