Katuni.
Siyo siri tena kwamba ule uliokuwa unaangaliwa kama muungano wa hiari (coalition of the willing) miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), sasa unaonekana kukolezwa moto ili Tanzania ipate madhara zaidi.
Kenya, Uganda na Rwanda kwa muda sasa zimekuwa zikishirikiana katika miradi mikubwa ya miundombinu, kama vile kusaini mikataba ya matumizi na upanuzi wa bandari, ujenzi wa reli na hata bomba la mafuta miongoni mwake, huku Tanzania ikiwa ni mwanachama mwenzao kwenye Jumuiya hiyo, ikitengwa.
Awali juhudi hizi zilionekana kama kuitaka Tanzania kukubaliana na malengo ya nchi hizo ya kutaka pamoja na mambo mengine kuharakisha shirikisho la kisiasa la Jumuiya hiyo, lakini pia zikitaka Tanzania kufungua milango yake zaidi kwa wakazi wa Afrika Mashariki kutumia ardhi ya Tanzania kwa uwekezaji.
Hatua za hivi karibuni kabisa za kulazimisha Tanzania kwenda mwendo wa nchi hizo, ulichukuliwa na serikali ya Kenya kwa kupiga marufuku magari ya kubeba watalii ya Kitanzania kuingia katika viwanja vya ndege vya Kenya na katika mbuga za wanyama kwa kile kilichoelezwa na wadadisi wa mambo kuwa ni ‘jeuri’ ya Tanzania ya kuendelea kuufunga mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Bologonja ambao unatenganisha mbuga ya Taifa ya Serengeti na ile ya Kenya, Masai Mara.
Mpaka huu ulifungwa wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere miaka ya sabini kwa sababu za kimsingi za kiuchumi. Hadi kesho, sababu hizo bado zina nguvu na watawala wote watatu waliomfuata Mwalimu, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete, wameendelea kutambua na kuheshimu uamuzi huo wa kizalendo uliofikiwa na serikali ya Mwalimu ambayo asiliani haikuwa na mchezo kuhusu rasilimali za taifa.
Mbuga ya Taifa ya Serengeti ni moja ya vivutio vya utalii vinavyoaminika na kuheshimika sana duniani. Mbuga hii ina ukubwa wa kilometa za mraba 14,763 ikiambaambaa hadi kuingia Kenya ambako huitwa Masai Mara. Uotoa na mfumo wa ikolojia ya Serengeti kitaalam inachukuliwa kwa pamoja na Masai Mara yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,510. Kwa maneno mengine Kenya inamiliki asilimia 10 tu ya uoto na ekolojia ya Serengeti.
Kwa bahati mbaya, wanyama hawatambui mipaka iliyowekwa na binadamu, ndiyo maana wanyama wa Serengeti husambaa eneo lote la Serengeti na Masai Mara kama eneo lao moja la kujidai. Hii ndiyo inafanya Serengeti na Masai Mara kuwa kitu kimoja hata kama ni mbuga ambazo zinamilikiwa na nchi mbili tofauti.
Katika mazingira kama hayo, ni jambo lisilofaa na kwa kweli lisilokubalika kwamba moja ya nchi hizi mbili inataka kugeuza nyingine ngazi ya kunufaika tu na sekta ya utalii kwa kutaka kuwako kwa mifumo ambayo kisayansi na katika utaalam wa uhifadhi wa wanyama pori haukubaliki na haina tija kwa ustawi na uendelevu wa hifadhi hiyo.
Mgogogoro wa Kenya kutaka mpaka wa Bologonja ufunguliwe ni wa kujipendelea. Mosi, kwamba watalii waingie Kenya, walale Kenya, walipe fedha Kenya, lakini mchana wavuke tu mpaka wakitokea Masai Mara eneo dogo ambalo kwa hakika litakuwa na wanyama wachache, waingie Serengeti na kunufaika na wanyama kisha warejee Kenya jioni na Tanzania ibaki mikono mitupu. Hii siyo haki. Huu ni uporaji wa mchana kweupe.
Mbili, kutaka kufungua mpaka wa Bologonja ni kinyume cha taratibu za uhamiaji. Kokote duniani hakuna utaratibu wa kuwa shughuli za binadamu ndani ya mbuga ya wanyama pori. Kwamba sasa Bologonja iwe ni kituo cha forodha, uhamiaji na hivyo watu wapite tu hapo kama wanavyopita vituo vingine vya mpakani, huu ni utaratibu mpya ambao Tanzania haiwezi kuukubali.
Kwa maoni yetu sababu zilizotolewa miaka ya sabini za kuufunga mpaka wa Bologonja, bado zingali na nguvu na ni za msingi. Tanzania haina sababu ya kulazimisha Kenya kuruhusu magari ya kubeba watalii kuingia nchini humo, lakini tunajua na tuna hakika kwamba mtalii anayetaka kujionea maajabu ya Serengeti hatazuiwa na mbinu hizi ovu za kukataa magari kuingia viwanja vya ndege.
Ni rai yetu kwamba kama taifa tuimarishe miundombinu yetu, tujipange kwa makini zaidi kujitangaza kuwa tuna vivutio bora zaidi vya utalii siyo Afrika Mashariki na Afrika tu, bali duniani. Tuwaambie watalii waje washuhudie wanyama kwa wasaa wao, bila kubugudhiwa na utitiri wa magari na hoteli mbugani.
Kwa uungwana kabisa tuwajibu Kenya kwa kufanya mambo yetu kisayansi, kwa kuwa walichokifanya ni kukiri dhahiri kwamba wana nia ovu dhidi yetu, wanamezea mate Serengeti na kwa kuwa wanyama ni wetu na kipindi kikubwa cha mwaka hukaa Tanzania, basi wajipange upya kwani neema hii ni baraka ya Mungu kwa Tanzania asiliani Kenya hawawezi kuichukua. Muda wa kutishwa na kulazimishwa na watu wenye maslahi binafsi dhidi ya taifa letu umepita siku nyingi, tusonge mbele. Tunataka kuwa na viongozi imara na wenye fikra pevu katika kusimamia na kuongoza shughuli zote za maliasili ili kuimarisha sekta ya utalii mara dufu.
CHANZO: NIPASHE
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago