Ndugu, jamaa na marafiki wakiwa nje ya chumba cha maiti hospitali ya mkoa wa Singida, wakisubiri kuchukua miili ya ndugu zao waliokufa kwa kugongwa na basi la Kampuni ya Sumry wakati wakishirikiana na polisi kubeba mwili wa mwendesha baiskeli aliyekufa baada ya kugongwa na lori kwenye barabara kuu ya Singida-Dodoma eneo la Utaho wilaya Ikungi.PICHA: ELISANTE JOHN.
Jeshi la Polisi limepata pigo kutokana na askari wake wawili kuuawa kwa kupigwa risasi na majambazi na wengine wanne kufa kwa kugongwa na basi pamoja na watu wengine 15.
Askari wawili wa jeshi hilo waliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi katika Tarafa ya Usoke wilayani Urambo mkoani Tabora.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Suzan Kaganda, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku katika kijiji cha Usoke.
Kamanda Kaganda aliwataja askari waliouawa kuwa ni PC Shaban namba G 3388 ambaye alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi na majambazi hao na PC Jumanne namba F.5179 aliyejuruhiwa tumboni na baadaye kufariki dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete wakati akipatiwa matibabu.
Kamanda Kaganda alisema majambazi watatu walivamia nyumbani kwa mfanyabiashara, Ibrahim Mohamed, mkazi wa Usoke kisha kupora fedha tasilimu Sh. milioni 1.2. Mbali ya kufanya uporaji huo, yalipora vocha za simu zenye thamani ya Sh. 120,000.
Alisema baada ya askari hao kupata taarifa ya uharifu huo, walienda eneo la tukio kwa ajili kutoa msaada, lakini wakiwa mita chache kabla ya kufika katika eneo la tukio, walikutana na majambazi hao na kuanza kuwafyatulia risasi kwa kasi na kumuua PC Shaban.
“Ndugu zangu waandishi wa habari hili ni pigo kubwa sana kwa Jeshi la Polisi, lakini naapa kuwasaka hadi kuwakama wakiwa hai au wafu, sasa tumechoka na uharifu huu,” alisema Kaganda.
Kamanda huyo alisema kabla ya tukio la mauaji ya askari hao, majambazi hao yalifyatua risasi hovyo hewani mfululizo kwa lengo la kuwatisha raia na kwamba maganda 25 ya risasi aina ya SMG na SAR yaliokotwa katika eneo la tukio.
Kufuatia tukio hilo jeshi la Polisi mkoani Tabora linaendesha msako na tayari watu watano wametiwa mbaroni kuhusiana na tukio hilo.
Katika tukio la pili, askari polisi wanne wamekufa pamoja na watu wengine 15 baada ya kugongwa na basi la lililokuwa linatokea Kigoma, katika kijiji cha Utaho, wilayani Ikungi, barabara kuu ya Sindida- Dodoma.
Aidha, watu wengine wanane wamejeruhiwa katika ajali hiyo ilitokea juzi usiku saa 2:45 na kulihusisha basi namba T 799 BET Nissan mali ya kampuni ya Sumry lililokuwa likitokea Kigoma kwenda Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa Singida, Geofrey Kamwela, alisema siku ya tukio hilo wananchi wakiwa na askari polisi wa doria walikuwa wamekusanyika pembezoni mwa barabara kuupakia mwili wa mwendesha baiskeli, Gerald Zefania, aliyegongwa na lori na kufa papo hapo siku hiyo saa 1:30 jioni.
Alisema wakati wakiupakia mwili huo kwenye gari la polisi namba PT 1424 huku likiwa limeegeshwa pembeni mwa barabara, basi hilo lilitokea ghafla kwa kasi na kuwagonga watu 15 na kufariki dunia papo hapo, wengine wanne walikata roho wakati wakipelekwa hospitalini.
Kamanda Kamwela alisema dereva wa basi hilo, Paulo Njilo, mkazi wa jijini Dar es Salaam baada ya kukaribia eneo hilo aliliona gari la polisi likiwa limeegeshwa pembeni kushoto mwa barabara, lakini wakati akijaribu kulikwepa ndipo alipoliparamia kundi la watu waliokuwa na askari.
Aidha, alisema dereva wa basi hilo baada ya ajali hiyo aliendelea na mwendo hadi aliposimama kilomita 25 katika makao makuu ya Wilaya ya Ikungi na kutokomea kusikojulikana, lakini juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Aliwataja askari waliokufa kuwa ni F.849 D/CPL Boniface Magubika wa CID Wilaya ya Singida, F.6837 Pc Jumanne Mwakihaba wa FFU Singida, G.7993 Pc, Novatus Tarimo wa ofisi ya RCO na G.8948 Pc, Michael Mwakihaba wa FFU Singida.
Wengine ni Ofisa Mtendaji Kijiji cha Utaho, Ramadhan Mjengi; Mwenyekiti wa Kijiji Utaho, Paul Hamis; Mwenyekiti wa Kitongoji cha Utaho, Ernest Salanga; Said Rajab, Usirika Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhan, Mwinyi Hamis na Issa Hussein, wote wakazi wa kijiji cha Utaho.
Kamanda Kamwela alisema miili ya marehemu wengine wanne bado haijatambuliwa na ndugu zao na imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Kamanda Kamwela alisema majeruhi wawili wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa Singida na wengine sita wapo hospitali ya Misheni Malikia wa Ulimwengu iliyopo Puma.
Aliongeza kuwa miili ya askari polisi inatarajiwa kusafirishwa kwenda katika mikoa wanakotoka wakati wowote baada ya taratibu za kipolisi kukamilika ikiwamo kuwasiliana na ndugu zao walioko mikoa ya Kilimanjaro, Pwani, Mbeya na Iringa.
MAJERUHI AZUNGUMZA
Mmoja wa majeruhi aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa Singida, Mussa Mohammed, alisema kuwa wakati wakisubiri kuupakia mwili wa marehemu Gerald, basi hilo lilitokea ghafla na kwa kasi na lilikwepa gari la polisi lililokuwa limesimama kisha kuparamia kundi la watu na tangu hapo hakujielewa hadi alipozinduka jana asubuhi akiwa hospitalini.
Kamanda Kamwela alisema uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea ili kujua chanzo cha ajali hiyo.
AJALI ZA AINA HII
Mazingira ya ajali hii yanafanana na ajali mbili zilizotokea hivi karibuni.
Machi 29, mwaka huu, ajali iliua watu 21 na kujeruhi wengine tisa katika Kata ya Mkupuka, wilayani Rufiji, barabara ya Dar es Salaam-Kilwa mkoani Pwani.
Kati ya watu hao, saba walikufa papo hapo baada ya magari mawili aina ya Mitsubishi Canter na Toyota Hiace kugongana uso kwa uso na wengine 14 kuparamiwa na basi wakati wakiwaokoa majeruhi. Basi hilo lililokuwa linatokea mkoani Lindi kwenda Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilitokea saa 24 baada ya nyingine iliyosababisha watu 12 kufa papo hapo na wengine saba kujeruhiwa nje kidogo ya mji mdogo wa Hedaru, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
CHAGONJA AJA JUU
Jijini Dar es Salaam, makao makuu ya jeshi hilo, yametangaza msako mkali kwa majambazi na kuwashughulikia madereva wazembe.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na kuhusiana na matukio yaliyo tokea Singida na Tabora.
Chagonja alisema ajali ya basi la Summry ilitokana na uzembe wa dereva ambaye alikiuka sheria za usalama barabarani.
Alisema katika ajali hiyo kulikuwa kumewekwa ishara zote zakuashiria kuna ajali mbele ila dereva hakuzingatia sheria barabarani.
“Chanzo za ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliendesha zaida upande wa kushoto kwa kutozingatia sheria ya barabara,”alisema Chagonja.
Chagonja akizungumzia tukio la Tabora na kusema wahusika watasakwa.
Imeandikwa na Elisante John, Singida, Kamili Mmbando, Dar na Moses Mabula, Tabora.
CHANZO: NIPASHE
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago