Filamu ya Ponda na wenzake, Jamii inaanza kuikinai


Sheikh Ponda Issa Ponda alipokuwa mahakamani

Na Mwandishi Wetu
IMENIBIDI niandike ingawa sikupenda kufanya hivyo katika sakata la Sheikh Ponda na wenzake. Ila nimelazimika kuandika ili kuweka kumbukumbu sawa ili walio na maswali kama ya kwangu wajue kwamba si wao tu, bali tuko wengi tunaowaza na kuona mambo kama wao.   Sikupenda kutumia ufahamu, maarifa na ujuzi wangu kuandika ya filamu ya Ponda na wenzake, inayoonekana kuacha maswali mengi kuliko majibu. Tena maswali yasiyokuwa na manufaa au maslahi mapana kwa jamii na kwa taifa.
Pia ningependa ieleweke mapema kwamba ninayaandika haya, nikiwa najilazimisha kwa sababu tu ni wajibu wangu kuandika na si vizuri kuacha kumbukumbu za maswali na mtazamo mbaya katika jamii.   Kutokana na maswali kuwa mengi kuliko majibu, ndiyo sababu wakati filamu ya Sheikh Ponda na wenzake inaendelea, ilinibidi kugonga hodi kwa msajili wa dini na vyama vya hiyari, iliyopo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Lengo la kwenda huko ni kupata jibu la swali, kinachoitwa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, ni nini na kilisajiliwa lini na kwa malengo gani na ofisi zao ziko wapi?   Safari yangu hiyo, haikuzaa matunda kwa sababu msajili wa dini na Taasisi zisizo za kiserikali (NGO’s) sikumwona. Hakuwepo ofisini na kama ilivyozoeleka katika ofisi za umma zilizo nyingi, kila mtu hataki kusema akidai si msemaji na pengine hata wasemaji hawasemi. Baada ya jibu hilo, nilisimama nje ya ofisi hiyo nikiwa nimechoka, maana raha ya mtafutaji ni kupata anachokitafuta.   Nikiwa bado nimesimama, nikasikia madereva wa magari ya viongozi wa wizara hiyo wakipiga soga, lakini mjadala ukiwa ni mwendelezo wa ‘filamu ya Ponda na wenzake’. Mjadala unanivuta kuwasogelea na kujumuika nao, maana waswahili tunao msemo usemao ‘Sikio halilali njaa’   Kadri mjadala unavyokolea, ndiyo ninavyogundua kwamba madereva hao wanayo majibu ya maswali magumu yaliyonifanya nifunge safari ya kwenda hapo wizarani ingawa taarifa zao si rasmi.
Dereva mmoja anasema kama kuna siku nitakutana na Sheikh Ponda Issa Ponda, nitamuuliza maswal anieleze kwa nini anatumia taasisi hewa (isiyosajiliwa na kutambulika kwa mujibu wa sheria za nchi) kuuchafua uislamu?   Anaendelea kusema, “ukweli hivi sasa dini yetu (ya kiislamu) imechafuka kundi la hawa jamaa limetuchafua katika jamii, kiasi kwamba ninaamini kila mtu anajua Waislamu tuna fujo na vurugu, mimi jambo hilo linaniuma. Uislamu ni dini ya amani na kwa zama hizi, huwezi kueneza dini kwa harakati za mapambano ya kimabavu”.   Msomaji, mjadala huo wa madereva wa viongozi wa wizara unaakisi hali ya mambo katika jamii. Kwamba miongoni mwa jamii, wapo waliokinai na wanaokerwa tena wako tayari kufanya mambo kwa namna ambayo haitarajiwi ili kuhakikisha heshima, hadhi na aiba ya dini yao (ya kiislamu) haichafuliwi na watu wachache.
Hawa wanaamini kwamba harakati za kueneza dini yao (ya kiislamu), inatatizwa na makundi yanayotaka kueneza dini hiyo kwa fujo na vurugu.   Nikirejea maelezo ya madereva wale kwamba kinachoitwa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, ni taasisi hewa. Je imekuwaje imekuwa ikiwasiliana na Serikali kwa nembo hiyo? Itakumbukwa kwamba, viongozi wa taasisi hiyo hewa walialikwa katika semina kuhusu sensa na mwisho wake kukaibuka harakati za kuipinga sensa.
Pia, hivi karibuni taasisi hiyo imemwandikia waziri mkuu kupinga mpango wa kuanzisha kamati za ulinzi na usalama katika msikiti. Je, wangewezaje kumuandkia kama si taasisi inayotambulika na kukubalika kwa viongozi wakubwa?   Maswali yanayochanganya katika filamu hii ni kwamba katika maeneo ya ibada kama hilo, wafuasi au waamini kwa kawaida huwa ni watii na waaminifu kwa kiongozi wao wa kiroho. Je, wanapoamua kurusha mawe kwa Polis.
www.hakileo.blogspot.comWanafanya hivyo bila ruhusa ya viongozi wao au walilazimika kumtii mmoja wa viongozi wao, naye ni nani maana kama yupo naye alitenda kosa kwa kuhamasisha au kuagiza watu kuwazuia Polisi kufanya kazi yao.   Wengine wanajiuliza na kujadiliana wakisema Sheikh Ponda anaendelea kutumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja, kifungo hicho bado hakijaisha na kinaambatana na masharti kwamba asitende kosa lolote katika kipindi hicho.
Hata hivyo katika hali ya uungwana wa kawaida, kwa mtu aliye katika uangalizi huo wa kisheria, anapotuhumiwa kufanya kosa na kutangazwa katika vyombo vya habari kwamba anatakiwa kukamatwa au ajisalimishe, kwa nini ukatae kujisalimisha au awakimbie Polisi hadi yamkute haya?   Kwa muungwana tena ambaye anatajwa kuwa ni kiongozi, anapaswa kuonesha mfano bora kwa umma anaouongoza katika kuzitii mamlaka halali na tena kutii sheria bila shuruti.
Ndiyo sababu kwa kuyasoma mazingira mazima ya ‘filamu ya Ponda na wenzake’, kunatoa viashiria kwamba Watanzania wanatakiwa kuelimishwa ili kuyatambua matakwa ya kisheria, ili kuepuka matendo yanayoweza kutafsiriwa kwamba ni kuvizuia vyombo vya dola kulinda, kuhoji au kukamata kwamba ni kuvizuia vombo hivyo kufanya kazi yao jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi.   Pamoja na hayo watu wanauliza kuwa, baada ya kiongozi huyo kujeruhiwa na kupelekwa hospitali na kisha kuzuka tafrani baina ya wafuasi wa Ponda na wafanyakazi wa hospitali ya Mkoa wa Morogoro, mbona hao waliopigwa na kujeruhiwa wakiwa kazini (hospitalini) na wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Ponda, mbona hakuna anayewasemea ingawa taarifa zipo?   Umma unapenda kufahamu kuwa, baada ya kutoroshwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro, kiongozi huyu wa kiroho alipelekwa wapi na kwa nini alipelekwa huko? Je, kulikuwa na wataalamu wa kutosha kumsaidia vema, au alipelekwa kufanyiwa majaribio ya kutibu? Huko je, alifuata taratibu halisi za matibabu yanayotokana na matukio ya namna hiyo, ikiwemo kuwa na fomu ya Polisi iitwayo PF3 au alitibiwa kimyemela?   Je, huko alipopelekwa kutibiwa, kama hakujulikani vizuri hususan uwezo wa wataalamu na nia iliyokuwapo, kusingekuwa na uwezekano wa kuwapo wasiomtakia mema Ponda na hivyo badala ya kumsaidia, wao wakazidi kumdhuru maana msafara wa mamba siku zote haukosi kenge?
Au, basi hakukuwa na uwezekano wa wengine kutaka kupotosha ukweli wa mazingira ya tukio, ili kuwatwika mzigo wale waliotimiza wajibu wao uliolenga kuhakikisha matakwa ya kisheria yanatimizwa dhidi ya Ponda?   Pia, tunapaswa kujiuliza kwamba tuna uhakika gani kwamba matibabu aliyoyapata uko mafichoni yalikuwa ni salama na hakuwekewa sumu katika dawa na vifaa vilivyotumika?   Kama wanavyosema wengi, hapa ni pagumu kujua ukweli na kupata majibu ya maswali mengi yanayoibuka. Hivi ni kwa nini alitolewa tena kwa namna ya kibabe katika Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Morogoro na kufichwa kusikojulikana?   Ni muhimu jamii ikatafakari pia kwamba wakati mwingine hata nje ya siasa, watu wana mbinu kama za wanasiasa wanapotafuta huruma za watu au umaarufu. Si siri kwa mazingira tulivyomo, busara za Watanzania zinahitajika zaidi kuliko kuongozwa na hisia na jazba.   Hakuna anayefurahia Sheikh Ponda kujeruhiwa, maana ana haki ya kuwa salama na hakuna anayependa kumuona kila wakati anakuwa katika msukasuko na migogoro hata kama yeye anaitaka.
Pia hakuna anayefurahia kusikia kwamba licha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumkuta na hatia na kumpa adhabu ya kifungo cha nje, kwa sharti la kutotenda kosa lingine, eti bado anatuhumiwa kukaidi amri hiyo.
Waswahili tuna msemo wetu, usemao ngoma ikilia sana, ujue… Pia, sanjari na hilo ni muhimu wanaoshabikia “filamu ya Ponda na wenzake” wakafahamu kwamba, sasa watanzania walio wengi wameanza kuikinai!
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company