CCM, Ukawa waporana majimbo

Kwa ufupi

Wakati CCM ikipora majimbo tisa hadi sasa kutoka vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF vinavyounda Ukawa, umoja huo umejiimarisha zaidi kulinganisha na mwaka 2010 kwa kuweka chini ya himaya yake majimbo 21 yaliyokuwa yanashikiliwa na CCM.By Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar/Mikoani. Wakati matokeo ya ubunge yakiendelea kutangazwa, CCM na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vinazidi kunyang’anyana majimbo vilivyokuwa vinayashikilia, yakiwamo majimbo yaliyokuwa chini ya wabunge maarufu.

Wakati CCM ikipora majimbo tisa hadi sasa kutoka vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF vinavyounda Ukawa, umoja huo umejiimarisha zaidi kulinganisha na mwaka 2010 kwa kuweka chini ya himaya yake majimbo 21 yaliyokuwa yanashikiliwa na CCM.

Hadi jana jioni, CCM ilikuwa imefanikiwa kuchukua majimbo ya Ilemela, Nyamagana, Biharamulo, Maswa Mashariki na Magharibi, Bukombe, Lindi Mjini, Kasulu Mjini na Kigoma Kaskazini.

NLD, ambayo inaunda Ukawa pamoja na NCCR, CUF na Chadema haikuwa na jimbo lolote.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyokuwa yametangazwa hadi jana jioni, majimbo yaliyochukuliwa na Ukawa ni Longido, Simanjiro, Kilombero, Ukonga, Mikumi, Siha, Monduli, Bunda Mjini, Arumeru Magharibi na Buyungu.

Mengine yaliyochukuliwa na Ukawa ni Temeke, Babati Mjini, Tarime Mjini, Tandahimba, Moshi Vijijini, Mtwara Mjini, Serengeti, Tanga Mjini, Bukoba Mjini, Same Mashariki na Liwale.

Miongoni mwa wabunge ambao wameathirika na vita hiyo ya kunyang’anyana majimbo ni pamoja na Ezekiel Wenje ambaye ameangushwa Jimbo la Nyamagana, Stephen Kebwe (CCM, Serengeti), Profesa Juma Kapuya (CCM, Kaliua), Vicent Nyerere (Chadema, Musoma Mjini), Steven Wasira (CCM, Bunda), James Lembeli (Chadema, Kahama) na Anne Kilango (CCM, Same Mashariki).

Wapambana majimbo mapya

Ukawa na CCM pia walikuwa na vita nyingine kali kwenye majimbo mapya yaliyoanzishwa kwa kuzingatia idadi ya watu na kuanzishwa kwa halmashauri mpya. Katika majimbo hayo, Ukawa imeshinda Mlimba, Tunduma, Kibamba, Mbozi na Momba, ambayo yamechukuliwa na Chadema wakati Vwawa, Busokelo, Itilima na Butiama yamechukuliwa na CCM.

Wapinzani waiteka Dar

Kwa mujibu wa matokeo yaliyokuwa yakiendelea kutangazwa jana, Halima Mdee alitangazwa tena kuwa mshindi wa Jimbo la Kawe baada ya kumshinda mpinzani wake wa karibu, Kippi Warioba kwa takriban kura 10,000.

Ushindi wa Mdee, wa John Mnyika katika jimbo jipya la Kibamba pamoja na wa mgombea wa CUF wa Jimbo la Temeke, Abdallah Mtolea umeifanya Ukawa iendelee kujichimbia mkoani Dar es Salaam.

Ukawa sasa imetwaa majimbo matano kati ya 10 ya jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza kutwaa zaidi ya majimbo matatu tangu mwaka 1995.

Kabla ya uchaguzi wa mwaka huu, Chadema ndiyo pekee iliyokuwa inashikilia majimbo ya Kawe na Ubungo kati ya majimbo kumi ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyokuwa yametangazwa hadi jana jioni Ukawa imetwaa majimbo ya Temeke, ambako mbunge anayemaliza muda wake, Abbas Mtemvu ameangushwa na Mtolea wa CUF huku Jimbo la Ukonga, Meya wa Ilala, Jerry Silaa ameangushwa na Mwita Waitara wa Chadema, na Kibamba, ambako John Mnyika wa Chadema amemshinda waziri wa serikali inayomaliza muda wake, Fenella Mukangala.

Jimbo jingine ni Ubungo, ambalo limechukuliwa na mwandishi maarufu wa habari, Saed Kubenea (Chadema) na Kawe, ambako Mdee (Chadema) amefanikiwa kurudi bungeni baada ya matokeo kuchukua muda mrefu kutangazwa kutokana na mpinzani wake kuweka pingamizi.

“Kuna ujanja unafanywa na chama cha siasa na watendaji wa halmashauri,” alisema Mdee akiwa ameambatana na mama yake mzazi baada ya matokeo kutangazwa jana kwenye kituo cha Shule ya Msingi Oysterbay. “Kwa hiyo usipokomaa, utashindwa. Watu wamepoteza haki zao kwenye majimbo mengi kwa sababu ya wizi huu.”

CCM, ambayo imekuwa ikitamba mkoani Dar es Salaam tangu siasa za ushindani ziliporejeshwa mwaka 1992, hadi jana jioni ilikuwa imeambulia viti viwili vya Ilala, ambako Mussa Hassan Zungu amefanikiwa kutetea kiti chake na Jimbo la Kigamboni ambalo Dk Fasutine Ndungulile ameshinda.

Matokeo katika majimbo ya Kinondoni, Segerea, Mbagala na Kigamboni bado hayajatangazwa, sababu kubwa ikiwa ni kurudia kutangaza matokeo.

Katika matokeo mengine yaliyotangazwa jana, kada wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa alifanikiwa kutetea kiti chake cha Iringa Mjini baada ya kumbwaga katibu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) na aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela.

Matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo yalichelelewa kutangazwa kutokana na Mwakalebela kulalamikia matokeo ya kituo kimoja na hivyo kuamuliwa kura kurudiwa kupigwa jana.

Kwenye jimbo jipya la Kibamba, Dk Fenella Mkangala aliangushwa na Mnyika baada ya matokeo kuchelewa kutangazwa kutokana na wakazi wa Kimara Stop Over kupiga kura Jumatatu.

Upigaji kura kwenye eneo hilo haukufanyika Jumapili kutokana na kukosekana kwa vifaa.


Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company