Zitto amkaanga Magufuli


Zitto-Kabwe[1]

Na Charity James WA JAMBO LEO
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema Wizara ya Ujenzi imetumia vibaya sh. bilioni 348 ilizoomba kwa ajili ya ujenzi wa barabara na badala yake ilizitumia kulipa wakandarasi.   Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe baada ya kamati hiyo kukutana na viongozi wa wizara hiyo ambayo inaongozwa na Dk. John Magufuli.
Zitto alisema wizara hiyo ilipeleka taarifa bungeni ya kutaka iidhinishiwe kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi maalumu wa barabara kwa mwaka 2011/12, lakini zimetumika vibaya.
Kutokana na hali hiyo, Zitto alisema wizara hiyo imelidanganya, Bunge kuhusiana na fedha hizo, hivyo watawasilisha suala hilo Kamati ya Maadili ya Bunge ili Dk. Magufuli ahojiwe.   Alisema katika ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), ilibainika kilichofanyika ni ujenzi vivuli.
Alisema katika ujenzi huo ilibainika kuwa wizara iliomba kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi huo, lakini Hazina iliwakabidhi sh. bilioni 100 kwa ajili ya kutekeleza suala hilo.WWW.HAKILEO.BLOGSPOT.COM
Zitto alisema kilichofanyika ni tofauti na kile wizara ilichoomba. Pia kamati hiyo ilisema wizara hiyo ina madeni mengi ambayo yanafikia sh. bilioni 252 ya miaka iliyopita.
Pamoja na mambo mengine, alibainisha kuwa wizara hiyo haina mpango mkakati hivyo kamati imetoa muda kwa wizara kuunda mpango mkakati hadi ifikapo Desemba mwaka huu.   LAAC
Wakati huo huo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imesema sh. bilioni 1.2 za Halmashauri ya Mvomero mkoani Morogoro hazifahamiki zilipo.   Kutokana na hilo, kamati hiyo imemwita aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Sara Niluma na aliyekuwa mweka hazina, Kabilile Stim kufika mbele ya kamati hiyo ili kueleza fedha hizo zilivyotumika.   Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ofisi Ndogo za Bunge, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Selemani Zed, alisema mamilioni hayo ya fedha hayafahamiki yameenda wapi.   Alisema CAG alipofanya ukaguzi kwenye halmashauri hiyo alibaini kiasi hicho cha fedha kimetumika vibaya. Alisema fedha hizo ni za mwaka wa fedha 2011/2012.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company