
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amesema serikali ina hali mbaya kifedha.
Utouh alitoa kauli hiyo jana wakati akiwasilisha hotuba yake kwa mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimemti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi, wakati akifungua mkutano wa pili wa Baraza la Wafanyakazi, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali.
Alisema kwa sasa hali ya fedha serikalini ni mbaya zaidi, hivyo kuna kila sababu ya serikali kuangalia upya vyanzo vyake vya mapato.
“Tunaiomba na kuishauri serikali na Bunge liangalie upya vyanzo vya mapato ya serikali na matumizi ya fedha zinazopatikana kwa kuwa ni dhahiri kuwa hali ya fedha ya serikali si nzuri kabisa,” alieleza Utouh.
Mbali na hilo, Mkaguzi Mkuu huyo wa Hesabu za Serikali alihoji kama serikali imeainisha vyanzo vyote vya mapato, pia alitaka kuelewa kama serikali inajua matumizi yake, ikilinganishwa na bajeti zilizoidhinishwa na Bunge.
Aliitaka serikali itafakari hatua za kuchukua kuwa na uwiano mzuri zaidi baina ya makusanyo na matumizi ya fedha za serikali.
Alisema suala hilo ni changamoto kubwa na ni wajibu wa taifa kupitia kwa viongozi kuwajibika kulitafakari kwa kina ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Mbali na hilo, Utouh alisema kuwa Ofisi ya CAG bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile mgawo mdogo wa fedha ambao hautoshelezi mahitaji ya ofisi hiyo, ikiwemo ujenzi wa ofisi na kupata vitendea kazi.
“Idara ya rasilimali watu bado ni ndogo sana ikilinganishwa na ongezeko la majukumu ya ofisi kwa kuzingatia ongezeko la mikoa, halmashauri na wilaya mpya pamoja na ukaguzi wa Umoja wa Mataifa (UN).
“Masilahi na hasa mishahara midogo kwa wafanyakazi, hivyo kupunguza ari ya utendaji wa kazi zao,” alieleza Mkaguzi Mkuu.
Aidha, alisema kuwa katika ofisi yake kuna changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na baada ya ugunduzi wa rasilimali adimu ya gesi na mafuta, ofisi na nchi kwa ujumla wake inao wajibu wa kuanza kutayarisha wataalamu mbalimbali watakaohusika na fani ya ukaguzi wenye utaalamu na ujuzi wa kukagua shughuli zote zitakazoambatana na uzalishaji wa rasilimali, ikiwa lengo kubwa ni kuipatia serikali mapato.
Mbali na hilo, alisema kuwa ofisi inao mpango mkakati wa kuwaendeleza watumishi katika taaluma mbalimbali.
“Kama mnavyoelewa ofisi ya taifa ya ukaguzi kwa sasa hivi ina watumishi wa kada mbalimbali, tofauti na kada ya uhasibu na ukaguzi kama ilivyozoeleka huko nyuma,” alisema Utouh.
Kwa upande wake, Yambesi, alisema kuwa watumishi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wanatakiwa kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
“Ni lazima watumishi wa umma wakafanya kazi zao kwa nidhamu ya hali ya juu na kabla ujaenda kumkagua mkaguliwa hakikisha wewe ni msafi.
“Wapo baadhi ya watumishi ambao si waaminifu na wamechafua utumishi wa umma na wale wenye kuhusika na vitendo ambavyo ni kinyume cha maadili ni lazima wawajibishwe,” alisema Yambesi.
CHANZO TANZANIA DAIMA.