“EX Africa simper aliquid novi” ni maneno yaliyopata kutamkwa na mwanafalsafa maarufu wa kale wa Kiyunani, Ptolemy, yakiwa na maana kwamba kila kukicha kitazuka kioja kingine Afrika. Kwa mambo yalivyo hivi sasa, naweza pia kuyatumia maneno hayo kwa nchi yetu: Ex Tanzania simper aliquid novi. Naam, kila kukicha kinazuka kioja kingine Tanzania.
Kama si mauaji ya vikongwe, ni mauaji ya albino. Kama si kikombe cha babu Loliondo, ni kuwanga kwa mbunge bungeni. Kama si ufisadi wa Meremeta, ni ufisadi wa EPA, Richmond, Downs, Kiwira, UDA, kuuziana nyumba za serikali, twin towers, kutorosha nje wanyama hai, biashara haramu ya meno ya tembo na magogo.
Kama si kituko cha mauaji ya polisi ya mwandishi wa habari (Mwangosi), ni utekwaji na uteswaji wa Dk. Ulimboka na wa mwandishi Absalom Kibanda. Kama si umwagiwaji wa tindikali wa mmiliki wa Home Shopping Centre, ni umwagiwaji tindikali wa wasichana wawili wa Uingereza waliokwenda Zanzibar kwa kazi za kujitolea.
Kama si polisi kurusha mabomu kwenye mkutano wa hadhara wa CHADEMA huko Arusha na kuua watu, ni kumshambulia na kumjeruhi Sheikh Ponda wakati akihutubia waumini huko Morogoro.
Kama si wakazi wa Mtwara kugomea gesi kusafirishwa Dar es Salaam, na hivyo kukaribisha vipigo vya polisi, ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa agizo kwa polisi la “piga tu” watuhumiwa!
Kama sio kufeli kwa zaidi ya asilimia 60 kwenye mtihani wa taifa kwa wahitimu wa kidato cha nne, ni uamuzi wa serikali wa kushusha viwango vya alama za kufaulu ili sasa kila aliyefeli aonekane amepasi!
Kama si kigogo kuwekewa kwenye akaunti ya nje mgao wake wa ununuzi wa kifisadi wa rada, ni Benki Kuu ya Uswisi kutangaza kuwa vigogo kadhaa wa Tanzania wameficha mabilioni katika mabenki ya nchi hiyo.
Kama si ndege ya kijeshi ya Qatar kutua nchini na kutorosha twiga wetu hai kuwapeleka Uarabuni, ni visichana viwili vya Kitanzania kukamatwa na kilo 180 za ‘cocaine’ huko Afrika Kusini walizozipitisha uwanja wetu wa ndege wa Dar es Salaam!
Naam, ex Tanzania simper aliquid novi. Kila kukicha kuna kituko kipya Tanzania! Unaweza kukisikia kimoja, na ukasema hapo ndipo kikomo chetu, lakini kesho yake utakisikia kingine kikubwa kupita kile cha jana, na keshokutwa vivyo hivyo!
Ni kwa kuzingatia yote hayo, namwonea huruma Rais Kikwete kwa anavyohangaika kusafiri kwa wakubwa huku na huko duniani akijaribu kuwajengea picha kuwa Tanzania mambo ni safi na poa – waje wawekeze na waje kutumwagia mapesa ya misaada!
Yaani anahangaika kuiweka nchi na yeye binafsi kwenye centre stage ya masuala ya dunia ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini kila anavyohangaika kuisafisha Tanzania huko nje ndivyo pia inavyozidi kuchafuka.
Tafakari mfano huu wa hivi karibuni. Wakati Rais Kikwete anashusha pumzi kwa furaha kwa kutembelewa na Rais wa sasa wa Marekani na wengine wawili wa zamani, na pia kutembelewa na Rais wa China – ziara zilizoipandisha kidogo chati Tanzania kimataifa, skandali ya biashara ya madawa ya kulevya na ya kumwagiwa tindikali kwa wasichana wawili wa Kiingereza waliokwenda Zanzibar kufanya kazi za kujitolea, zinaibuka na kudakwa na vyombo vya habari vya kimataifa. Ni dhahiri skandali hizi zimepunguza mno mafanikio hayo ya Kikwete ya hivi karibuni ya kuitangaza vyema Tanzania.
Kwa sasa, kinachozungumzwa Beijing (China) si tena suala la maliasili zetu kupatikana kwa wageni kirahisi na kwa utaratibu ‘poa’; bali ni kubobea kwa Watanzania katika biashara haramu ya ‘cocaine’ (mihadarati) duniani.
Kwa sasa, kinachozungumzwa London (Uingereza) na Washington (Marekani) si tena ni sifa za uchumi wa Tanzania kukua na nchi kuwa na utawala bora; bali ni habari za mabinti hao wa Kiingereza kumwagiwa tindikali Zanzibar; ilhali walikwenda huko kufanya kazi za kujitolea.
Nina hakika, kwa mtu anayependa kusifiwa na mataifa makubwa kama Rais Kikwete, baadhi ya matukio hayo yanayoipaka matope Tanzania yanamsononesha na kumkosesha sana raha. Nimetumia maneno “baadhi ya matukio”, kwa sababu sina hakika kama yote yanamkosesha raha kwa kiwango kikubwa kama yanavyowakosesha raha Watanzania wengine!
Vyovyote vile, jaribu kujenga picha kichwani mwako ya Mtanzania ambaye sasa akiwasili kwenye uwanja wowote wa ndege wa miji mikubwa duniani hupekuliwa kidhalilishaji (kuvuliwa nguo zote kama huko Beijing), kwa sababu tu ni Mtanzania (na Watanzania ndiyo wanaosifika kwa kusafirisha madawa ya kulevya), utaelewa ni kiasi gani nchi yetu imechafuka nje.
Mfikirie, anajisikiaje, kwa mfano, Mtanzania anayejitambulisha kwenye mkutano wa kimataifa huko Sweden, na kisha wakati wa mapumziko Wazungu wanamwendea na kumuuliza: “Ah unatoka Tanzania walikomwagiwa tindikali mabinti wawili wa Kiingereza waliokuja kwenu kujitolea?”
Ndugu zangu, naishiwa maneno ya kuyatumia kueleza ni kwa kiasi gani ufisadi na uhalifu unaoendelea Tanzania unavyoipaka matope nchi yetu huko nje. Hata hivyo, nirejee katika kukisema kile ambacho nimekuwa nikikisema huko nyuma kwenye safu hii, na ambacho sitachoka kurudia kukisema; nacho ni kwamba nchi yetu inapitia kipindi kigumu mno kuliko vipindi vyote tangu tupate uhuru wetu mwaka 1961.
Jambo la kukumbuka ni kwamba hatukufika hapa mara moja, bali tumefika hapa kwa kupiga hatua moja hadi nyingine. Ufisadi mmoja ulizembewa kudhibitiwa ukazaa ufisadi mwingine ambao nao ulizembewa kudhibitiwa, na kisha nao ukazaa ufisadi mwingine uliozembewa nao kudhibitiwa….nk; yaani ni mkusanyiko wa ufisadi usiodhibitiwa juu ya ufisadi usiodhibitiwa, na sasa karibu taasisi zote za kiutawala zimeoza kiutendaji - zimwi la ufisadi limekuwa kubwa kiasi cha watawala kushindwa kulidhibiti.
Nikirejesha fikra zangu nyuma, naamini kwamba tulipokosea ni pale tulipoachana na miiko ya uongozi na maadili ya uongozi, na hivyo kukaribisha ufisadi kustawi katika kada za uongozi na kusambaa kwa wananchi wote. Wananchi wakiona wakubwa wanakwiba, wanatajirika, na hawafungwi, nao watafuata nyayo!
Ni maoni yangu kwamba, kila uovu niliouzungumzia mwanzoni mwa safu hii unaoipaka matope Tanzania huko nje asili yake ni ufisadi. Kuuawa kwa albino ni ufisadi, kumwagiana tindikali ni ufisadi, kutekana na kutesana ni ufisadi, biashara ya ‘cocaine’ ni ufisadi, biashara haramu ya magogo na pembe za ndovu ni ufisadi, kuuziana nyumba za serikali ni ufisadi nk! Ni kama vile kasha la Pandoralimefunguliwa na kila aina ya ufisadi umetoka na kusambaa kote nchini!
Isitoshe, ukishajenga utamaduni wa kutokuwashitaki na kuwafunga mafisadi (impunity culture), na tena ukiwazawadia kwa kuwapa vyeo, maana yake ni kwamba unatuma ‘meseji’ kwa Watanzania wote kwamba ufisadi ‘unalipa’; yaani kwamba ukitaka mafanikio ya maisha kwa njia ya mkato, jitose kwenye ufisadi.
Hali hii imewafanya Watanzania wengi, hususan vijana, wasiamini tena kwamba hali bora ya maisha au utajiri unapatikana kwa kuchapa kazi halali. Wengi sasa wanaamini kwamba ukitaka utajiri jiingize kwenye njia ya mkato ya kuufikia – nayo ni ufisadi.
Kwa bahati mbaya, wanaoamini hivyo wana mifano ya kweli ya majina ya watu matajiri au ya viongozi matajiri ambao jana walikuwa watu wa kawaida tu, lakini leo baada ya kujitosa kwenye ufisadi ni matajiri wakubwa wanaoogopwa hata na watawala wenyewe!
Kwa hiyo, kwa vijana na Watanzania wengine, ukitaka kumiliki nyumba ya kifahari au kuendesha hammer, jibu si kuchapa kazi halali, bali ni kutafuta njia ya mkato, na haijalishi kama ni kusafirisha nje ‘cocaine’ au ni biashara haramu ya pembe za ndovu au magogo au hata kuwa mtu wa kukodiwa kuua wengine (hitman) au kuwamwagia tindikali!
Hayo ndiyo matunda tunayoyavuna hivi sasa baada ya kupandikiza, nchini mwetu, kwa miaka 20, mbegu za impunity culture; hasa baada ya kutelekeza miiko ya uongozi na maadili ya uongozi aliyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Kuna rafiki yangu mmoja alipata kuniambia kwamba katika watawala wa sasa wa Tanzania, hakuna aliye msafi kiasi cha kuweza kumkemea mwenzake au kumchukulia hatua mwenzake.
Naanza kuliamini hilo, kwa sababu, hata hizo hatua ambazo serikali inafurukuta za kuwakamata mafisadi wanaofanya uovu huo unaopaka matope nchi yetu, zinaishia kwenye vijidagaa tu; ilhali mipapa inaendelea kuwa huru.
Kwa mfano, tumesikia mara kadhaa, kwa midomo ya mawaziri wenyewe, kwamba washiriki wa biashara haramu ya madawa ya kulevya, ya magogo na pembe za ndovu, ni watu wakubwa serikalini wenye mitandao mikubwa.
Lakini natujiulize: Ni kigogo gani aliyekamatwa mpaka sasa? Au natujiulize swali jingine muhimu zaidi: Ni kigogo gani, hivi sasa, anayetumikia kifungo baada ya kutiwa hatiani kwa ufisadi? Jibu ni hakuna.
Kwa hakika, kinachoonekana hapa Tanzania katika vita hii dhidi ya ufisadi ni juhudi za waziri mmoja mmoja hapa na pale – na hata hao huishia tu kwenye kuandama vijidagaa tu, na si kuwagusa wakubwa wenzao! Jiulize tena: Katika jaribio hili la hivi sasa la kuidhibiti biashara ya madawa ya kulevya, anasikika tu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe. Mawaziri wengine wako wapi? Waziri Nchimbi (kwa mfano) yuko wapi wakati jeshi la polisi liko chini yake?
Hitimisho langu ni kwamba vita hii dhidi ya ufisadi haitafanikiwa kwa sababu inaendeshwa dhidi ya vijidagaa na waziri mmoja mmoja, na si serikali nzima.
Na ndiyo maana vituko vya ufisadi vinavyoipaka matope Tanzania vitaendelea kuibuka kila mara katika sura mbalimbali. Naamini, vilevile, kwamba Rais Kikwete hataweza kulisafisha jina la Tanzania lililochafuliwa nje katika miaka yake hii miwili na ushee aliyobakisha Ikulu kama bado hatajipa ujasiri wa kuwakamata vigogo, kuwafikisha mahakamani na hatimaye kufungwa gerezani.
Ni kwa njia hiyo tu ya kuonyesha mfano wa kuwafunga gerezani vigogo mafisadi nchini, tunaweza kutuma ‘meseji’ nyingine kwa Watanzania wote kwamba, ufisadi na uhalifu wa aina yoyote haulipi, na kwamba mahali pa kuishi wanaoshiriki uovu huo ni gerezani.
Naamini kwamba bila kufanya hivyo, Tanzania itaendelea kupanda chati ya nchi ovu (devilish countries) duniani, na kwamba kina Bernett wa kipindi cha CNN cha Inside Africa watakuja Tanzania kufuatilia habari si za kukua kwa uchumi wetu, bali za matajiri wetu wa ghafla wa ‘cocaine’ au wa pembe za ndovu nk.
Tunavyoenenda kwa kuzidi kukumbatia impunity culture, sitashangaa ukiibuka uhalifu mwingine mpya nchini wa Watanzania kuuana kwa kutoleana figo milini mwetu ili kuziuza Ughaibuni! Ex Tanzania simper aliquid novi!