Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete anatua nchini leo akiwa na lake moyoni kuhusu hatima ya baraza lake la mawaziri, baada ya kutengua uteuzi wa mawaziri wake wanne, wiki mbili zilizopita.
Rais Kikwete alikwenda Marekani, Desemba 18, mwaka huu kufanyiwa uchunguzi wa afya yake na akiwa huko, upepo wa kisiasa ulibadilika na kumlazimisha kuchukua hatua hiyo ambayo inampa wajibu wa kupanga upya safu yake ya uongozi.
Mawaziri ambao uongozi wao ulitenguliwa ni wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo David Mathayo.
Kung’oka kwao kunatokana na ripoti ya kamati ndogo ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu athari zilizotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, ambayo ilizua mjadala mkali kiasi cha wabunge kumshinikiza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwamba naye aachie ngazi.
Hivyo kitendawili kingine kikubwa kinachomkabili Rais Kikwete ni iwapo ataamua kuendelea kufanya kazi na Pinda ambaye alishambuliwa na wabunge kwamba naye ang’oke kwa madai kwamba ameshindwa kusimamia utendaji serikalini.
Kwa mujibu wa Katiba ya nchi, Ibara ya 52(1) Waziri Mkuu ndiye mwenye madaraka juu ya kudhibiti usimamiaji na utekelezaji wa siku wa kazi na shughuli za Serikali.
Katiba inasema: “Katika utekelezaji wa madaraka yake, Waziri Mkuu atatekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe. Ibara ya 53 (1) inaeleza: “Bila kuathiri masharti ya Katiba hii, Waziri Mkuu atawajibika kwa Rais kuhusu utekelezaji wa madaraka yake.”
Hata hivyo, ni kama Rais Kikwete alishaamua kumwokoa Pinda pale alipompa maagizo kwamba alitangazie Bunge uamuzi wake wa kutengua uteuzi wa mawaziri wanne.
Ripoti hiyo iliyosomwa na Mwenyekiti wake, James Lembeli ilifichua kuwapo kwa vifo na mateso ya wananchi vilivyofanywa wakati wa operesheni hiyo iliyoendeshwa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), maofisa wa Usalama wa Taifa na Polisi.
Mbali ya pengo lililoachwa na mawaziri hao wanne, Rais Kikwete pia ndiye mwenye majawabu kuhusu hatima ya wale waliotajwa kuwa ni mawaziri mizigo kwa kushindwa katika utendaji wao, hasa ikizingatiwa kuwa shinikizo la kuwajibishwa kwao linatoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye ni mwenyekiti wake.
Kitendawili cha Pinda
Zipo hoja kadhaa, iwapo Rais Kikwete atamwondoa Pinda kama ambavyo wabunge walisisitiza wakati wakichangia ripoti hiyo, huku wakirejea yaliyowahi kutokea serikalini lakini Waziri Mkuu huyo akakwepa kuwajibika.
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba isingekuwa rahisi kwa Pinda kuachia ngazi wakati Rais akiwa nje ya nchi kutokana na ukweli kuwa ingekuwa na maana kuwa Baraza la Mawaziri lingetakiwa kuondoka.
Akizungumza juzi, Jaji Mstaafu, Thomas Mihayo alisema kitendo cha Waziri Mkuu kujiuzulu kitamweka Rais katika wakati mgumu kwa sababu Serikali itavunjwa na kuundwa upya.
“Kuunda upya Baraza la Mawaziri ni gharama, tena ikizingatiwa kuwa tunaelekea katika Bunge la Katiba, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu wa 2015, mabadiliko yakifanyika nadhani nchi itayumba,” alisema Jaji Mihayo.
Jaji huyo alisema haoni sababu za Pinda kung’olewa wakati imebaki miaka miwili tu ufanyike uchaguzi mkuu mwingine, na kufafanua kuwa hata kama akija Waziri Mkuu mpya hataweza kufanya mapya kutokana na muda uliobaki.
“Sidhani kama ni busara kushinikiza ang’oke ni wazi kuwa madhara yatakuwa makubwa kuliko mema, lakini ngoja tusubiri tuone uamuzi utakuwaje,” alisema Jaji Mihayo.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema hatua hiyo haitatatua tatizo la mfumo mbovu uliopo zaidi ya kuongeza gharama za kuwatunza mawaziri wakuu wastaafu.
“Ukichunguza kwa makini, Waziri Mkuu Pinda hana tatizo, bali ni mfumo mbovu ambao kimsingi unatakiwa urekebishwe na Rais Kikwete,” alisema na kuongeza:
“Ukimtoa Pinda leo, sanasana unaongeza tu gharama za kutunza mawaziri wakuu wastaafu. Tangu Rais Kikwete anaingia madarakani alishaujua mfumo alioukuta, kwa nini asingeurekebisha ili haya yasitokee?
“Rais anapaswa kupunguza safari za nje na ajikite kushughulikia matatizo kama haya kwa kurekebisha mfumo wa nchi ili usiingize nchi kwenye matatizo.”
Kwa upande mwingine kumekuwa na harakati za kukusanya saini za wabunge ili kuendesha mchakato wa kumng’oa Pinda iwapo Rais hatachukua hatua.
Mawaziri mizigo
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye ndiyo walikuwa watu wa mwanzo kutoa orodha ya mawaziri mizigo wakati walipokuwa katika ziara kwenye mikoa ya kusini.
Waliwataja Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, Dk Mathayo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima.
Viongozi hao walitaka mawaziri hao wajieleze mbele ya Kamati Kuu (CC), ya chama hicho juu ya kushindwa kwao kwenye utendaji wao.
Hata hivyo, orodha hiyo iliongezeka baada ya Bunge kumtaja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Hawa Ghasia pamoja na Manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kupima na kutafakari kama wanatosha kusimamia wizara hiyo kutokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kufichua ufisadi katika wizara hiyo.
Kamati Kuu ya CCM iliyokutana Desemba 14, mwaka huu chini ya Rais Kikwete na iliwahoji Chiza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Ghasia na Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum na baadaye taarifa ya chama hicho ilisema imeliacha suala hilo mikononi mwa Rais kwa hatua zaidi.