Manchester City haikutumia nafasi walizopata kufunga wakati wa mechi hiyo.
Juhudi za washambuliaji wake David Silva na Carloz Tevez hazikufua dafu pale mikwaju yao ilipogonga mlingoti.
Kipa wa Stoke Thomas Sorenson vile vile alifanya kazi ya ziada kuokoa mikwaju ya washambuliaji hao wa Manchester City.
Stoke haikufanya mashambulizi yoyote ya maana wakati wa mechi hiyo.
Lakini wakati mechi hiyo ilipoonekana kuisha kwa timu hizo mbili kutoshana nguvu, Sergio Aguero alimpa pasi nzuri Zabaleta ambaye aliiweka kimyani na kuwaacha mashabiki wa Stoke vinywa wazi.
Mchezaji wa ziada ya Stoke Cameron Jerome, alipata nafasi nzuri sana ya kusawazisha lakini, akaupiga mpira ovyo licha ya kuwa katika nafasi nzuri na kipa pekee.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Manchester City katika uwanja huo wa Stoke tangu mwaka wa 1999, wakati timu hizo mbili zilikuwa zinacheza ligi daraja ya pili.