RAIS Jakaya Kikwete amesema habari kuwa Tanzania iko mbioni kuingia vitani na nchi jirani za Malawi na Rwanda zinachochewa na baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo vinataka kutumia matatizo yaliyopo kisiasa.
Akizungumza nchini Malawi mwishoni mwa wiki, Rais Kikwete alisema yeye kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania hajawahi kuagiza majeshi yake kuvamia nchi yoyote ile au kukaa mkao wa kivita.
“Mimi ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania. Sijawahi kuagiza majeshi yangu yakae mkao wa kivita na wala kwenda vitani. Hivyo kama mimi sijawahi kutoa maagizo hayo, taarifa zote mnazozisikia haziwezi kuwa za kweli,” alisema Kikwete mara baada ya kumaliza mkutano wake na Rais Joyce Banda wa Malawi.
Rais Kikwete alikwenda Malawi kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Lilongwe, Malawi.
Ziara hiyo ya Rais Kikwete ilikuwa katika kipindi ambacho nchi hizi mbili zimekuwa katika vuta nikuvute ya maneno kuhusu umiliki wa Ziwa Nyasa ambalo Malawi inadai lote ni lake huku Tanzania ikidai pia kumiliki sehemu ya ziwa hilo.
Kikwete, kupitia mkutano wake huo na Rais Banda, aliwahakikishia Wamalawi kwamba Tanzania haina mpango wa kuingia vitani na Malawi na kwamba kwa muda mrefu imekuwa ikifurahia uhusiano mwema baina ya nchi hizo mbili.
Vyanzo vya gazeti hili kutoka katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, vinaeleza kwamba katika mkutano huo baina ya marais hao wawili, makubaliano muhimu yalifikiwa.
“Kwanza ilikuwa ni kuundwa rasmi kwa kamati maalumu ya pamoja kati ya nchi hizo mbili ambayo lengo lake kubwa litakuwa ni kujadili nini kifanyike ili suala la Malawi limalizwe kwa amani.
“Nafahamu mkutano wa kwanza wa kamati hiyo umepangwa kufanyika Jumanne ya wiki hii, kule katika mji wa Mzuzu uliopo kaskazini mwa Malawi na baada ya hapo mambo mengine yatafuata,” kilisema chanzo hicho cha gazeti hili.
Raia Mwema lilielezwa kwamba wananchi wengi wa Malawi walimwamini Kikwete kwa sababu ya tabia yake ya kumwita Banda “Dada yangu” kila wakati alipomtaja, jambo lililoonyesha ukaribu baina ya viongozi hao.
“Kwa kweli ziara ya Kikwete Malawi ilikuwa na mafanikio makubwa, hususan katika suala zima la uhusiano baina ya nchi zetu mbili. Kama ungewaona viongozi hao wawili usingejua kabisa kwamba eti nchi zao zinakaribia au ziko kwenye mgogoro mkubwa, gazeti hili limeambiwa na mmoja wa wana diplomasia wa Tanzania waliokuwemo kwenye msafara wa Kikwete nchini humo.
Katika mkutano huo, Rais Banda alimshukuru Kikwete kwa kukubali kutumia muda wake mfupi nchini mwake kuzungumzia pia suala la Ziwa Nyasa kwa vile taarifa mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kupitia vyombo vya habari, zilikuwa zikiwatisha wananchi pasipo sababu.
Wakati huohuo, vyombo vya habari vya Malawi vimeandika namna viongozi wa SADC walivyokuwa wakiwatania marais Banda na Kikwete kutokana na mzozo wao kuhusu ziwa hilo.
Wakati akifungua mkutano huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa SADC, Rais Armando Guebuza wa Msumbiji, alitania kwamba viongozi hao wana kazi ya kutanzua mgogoro huo wa Tanzania na Malawi, na Rais wa Zambia, Michael Satta, akadakia kutoka katika kiti chake na kusema; “Kama wataanza kupigana, tutakuwa tayari kupokea wakimbizi.”
Mbali na masuala hayo, mkutano huo wa SADC ulimpa uenyekiti Rais wa Malawi, Joyce Banda huku Rais Jakaya Kikwete akikamilisha ngwe yake ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi, Siasa na Usalama (TROIKA) ya SADC na Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara ya Afrika Mashariki, Dk. Stregomena Tax Bamwenda akichaguliwa kuwa Katibu Mtendaji wa SADC, akimbwaga kwa kura Waziri wa Uwekezaji, Maliasili na Viwanda wa Seychelles, Peter Sinon.
Katika hatua nyingine, kijiti alichokiacha Kikwete cha uenyekiti wa Troika kimechukuliwa na Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba. Pohamba aliwahi kuishi Tanzania kama mkimbizi wa kisiasa na taarifa zinaonyesha kwamba alikuja Tanzania (Tanganyika) kwa mara ya kwanza tarehe 9 Desemba 1961, siku ambayo nchi hiyo ilipata Uhuru wake.