WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaonya Watanzania kuwa makini na watu wanaotumia rushwa ili kupata nafasi za uongozi na hasa kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2015.
Ametoa onyo hilo leo mchana (Jumapili, Julai 27, 2014) wakati akizungumza na mamia ya waumini na viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya uzinduzi wa dayosisi mpya ya Ruvuma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kuwekwa wakfu Askofu Amon Mwenda aliyeteuliwa kuongoza dayosisi hiyo.
“Ninawasihi wananchi wawe makini na viongozi wanaopenda kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu. Kama mtu ana nia ya kweli ya kuongoza ni kwa nini atumie fedha ili kupata nafasi ya uongozi?,” alihoji.
“Tatizo ni kwamba hata wananchi hivi sasa wanakubali kupokea kile kinachotolewa na wagombea. Atakuja huyu atakupa hiki na mwingine naye atakupa kile, lakini ujue akiingia madarakani anaanza kurudisha haraka vile alivyowagawia,” alisema.
Aliwaonya wananchi kuwa makini ili wasije wakageuzwa mtaji wa kuwanufaisha watu binafsi. “Tukikubali kutumika ni sawa tutapata viongozi wakati wa uchaguzi, lakini watakuwa ni wale wasio na hofu ya Mungu, wenye kujali maslahi yao kuliko ya wananchi waliowachagua,” aliongeza.
Aliwaomba viongozi wote wa dini waliohudhuria sherehe hizo pamoja na waumini wote waendelee kuliombea Taifa ili Mungu aliepushe na janga hilo la watu kupenda rushwa. Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wazidi kuuombea mchakato wa kupata Katiba mpya ili wabunge wote warejee ndani ya Bunge na kuikamilisha kazi waliyoianza.
Alimuomba Askofu huyo mpya apokee jukumu hilo kwa mikono miwili na kumuahidi kuwa kama Serikali watakuwa naye bega kwa bega kuwaongoza Watanzania walioko kwenye dayosisi yake. Dayosisi hiyo mpya inahusisha mkoa wote wa Ruvuma na wilaya ya Ludewa eneo ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 72,630. Kati ya hizo km. za mraba 64,233 ni za mkoa wa Ruvuma na km. za mraba 8,397 ni za wilaya ya Ludewa.
Mapema, akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kusimikwa rasmi, Askofu Mwenda alisema dayosisi mpya ya Ruvuma imezaliwa katika kipindi chenye changamoto nyingi za kidunia na utandawazi ukiwemo mmomonyoko mkubwa wa maadili.
Hata hivyo, akiainisha malengo ya dayosisi hiyo ambayo anakuwa Askofu wake wa kwanza, Askofu Mwenda alisema mbali ya kufundisha neno la Mungu, dayosisi hiyo itahimiza ufanyaji kazi ili wakazi wake wawe na akiba ya chakula cha kutosha.
Alisema watashirikiana na Serikali na wadau wa ndani najje katika kutoa huduma za kijamii hasa elimu na afya. Aidha alisema atakabiliana na changamoto za sasa ambazo alizitaja kuwa ni mmomonyoko wa maadili, rushwa, mauaji ya albino, unajisi wa watoto na ubakaji wa wanawake.
Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa alisema Kanisa lingependa kupata viongozi ambao ni wacha Mungu.
Akirejea mahubiri yake, Askofu Malasusa alisema inashangaza kuona kuna baadhi ya watu wanagombea nafasi za uongozi lakini hawana mapenzi na Mungu aliyewaumba watu anaotaka kuwaongoza. “Bila kujali imani ya mtu, tunatamani tungepata kiongozi ambaye anamcha Mungu. Awe anapenda kuhudhuria ibada. Awe anampenda Mungu ndipo atawapenda watu anaowaongoza,” alisisitiza.