skip to main |
skip to sidebar
Na Fidelis Butahe kwa hisani ya mwananchi gazeti
Balozi Sefue alisema Rais Kikwete ameanzisha kitengo kipya katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), kitakachokuwa kikishughulikia afya ambacho kitasimamiwa na Dk Mtasiwa.
inShare
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa makatibu wakuu kumi na mmoja na naibu makatibu wakuu 14 wapya katika wizara mbalimbali.
Miongoni mwa walioteuliwa ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Sifuni Mchome ambaye sasa anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deodatus Mtasiwa ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu, Tamisemi.
Mtasiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni walisimamishwa kazi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Februari, mwaka jana kupisha uchunguzi dhidi yao, kutokana na kukithiri kwa migomo ya madaktari nchini, pamoja na utendaji wao kulalamikiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema: “Mtasiwa ameteuliwa kwa kuwa uchunguzi dhidi yake haujaonyesha kuwa ana kosa lolote, lakini wenzake (Nyoni) na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo bado wanachunguzwa.
Katika uteuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo amehamishiwa Ikulu kusimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), kuwa Naibu Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo.
Makatibu wakuu walioachwa kwa maelezo kuwa watapangiwa kazi nyingine ni Sethi Kamuhanda (aliyekuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Kijakazi Mtengwa (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) na Omary Chambo (Uchukuzi), huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa akistaafu wa hiari.
Balozi Sefue alisema Rais Kikwete ameanzisha kitengo kipya katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), kitakachokuwa kikishughulikia afya ambacho kitasimamiwa na Dk Mtasiwa.
Aidha, aliwataja makatibu wakuu waliohamishwa wizara kuwa ni Florens Turuka kutoka Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu na Joyce Mapunjo kutoka Viwanda na Biashara kwenda Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Makatibu wakuu wapya
Alisema Jumanne Sagini ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Dk Servacius Likwelile ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo. Dk Patrick Makungu ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia pia ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Alfayo Kidata ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.