JANA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk Emmanuel Nchimbi, aliwasimamisha kazi maofisa Polisi watano na kumpa
mwingine likizo ya mwaka mmoja, kwa tuhuma mbalimbali za kukiuka maadili
na utaratibu wa Polisi.
Kati ya Polisi hao, aliyekuwa Mkuu wa
Upelelezi Mkoa wa Mbeya, Elias Mwita, aliyekuwa Msaidizi wake, Jacob
Kiango na aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya,
Charles Kinyongo walisimamishwa kazi kutokana na tuhuma moja.
Inadaiwa viongozi hao walikabidhiwa
kidhibiti cha dawa za kulevya aina ya cocaine kilo 1.9, wakatakiwa
kuipeleka Ofisi ya Mkemia Mkuu, badala yake, ‘wakachakachua’ na kupeleka
chumvi na sukari.
Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi mkoani
Kagera, Peter Matagi naye amesimamishwa kazi na atafunguliwa mashitaka
ya kijeshi, kutokana na kukabiliwa na tuhuma za kuwabambikiza kesi
zisizo na dhamana wananchi 13 wa Kata ya Nyakasimbi, wilayani Karagwe
katika Mkoa wa Kagera.
Wananchi hao inadaiwa walibambikizwa
kesi ya ujambazi wa kutumia silaha, na walikaa mahabusu kwa muda wa
miezi miwili, baadaye timu ya uchunguzi iliyoongozwa na Dk Nchimbi
mwenyewe, ikabaini kuwa mashitaka waliyoshitakiwa, hayakuwa sahihi.
Pia, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi, aliyekuwa anasimamia ajira katika jeshi hilo nchini, Renatus
Chalamila, amepewa likizo ya mwezi mmoja, kutokana na tuhuma za kutajwa
mara nyingi kuhusika kuwatoza fedha vijana walioomba ajira Polisi ili
awapatie kazi hiyo.
Tunaipongeza Serikali kwa ujumla na Dk
Nchimbi binafsi kwa kuchukua uamuzi huo, ambao unalenga kuimarisha
nidhamu ndani ya Polisi na kuimarisha haki na usawa kwa kila Mtanzania.
Tunaunga mkono hatua hiyo ya Dk Nchimbi,
kwa kuwa ni muhimu katika kuiondoa Serikali kwa ujumla na Polisi kama
taasisi, katika kizimba cha kulalamikiwa na wananchi kila siku, kwa
ukiukwaji wa haki za wananchi na ukosefu wa maadili.
Hata hivyo, tunashauri moto huo
ulioanzia Makao Makuu ya Polisi mkoani Dar es Salaam, ukaenda Mbeya na
Kagera, uendelezwe katika mikoa mingine na hasa katika hili la
kubambikizia kesi wananchi na kulazimishwa rushwa ili kupata ajira.
Hatusemi kwamba suala la dawa za kulevya
halina uzito, hapana, tunaipongeza sana Serikali katika hilo kwa kuwa
dawa hizi zinaharibu zaidi vijana, rika ambalo linategemewa leo kwa
ajili ya ujenzi wa uchumi wetu.
Lakini, tunasisitiza mkazo zaidi pia
uwekwe katika suala la kubambikizwa kesi na rushwa katika ajira, ambayo
athari zake ni kwa wananchi wa kipato cha chini zaidi, na yamekuwa kama
saratani isiyo na dawa, ambayo imekuwa ikichafua jina la Serikali.
Ni vigumu kusikia Mtanzania mwenye
kipato kizuri amebambikiziwa kesi, au anatapatapa kutafuta ajira kwa
kutoa hongo, kama ilivyo kwa Watanzania wenye kipato cha chini, ndio
maana tunasisitiza ili kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali,
masuala hayo yawekewe mkazo.
Tunashauri watuhumiwa hao, wachukuliwe
hatua sahihi za kisheria na ziwekwe wazi, ili iwe fundisho kwa wote na
tunatarajia pia wananchi na wanasiasa wataiunga mkono Serikali katika
hili na kuipongeza, kwa kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha Polisi
itakayozingatia haki na usawa kwa Watanzania.