Wazee wetu wa kale wengi hawakupata fursa ya kupata elimu ya juu, sekondari na vyuoni kutokana na fursa hizo kuwa chache kwa wakati huo.
Hata hivyo walibahatika kuheshimu tamaduni zetu katika kutanzua matatizo yaliyokuwa yanawakabili kifamilia, koo, kaya na kijamii.
Walitumia tamaduni zetu kutengeneza vijana. Ingawa vijana wengi wa kale nao pia hawakupata fursa ya kufika elimu ya juu kama ilivyo kwa sasa.Lakini kwa wachache waliobahatika kufika huko ndio tunaowaita waasisi wa Taifa.
Waliishi kwa kuheshimu misemo iliyolenga kuimarisha mahusiano, uadilifu, ushupavu, ustaarabu, busara na ujasiri miongoni mwa watu wa rika mbalimbali.
Tamaduni na misemo iliwajenga vijana kuwa wajasiri.
Kwa mfano; kitendo cha kijana “kuzira” au kwa lugha nyingine “kususia” jambo, kitu, kikao, chakula na mambo mengine ya aina hiyo, kilipigwa vita kali na familia, koo, kaya na jamii kwa ujumla. Kijana wa aina hii ya kususia alipewa majina mengi ya dhihaka, kebehi na hata kupuuzwa na jamii inayomzunguka.
Hali kadhalika, wazee waliokuwa na tabia kama hii ya kususia walizomewa, walisutwa, walibezwa huku wakipewa majina ya dhihaka. Hali hii iliwafanya vijana wengi wasithubutu kuzira au kususia jambo. Wale waliokuwa wakisusa waliambiwa ni waoga hata kupata kwao wachumba haikuwa jambo rahisi.
Nimelazimika kuanza makala haya kwa kutafsiri makuzi ya wazee wa kale kwa vijana kutokana na kitendo cha baadhi wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kususia kikao cha majadiliano Bungeni na kutoka nje. Wajumbe hawa ni masalia ya wazee na vijana kama nilivyoainisha hapo juu.
Mbaya zaidi ni kwamba baadhi ya wajumbe walioongoza kitendo hiki ni watu wasomi wasiotiliwa shaka. Wengi wamebobea kushiriki kwenye mikutano, kongamano, semina, warsha na vikao vingine vya majadiliano vinavyo tambulika kitaifa na kimataifa.
Sipendi kuwatia hatiani wajumbe waliosusia vikao halali vya Bunge la Katiba; isipokuwa nasikitishwa na kitendo cha “kususia” au “kuzira”, tabia ambayo ilipigwa vita na wazee wa kale.
Ijapokuwa kwa kutumia vigezo vya kidemokrasia, nakubaliana nao kwamba walikuwa wana haki na uhuru wa kususia vikao Lakini, bado sikubaliani nao kwamba njia sahihi ya kuchukua ilikuwa ni kususia na kutoka nje.
Katika karne hii, dhana ya demokrasia imepata tafsiri mbalimbali kama ilivyokuwa kwenye karne ya 14 na kuendelea.
Wanafalsafa wa karne za nyuma walitumia itikadi katika kutafsiri demokrasia kwa kadri mageuzi ya kifikira, kitamaduni, kiviwanda yalivyokuja kwa kasi.Wanafalsafa hao walitafsiri demokrasia kwa mtazamo unaosigana.
Aidha, kuna wanafalsafa wengine waliotikisa dunia katika masuala ya katiba kwa kujiuliza, Je! ni aina gani ya katiba ambayo ingewafaa jamii katika karne hizo.
Hata hivyo, japo wanafalsafa hawa pamoja na kupata changamoto za hapa na pale, hawakukata tamaa bali waliendelea kufanya utafiti jambo ambalo limewezesha kukua kwa Demokrasia tunayoishuhudia leo.
Ninachotaka kusema ni kwamba; kimsingi kuandaa katiba sio jambo jepesi.
Katiba ndio roho ya Taifa lolote duniani. Katiba hazitofautiani sana kutoka Taifa moja na jingine. Wenzetu waliosusia majadiliano wangetafakari kabla ya kususia vikao hivi.
Wangefuatilia na kujiuliza je! wanafalsafa wa karne (kabla ya ujio wa yesu-BC) walifanikiwa vipi kutunga katiba ambazo zilisaidia jamii katika karne hizo.
Je! kwanini sisi tushindwe kutunga katiba katika karne hii.
Siafikiani na sababu nyingi walizozitoa katika maneno yafuatayo: Mosi; wajumbe walikuwa wakijadili rasimu ya katiba na siyo katiba halisi. Wenye kuamua katiba halisi ni wananchi ambao watapiga kura ya mwisho. Mbona wanasusa kabla wananchi hawajasusa?
Jambo la pili ni kwamba, kipindi cha majadiliano kila mjumbe alikuwa yu huru kuongea kulingana na muda uliotolewa kikanuni.
Muda huo ndio ulikuwa wa kupangua hoja hasi usizoziafiki na kujenga hoja chanya unazokubaliana nazo. Mwisho wa siku, kanuni zinatumika kupata suluhisho la kidemokrasia.
Jambo la Tatu, kususia jambo ni sawa na ‘kumwachia nyani shamba la mahindi’. Ukirudi hupati mavuno tena. Kongamano, warsha, semina ndizo vikao vinavyotumika kuamua mawazo ya waliowengi.
Sijawahi kuona wajumbe wakisusia vikao vya aina hizi.Jambo la Nne, ifahamike kwamba katiba si mali ya chama chochote cha siasa.
Katiba inatumiwa na chama chochote kinachoshika dola. Haijalishi ni chama gani. Katiba haipigi kura, wananchi ndio wapiga kura.
Sijaona sababu kubwa iliyowafikisha wajumbe wa Ukawa kususia vikao. Shuruti watu watambue kwamba nchi hii itaendelea kuishi hata bila Ukawa wala CCM.
Si busara kwa watu wasomi wa aina yake Profesa Lipumba kufanya maamuzi yasiyokuwa ya busara.
Rais wa nchi Jakaya Kikwete kwa hiari yake alikubali kuandikwa kwa katiba mpya. Fursa hii ingetumika kufanya masahihisho ya katiba.
Naamini kama Rais asingekuwa na utashi wa kisiasa, angekaa kimya tu mpaka muda wake unakwisha na kuwaachia wengine.
Nitumie fursa hii kuwasihi viongozi wa Ukawa na wajumbe wengine waliosusia vikao kwamba wakubali kurudi kwenye meza ya majadiliano.
Wajiulize je! ilikuaje wanafalsafa wa enzi za karne ya BC walifanikiwa vipi kuwa na katiba toshelezi karne hizo. Wajiulize, je! waliwasiliana na Watanzania kupata ridhaa yao kabla ya kususia vikao.
Wahenga walinena, “kutenda kosa si kosa, kosa ni kurudia kosa”.
Ukawa bado wana nafasi ya kurudi kwenye meza ya mazungumzo. Kususia sio utamaduni wa vijana waliopata makuzi mema kutoka kwenye familia, koo, kaya zilizostaarabika.
Makala haya yameandikwa na John M. Kibasso
Simu: +255 713 399 004 / +255 767 399 004
E-mail: jmkibasso@yahoo.com
CHANZO: NIPASHE
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago