
Hata hivyo, baadhi wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema hii ni mbinu tu ya kisiasa ya kuhadaa umma na kurejesha chama hicho kwa wananchi, ili kionekane kinawasemea wananchi kuhusu kero zao lakini anayegoma kusikiliza ni Mwenyekiti wake, Rais Kikwete, ambaye hata hivyo hatarajiwi kuomba uongozi kwenye chama au serikali baada ya kustaafu mwaka kesho.
CCM imebuni njia hii baada ya Rais Kikwete kutofukuza mawaziri hao kama alivyokuwa amekubaliana na mapendekezo ya Kamati Kuu ya CCM, ambayo baadhi ya viongozi wake wanadai alikubaliana nayo, naye akapendekeza majina ya nyongeza; lakini alipoteua mawaziri akawarejesha wote waliotuhumiwa.
Mmoja wa watu waliokosoa uteuzi wa Rais Kikwete alisema mteuaji ndiye anayejua aina ya wasaidizi anaowataka; kwa hiyo kama ameamua kubaki na mizigo yake, hiyo ndiyo serikali anayoitaka.
Wachambuzi wengine wanasema hata viongozi waandamizi wa CCM wanaodaiwa kumkosoa Rais Kikwete kwa kupuuza uamuzi wa Kamati Kuu, wanafanya mchezo wa kitoto wa kujificha, kwani kama wasingekuwa wanazungumza lugha moja na mwenyekiti wao wangejiuzulu nyadhifa zao ili kuokoa heshima zao.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za CCM, jijini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nauye, alisema chama hicho sasa kitatumia vizuri wingi wa wabunge wake bungeni na wingi wa madiwani kwenye halmashauri kuisimamia vizuri serikali.
“Kuanzia sasa, kasi ya CCM kuisimamia serikali, kuisifu itakapofanya vizuri na kukosoa itakapofanya vibaya itaongezeka maradufu kwa kila ngazi,” alisema Nape.
Nape alitahadharisha kuwa hoja ya CCM kwamba kuna mawaziri ‘mizigo’ haikuwa kuwafukuza mawaziri hao bali kuchukua hatua za kurekebisha kasoro na kasi ya utendaji wao.
“Kufukuza inaweza kuwa ni njia ya kutatua tatizo lakini si njia pekee. Hivyo basi CCM tunaamini kuwa kurudishwa kwao ni sawa na kupewa fursa ya kurekebisha upungufu tuliousema kwa niaba ya wananchi. Tunaamini mawaziri wote hawatabweteka bali watatimiza wajibu wao na kuhakikisha wanawatumikia wananchi ambao ndio waajiri wa serikali,” aliongeza Nape.
Vile vile aliongeza kwamba: “Ifahamike kuwa Chama Cha Mapinduzi hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha mapungufu na watakaoshindwa kutimiza wajibu wao vizuri. Wakumbuke kushindwa kwao kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, CCM haitavumilia usaliti huo. Kukaa kimya kwa CCM itakuwa kujinyonga yenyewe jambo ambalo hatutaruhusu kabisa.”
Nape alisema wapo baadhi ya watendaji wa serikali wasiopenda kuhojiwa utendaji wao, hivyo aliwaasa wasiotaka kuulizwa juu ya utendaji wao waondoke serikalini wenyewe kwani CCM watakuwa wakali sana.
“Asiyetaka kuhojiwa na CCM akalime nyanya, au akafuge, lakini mtendaji yeyote aliyeko serikalini lazima tutamhoji, Chama Cha Mapinduzi ndicho kina Ilani inayotekelezwa, na CCM ndio watakaoulizwa Ilani ilitekelezwaje. Mawaziri wana safari nyingi nje ya nchi kuliko ziara za kutembelea wananchi, wananchi wanataka huduma lakini kuna vikao vingi, barua zinaandikwa hazijibiwi kwa kuwa mawaziri wapo kwenye vikao, CCM tutakuwa wakali, asiyetaka kuhojiwa atimize wajibu wake au asiyetaka kuhojiwa akalime nyanya,” alisema Nape.
Nape alisema dhana ya mawaziri kuteuliwa na kuanza kufikiri kuvaa suti tu ndiko kunasababisha sherehe zinakuwa nyingi baada ya uteuzi kwa sababu mawaziri wanafikiri ulaji badala ya uwajibikaji.
CCM imewaomba Watanzania kwa ujumla kuwapa muda wateule hao mizigo wa rais watimize wajibu wao, lakini tusisite kusema pale tutakapoona mambo hayaendi kama tunavyotarajia. Uwajibikaji wa kweli ndio msingi wa mafanikio na maendeleo yetu.
“CCM imewatakia kila la heri mawaziri walioteuliwa katika kutimiza wajibu wao. Ikiamini kuwa mawaziri hao hawataisaliti Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kusababisha wananchi kukosa imani kwa serikali yao,” alisema.
Kauli hiyo ya Nape ambayo ni mara ya kwanza tangu Rais Kikwete awarejeshe mawaziri mizigo, imekuja baada ya baadhi ya wananchi na wachambuzi wa mambo ya siasa kudai kwamba Rais Kikwete ameisaliti CCM.
Wakiwa ziarani katika Wilaya ya Namtumbo viongozi wa CCM waliwataja Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima, wameshindwa kazi na kupendekeza wang’olewe.