KOVA; `Vifo vya watoto bwawa la kuogelea ni uzembe`

NA JIMMY MFURU
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Kamishna Suleiman Kova

Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kwamba tukio la watoto watatu kufa maji wakati wakiogelea katika bwawa la Hoteli ya Land Mark, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ni uzembe.

Watoto hao walikumbwa na mkasa huo Jumapili iliyopita walipokwenda hotelini hapo kwa ajili ya sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa mwenzao.

Maofisa wa wizara hiyo Kitengo cha Leseni (Tala), ambao hawakutaka majina yao kutajwa gazetini, waliiambia NIPASHE jana kuwa kitendo cha kuwaacha watoto wadogo kuogelea bila muangalizi ni kinyume cha biashara ya uendeshaji hoteli kwa mujibu ya Sheria ya Usajili wa Biashara ya Utalii ya mwaka 2008.

Walisema kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa huduma za hoteli za kitalii, ni lazima kuwa na wataalamu wanaosimamia shughuli na utoaji huduma mbalimbali ndani ya hoteli.

Walisema kwa upande wa mabwawa ya kuogelea katika hoteli, zinatakiwa kuwa na wahudumu maalum wenye taaluma husika ambao wanatakiwa kusimamia wateja wao muda wote.

Walifafanua kuwa hata kama msimamizi anatakiwa kuundoka mara moja, ni lazima awepo mtu mbadala wa kusimamia watu wanaoogelea bila kujali umri.

Aidha, walisema katika eneo la bwawa lazima kuwe na waokoaji ambao wanatakiwa kuwepo muda wote kuanzia mmoja hadi watano kutegemea na kina cha maji, kuwepo na maboya na kamba kwa ajili ya kuwasaidia wateja ikiwa litatokea tatizo.

Waliongeza kuwa lazima kuwepo na tahadhari kwa watu waliolewa kutoruhusiwa kuogelea pamoja na kuwazuia watoto wadogo kuogelea katika kina kirefu cha maji.

Alisema wao hawahusiki katika kuchukua hatua, isipokuwa wanaoweza kufanya hivyo ni vyombo vingine likiwamo Jeshi la Polisi ikiwa itathibitika kuwapo kwa uzembe.

Watoto hao waliokufa ni Ndimbuni Bahati (09), Eva Nicholous (09) na Janeth Zacharia (10).

Habari zinaeleza kuwa watoto hao walikuwa wanaogelea katika bwawa la watoto, lakini kutokana na kuwa wengi, baadhi yao walitoroka na kwenda kuogelea katika bwawa la wakubwa lenye kina kirefu cha maji.

Hata hivyo, mwangalizi wa bwawa hilo, Chriss Patrick, alisema watoto hao walikuwa wanakula chakula jirani ya bwawa hilo, lakini ghafla walianza kukimbizana na kurukia katika bwawa la wakubwa wakati yeye akiwa kwenye bwawa la watoto.

Alisema siku hiyo alikuwa zamu peke yake kutokana na mwenzake aliyetakiwa kuwa naye zamu kupata udhuru kutokana na kuumwa.

Patrick alisema kutokana na kuwa peke yake, alizidiwa majukumu na kushindwa kuwaokoa watoto hao.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa hoteli hiyo, Wallace Chege, alisema watoto hao walikwenda katika hoteli hiyo kwa ajili ya kupata huduma ya chakula bila kulipia gharama za huduma ya kuogelea.

Chege alisema wakati mwangalizi akiwa anaangalia upande wa bwawa la watoto ndipo watoto hao walianza kukimbizana na kurukia kwenye bwawa la wakubwa kitu kilichopelekea vifo hivyo.

Hata hivyo, hakueleza sababu zilizosababisha hakueleza sababu za hoteli yake kutokuwa na idadi ya kutosha ya waangalizi kama sheria inavyotaka.

Familia mbili za marehemu Janeth Kihoko na Ndimbuni Sisala juzi zilisema kwamba wamesamehe na kusema wanamuachia Mungu.

Majomba wa Janet, John Mbugi, alisema jana kuwa walisafirisha mwili wa marehemu kwenda Iringa kwa maziko na wa Ndimbuni ulipelekwa Mbeya.

Naye Nicholas Mwakatobe, alisema mwili wa binti yake, Eva Mwakatobe, utazikwa leo katika makaburi ya Sinza, jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alipoulizwa jana kama wamiliki wa hoteli wamehojiwa kuhusiana na tukio hilo na kusisitiza kuwa suala hilo amemuachia Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura.

Hata hivyo, Kamanda Wambura alipoulizwa, siku nzima jana alikuwa akipokea simu na kusema yuko kwenye kikao.
CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company