www.hakileo.blogspot.com
Na Aidan Mhando
Kwa ufupi
- Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana huku ubomoaji ukiendelea, mmoja wa waathirika wa bomoabomoa hiyo, alilalamikia ubomoaji kufanyika kibaguzi.
Dar es Salaam. Wakazi wa Mbezi Beach, Tegeta na
Wazo katika Manispaa ya Kinondoni wamelalamikia kazi ya ubomoaji wa
nyumba zao ili kupisha utandazaji wa bomba la majisafi la Mamlaka ya
Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), kwamba inafanywa kwa
ubaguzi.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa Dawasa ilitoa siku 14
kwa wakazi hao kubomoa nyumba zao zipatazo 400 kupisha mradi huo wa
bomba utakaogharimu Sh120 bilioni.
Dawasa imelaumiwa kutokana na baadhi ya nyumba za
vigogo na watumishi wa Serikali kuachwa licha ya kuwekewa alama ya X
kuashiria zinatakiwa kubomolewa.
Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa eneo la tukio,
alishuhudia baadhi ya wananchi hao wakidai kuwa moja ya nyumba ambayo
imeachwa ni ya ndugu wa mmoja wa vigogo wa Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana huku
ubomoaji ukiendelea, mmoja wa waathirika wa bomoabomoa hiyo,
alilalamikia ubomoaji kufanyika kibaguzi.
Juma Shaaban alisema: “Ninashangaa kuona
tunabomolewa nyumba zetu huku nyumba zao zinaachwa,“Ninaweza kukuonyesha
nyumba ya ndugu yake kigogo (anamtaja) imewekewa X, lakini
chakushangaza haijabomolewa, hii tulalamike.”alisema.
Mkazi mwingine wa Tegeta, Khamis Ramadhani
alisema: “Tunashangazwa na bomoabomoa hii kufanyika bila hata kutupa
muda wa kuhamisha mali zetu.”
Katika hatua nyingine, bomoabomoa inayoendelea
ilisababisha hitilafu ya umeme na kusababisha moto ulioteketeza Baa
maarufuya Samaki Samaki.
Moto huo ulitokea Saa 4 asubuhi na kusababisha
watu kujaa na kufungwa barabara kwa muda ili kuzima moto huo kabla ya
magari ya kuzima moto kuwasili eneo la tukio