Miili ya baadhi ya wahamiaji haramu waliokufa katika bahari ya Meditteranian, Feb. 9, 2015.
Idara ya Umoja wa Mataifa ya kuhudumia wakimbizi-UNHCR ilisema jumatano takriban watu 200 wamefariki na wengine 100 wamepotea baada ya kujaribu kuvuka bahari ya Mediterranean kwa kutumia boti za kujaza upepo.
Kundi la boti nne ambazo zilikuwa zimebeba wahamiaji na wakimbizi kutoka barani Afrika chini ya jangwa la sahara ziliondoka Libya jumamosi ikiwa zinajaribu kufika nchini Italy. Boti tatu kati ya hizo zimeweza kupatikana hadi hivi sasa.
Umoja wa Mataifa ulisema watu 29 kutoka kwenye moja ya boti wameripotiwa kufariki siku ya jumapili huku watu 110 wakiokolewa na kikosi cha walinzi wa pwani cha Italy na kufikishwa kwenye kisiwa cha Lampedusa. Lakini ni watu tisa tu kati ya abiria 116 waliokuwa katika boti nyingine mbili walinusurika.
Mkurugenzi mkuu wa UNHCR kwa ulaya, Vincent Cochetel alisema haya ni maafa ya kiwango kikubwa sana na ni ukumbusho wa dhahiri kwamba maisha ya watu yanaweza kupotea kama wale ambao wanatafuta hifadhi salama wanaondoka wakitegemea kudra ya mwenyenzi mungu baharini.
Wahamiaji haramu wakikatisha bahari ya mediterranean
Kisiwa cha Lampedusa kiko kiasi cha kilometa 110 kutoka barani Afrika na kituo kikuu kwa wahamiaji haramu wanaojaribu kufika ulaya.
Rekodi ya wahamiaji 170,000 imevuka bahari ya Mediterranean na kuingia ulaya mwaka 2014 robo moja kati ya hao walikuwa wanakimbia ghasia nchini syria. Zaidi ya watu 3,000 wengine walifariki wakiwa safarini.
Wataalamu wanasema kiwango cha uhamiaji mwaka huu wa 2015 tayari kinaonekana kuvuka kile cha mwaka jana.