SERIKALI imetakiwa kueleza ni kwanini imeua kiwanda cha kutengeneza redio aina ya Philips kilichoko mjini Arusha.
Hoja hiyo iliibuliwa bungeni jana na mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema (CHADEMA).
Mbunge huyo aliitaka serikali itoe maelezo ni kwa nini iliamua kuua kiwanda hicho na kusababisha kuagiza redio kutoka nje.
Katika swali la msingi, mbunge wa Mji Mkongwe, Muhammad Ibrahim Sanya (CUF), alitaka kujua kama serikali haioni kuwa umefika wakati wa kutafuta mwekezaji ili kuwepo kiwanda cha kutengeneza betri za redio zenye viwango.
“Wananchi wengi hususan vijijini ambao njia pekee ya kupata taarifa mbalimbali za masuala yanayohusu kilimo, afya, uchumi na maendeleo hupatikana kupitia matangazo ya redio na redio hizo hutumia betri ambazo huingizwa kutoka nje ya nchi, lakini zikiwa katika viwango hafifu na zisizodumu muda mrefu.
“Je, serikali haioni kuwa umefika wakati wa kutafuta mwekezaji ili kuwepo kiwanda cha kutengeneza betri za redio zenye viwango,” alihoji mbunge huyo.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gergory Teu, alikiri idadi kubwa ya Watanzania hususan wanaoishi vijijini wanapata taarifa mbalimbali kupitia matangazo ya redio zinazotumia betri.
Teu alisema kwa sasa Tanzania ina upungufu wa betri milioni 15 kwa mwaka tofauti na mahitaji halisi ambayo ni betri milioni 250 kwa mwaka.
Alisema kuna kiwanda cha Panasonic Battery (T) Co.Ltd ambacho kinazalisha betri milioni moja kwa mwaka wakati mahitaji ni zaidi ya betri milioni 250.
Alisema kuwa kutokana na mahitaji ya betri kuwa makubwa nchini kampuni ya Tiger Head kutoka China imeingia mkataba na serikali wa kujenga kiwanda nchini cha kuzalisha betri.