NA JJ Mnyika
Nguvu ya Umma!
Salamu za Maulid na Barua ya wazi kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Nawatakia heri katika Maulid an-Nabi, ni siku ya
kukumbuka kuzaliwa na maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W)! Ifuatayo ni barua ya wazi kwa tume ya mabadiliko ya Katiba;
BARUA YA WAZI KWA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Mwenyekiti,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Dar es Salaam
Mheshimiwa,
YAH: KUPANUA WIGO WA KUKUSANYA MAONI YA WANANCHI BINAFSI KWA SIMU ZA MKONONI NA MAKUNDI YA WANANCHI KATIKA MABARAZA YA KATIBA
Nakuandikia nikirejea maelezo yako kwenye mkutano wako na waandishi wa
habari tarehe 5 Januari 2013 kuhusu mchakato wa ukusanyaji maoni ya
mabadiliko ya katiba.
Maelezo uliyotoa yanadhihirisha upungufu katika mchakato wa ukusanyaji
wa maoni ya wananchi binafsi unaoelezwa kukamilika kwa kuwa na idadi
ndogo ya watu waliotoa maoni mpaka sasa ambapo mpaka awamu nne
zinakamilika jumla ya watu 318,223 tu ndio waliotoa maoni; kwa tafsiri
yangu hii ni sawa na asilimia 0.7 ya wananchi wote zaidi ya milioni
44.9.