Khodorkovsky aungana na familia Ujerumani

Tajiri mkubwa kabisa wa zamani wa Urusi Mikhail Khodorkovsky Jumamosi (21.12.2014) ameungana na familia yake katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin baada ya kuachiliwa kwa ghafla kutoka gereza la Urusi na kuletwa Ujerumani.


Mikhail Chodorkowski (kushoto) akikaribishwa na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ujerumani Hans-Dietrich Genscher (kulia)katika uwanja wa ndege wa Schonefeld mjini Berlin. (20.12.2013).


Tajiri mkubwa kabisa wa zamani wa Urusi Mikhail Khodorkovsky Jumamosi (21.12.2014) ameungana na familia yake katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin baada ya kuachiliwa kwa ghafla kutoka gereza la Urusi na kusafirishwa kwa haraka kuja Ujerumani.
Siku moja baada ya kuondolewa kutoka gereza lilioko mbali kaskazini mwa Urusi na kusafirishwa kwa ndege kuja Ujerumani Khodorkovsky alisindikizwa hadi kwenye hoteli ya Adlon mojawapo ya hoteli za kifahari kabisa ilioko katika mji mkuu huo wa Ujerumani Berlin.

Operesheni hiyo ya kuachiliwa kwake ambayo sio ya kawaida iliowashtua Warusi na ulimwengu kwa jumla ilishughulikiwa kwa siri na serikali ya Ujerumani na imekuja kutekelezwa kufuatia mazungumzo kati ya waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ujerumani Hans-Dietrich Genscher na Rais Vladimir Putin wa Urusi.Genscher mwenyewe alikuwako uwanja wa ndege wa Berlin kumpokea.


Wazazi wa Mikhail Chodorkowski mama Marina na Mzee Boris.(2010)

Mtoto wake wa kiume Pavel tayari ameonana na baba yake huyo wakati wazazi wake Marina na Boris nao walikuwa tayari wamewasili Ujerumani kuonana na mtoto wao huyo.

Mama wa Khodorkovsky mwenye umri wa miaka 79 ambaye ana ugonjwa wa kansa amesema anatumia madawa kumsaidia akabiliane na jazba.Amekaririwa akisema kwamba "wameweza kunusurika na huzuni lakini pia ni vigumu kunusurika na furaha". Kauli hiyo ya Marina Khodorkovsky imerushwa hewani na televisheni ya taifa ya Urusi leo hii.

Rais Putin aliishtuwa Urusi hapo Alhamisi kwa kusema kwamba baada ya muongo mmoja akiwa gerezani Khodorkovsky ameomba amwachilie kwa msamaha kwa kutaja sababu za kuumwa kwa mama yake.


Pavel Chodorkowski mtoto wa tajiri wa mafuta wa zamani Mikhail Chodorkowski akizungumza kwa furaha na waandishi wa habari mjini Berlin. (21.12.2013)

Katika kipindi kisichozidi saa 24 baadae Khodorkovsky alipatiwa msamaha huo na kuruka kukelekea Ujerumani kwa kutumia jeti ya kibinafsi ilioandaliwa na Genscher. Maafisa wa gereza wamesema Khodorkovsky aliomba kuletwa Ujerumani ambapo mama yake aliwahi kupatia matibabu hapo kabla.

Yuko huru kurudi

Kasi iliotumika kumuachilia huru imesababisha baadhi ya wachambuzi kudokeza kwamba mfungwa huyo mashuhuri kabisa wa Urusi yumkini akawa amelazimishwa kwenda kuishi uhamishoni wakati Ikulu ya Urusi Kremlin ikiwa katika juhudi za kusafisha rekodi mbaya ya haki za binaadamu ya nchi hiyo kabla ya kufanyika kwa Michezo ya Olympiki ya Majira ya Baridi ambayo Urusi inaiandaa hapo mwezi wa Februari.


Rais Vladimir Putin wa Urusi akizungumza na waandishi wa habari mjini Moscow. (19.12.2013).

Hata hivyo msemaji wa Putin ametupilia mbali madai hayo.Dmitry Peskov ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kwa hakia yuko huru kurudi Urusi. Amekataa kuzungumzia iwapo kuna masharti yoyote yale yalioandamanishwa na kuachiliwa kwake au iwapo atakuwa huru kushiriki katika siasa.Peskov ameongeza kusema kwamba Khodorkovsky mwenye umri wa miaka 50 ameandika baruwa mbili binafsi kwa Putin moja ikiwa ni fupi na ya pili ikiwa refu.

Katika matamshi ya kwanza aliyotowa tokea kuachiliwa kwake Khodorkovsky amesema katika taarifa hapo Ijumaa kwamba ombi lake hilo la kupatiwa msamaha halimaanishi kukiri kuwa na hatia.

Njia ya Solzhenistsyn


Alexander Solzhenitsyn mwandishi mashuhuri wa Urusi aliekuwa akiukosowa utawala wa Muungano wa Kosovieti.

Wakati Urusi na ulimwengu ukisubiri mustakbali wa tajiri huyo mkubwa wa zamani utakavyokuwa, mchambuzi wa wa Kijerumani ambaye amesaidia kuhamishwa kwake amesema Khodorkovsky yumkini asijishirikishe kwenye siasa lakini akaandika vitabu kama vile alivyofanya mwandishi wa vitabu mpizani wa utawala wa Muungano wa Kosovieti Alexander Solzhenitsyn.

Alexander Rahr ambaye alikuwa mkalimani kwa Genscher amekiambia kituo cha televisheni ya kimataifa cha lugha ya Kirusi RTVi kwamba inawezekana akaamuwa kutimiza dhima fulani katika maisha ya wananchi wa Ulaya kwamba anaweza kufuata njia ya Solzhenitsyn akimaanisha mpinzani wa Muungano wa Kisovieti na mshindi wa Tuzo ya Nobel ya uandishi.

Jarida la upinzani la Urusi la The New Times ambalo kwayo Khodorkovsky aliliandikia makala wakati akiwa gerezani amesema tajiri huyo wa zamani amezungumza na chumba cha uhariri wa gazeti hilo kuelezea shukrani zake kwa kumuunga mkono.


Mikhail Chodorkowski akiwa gerezani mwaka 2004.

Jarida hilo limemkariri akisema "Kilicho muhimu leo hii ni Uhuru,Uhuru,Uhuru." Amesema "Mengi yako mbele yanawasubiri,kuachiliwa kwa mateka ambao bado wako gerezani, wa kwanza kabisa na kabla ya wote ni Platon Lebedev" akimkusudia mshirika wake wa kibiashara aliyeko gerezani.

Akikaribisha kuachiliwa kwake Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameitaka Urusi kuanzisha mfumo wa mahakama utakaokuwa wazi, huru na wa kuaminika.Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na waziri wa mambo ya nje Frank- Walter Steinmeir pia wamekaribisha kuachiliwa kwake huko.

Khodorkovsky baba wa watoto wanne ambaye alitupwa gerezani hapo mwaka 2003 baada ya kupatikana na hatia ya kukwepa kulipa kodi na ubadhirifu anatazamiwa kuwa na mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari mjini Berlin Jumapili mchana.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company