Rais wa Syria Bashar Al Assad ametetea hatua yake pamoja na ya jeshi la taifa lake wakati wa miaka minne ya mapigano dhidi ya vikosi vya upinzani na wanamgambo wa kiislamu.
Kwenye mahojiano na BBC Rais Assad amesema kuwa serikali ilichukua hatua ya mapema ili kuwalinda raia na kupigana na kile alichokitaja kuwa ugaidi.
Alisema kuwa wanajeshi wa Syria hawajashambulia shule wala hawajatumia silaha za kemikali kuwaua raia katika kipindi hicho licha ya madai chungu nzima dhidi yao.
Bwana Asad ameyapinga na kuyaita kuwa propaganda, madai kutoka kwa Umoja wa mataifa kuwa wanajeshi wa Syria mara nyingi walizuia misafara ya shirika hilo kufika maeneo ya raia.
Amesema kuwa Syria haijawasiliana moja kwa moja na Marekani kuhusu vita vya muungano dhidi ya kundi la Islamic State, lakini amesema kuwa Marekani ilipitisha habari kupitia nchi zingine ikiwemo Iraq.
CHANZO BBC SWAHILI