- HALMASHAURI KUU YARIDHIA,YATEUA MAKATIBU
Na Pendo Mtibuche, Dodoma
HALMASHAURI
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana imemaliza kikao chake cha siku tatu
mjini Dodoma
chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete. Kikao hicho kimeridhia baadhi ya
mapendekezo ya Kamati Kuu ya CCM, pamoja na kumvua uanachama Mjumbe wa Baraza
la Wawakilishi Kiembesamaki, Jimbo la Mjini Magharibi, Zanzibar, Bw. Mansour
Yusuf Himid.
Bw. Himid ni kada wa siku nyingi katika visiwa vya Zanzibar na Waziri
wa zamani, aliibua mjadala ndani ya CCM akitaka Zanzibar pate haki ya kuwa na mamlaka zaidi
ya kujiamulia mambo yake ndani ya Muungano. Mwanasiasa huyo, ambaye amepata
kuwa Mweka Hazina wa CCM Zanzibar wakati wote wa uongozi wa Rais Mstaafu, Amani
Abeid Karume, amekuwa mtetezi mkubwa wa muundo wa Muungano wa Serikali tatu
badala ya ule wa Serikali mbili.
Halmashauri Kuu ilitarajiwa kutoa uamuzi wa ama kufukuzwa au
kumbakiza kundini baada ya uongozi wa ngazi ya Mkoa, Wilaya pamoja na Kamati
Maalumu ya CCM Zanzibar, kupendekeza atimuliwe kutokana na msimamo huo. Taarifa iliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM
Taifa, Bw. Nape Nnauye, alisema baadhi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili Bw.
Himid ni kushindwa kusimamia malengo ya chama na kutekelezamasharti ya uanachama.Kushindwa
kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka maadili ya kiongozi wa CCM pamoja na kuikana Ilani ya chama ya Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2010-2015 na kuisaliti CCM. "Kwa uamuzi uliofikiwa wa kumvua Bw. Himid
uanachama wa CCM, kwa sasa si kiongozi tena wa CCM," alisema.
Hata hivyo,
Halmashauri Kuu ya CCM ilijadili kwa kina muundo wa Muungano na suala la Bw.
Himid ambaye alishatangaza kuwa, yuko tayari kufukuzwa kwa sababu ya kutofautiana
na chama chake juu
ya muundo wa sasa wa Muungano. Pia kikao hicho kimeridhia uteuzi wa
Makatibu wateule wapya wa jumuiya za CCM, Umoja wa Vijana (UVCCM), Jumuiya ya
Wazazi na Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT).Mapendekezo ya Kamati Kuu ambayo yameridhiwa na NEC, Sixtus
Mapunda ameteuliwa kuwa
Katibu wa Umoja wa Vijana CCM, ambaye awali alikuwa Kaimu Katibu
wa CCM mkoani Morogoro.
Bw. Seif Shabani Mohamed, ambaye ni Mjumbe wa NEC kutoka Pemba aliteuliwa nafasi
ya Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ambapo Katibu wa UWT ni Amina Makilagi
ambaye ameendelea
kushika wadhifa huo. Mapunda atachukua nafasi iliyokuwa imeshikiwa
na Martine Shigela ambaye ameongoza UVCCM kwa kipindi cha miaka mitano sasa ambapo Bw. Mohammed kutoka
Pemba akichukua nafasi iliyokuwa kishikiliwa na Hamis Suleiman Dadi ambaye pia
amekuwa katika wadhifa huo kwa miaka mitano.
Kikao hicho pia kimeridhia mapendekezo ya Kamati Kuu kwa ajili ya
kuziba nafasi za Makatibu wa CCM mikoa mitatu ya Morogoro, Kaskazini Pemba na
Geita. Mikoa hiyo ilikuwa haina Makatibu kwa muda mrefu kutokana na sababu
mbalimbali. Walioteuliwa na mikoa yao
kwenye mabano ni pamoja na Msaidizi Kitengo cha Uchaguzi CCM, Ofi si Ndogo
Makao Makuu ya chama, Romuli Rojas John (Morogoro). Wengine ni aliyekuwa Katibu
Wilaya ya Mkinga, Kassim Mabrouk Mbarak (Kaskazini Pemba) na aliyekuwa Katibu wa CCM Igunga, Mary
Maziku (Geita). Kuhusu sakata la madiwani wa Bukoba Mjini, mkoani Kagera, chama
hicho kilisema suala hilo linaendelea kushughulikiwa na baada ya kikao cha NEC, Kamati Kuu
itaendelea kukutana na viongozi wa Wilaya ya Bukoba, Mwenyekiti wa CCM na
Katibu wa Wilaya hiyo. Mapema kabla ya kikao cha NEC, Kamati Kuu ilikutana na
Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, Meya wa Manispaa ya Bukoba
Mjini Dkt. Anatory Amani na kuwahoji.