TULIKOTOKA: NDANI YA MIAKA KUMI, NYERERE ALITUVUSHA KWENYE MITIHANI MIGUMU MITANO, NA HAKUWA DIKTETA...

Ndugu zangu,
Historia ni Mwalimu mzuri. Na tuamini, kuwa ili mwanadamu ajue mahali alipo na anakokwenda, ni muhumi awe na uelewa na alikotoka. Aijue historia yake ili imsaidie kwenye kujitambua.

Nilipata kuyaandika haya kufuatia mada niliyoianzisha juu ya hamu inayojengeka kwenye jamii ya kutamani udikteta.

Nilimjibu mjumbe wangu ndugu Galinoma kama ifuatavyo;

"Galinoma, foleni za unga haikumaanisha udikteta. Dunia ilikuwa tofauti na sasa. Dunia ilikuwa kwenye vita baridi na mapambano ya kiitikadi; Ujamaa dhidi ya Ubepari. Mimi ni Mjamaa, na zaidi ni Social Democrat.

Nimekulia katikati ya mapambano hayo ya kiitikadi. Nchi yetu wakati huo ilipitia mitihani migumu mitano kama taifa; Mtihani wa kwanza; migogoro miwili ya mafuta duniani.

Ni kati ya 70 na 73. Mtihani wa kwanza wa mafuta ni mwaka 1970. Wa pili mwaka 1973. Mtihani wa tatu ni ukame wa mwaka 74. Watanzania tulikula 'Unga wa Yanga' kwa maana ya unga wa njano. Mtihani wa nne ni kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Mtihani wa tano ni Vita vya Kagera 1978-79.

Ndani ya miaka kumi nchi yetu ilipitia mitihani migumu mitano. Nilikuwa na miaka kumi na moja pale Kinondoni Biafra, nilipomsikia kupitia redio, Julius Nyerere akitangaza vita dhidi ya dikteta Idd Amin. Ni Idd Amin aliyetuvamia na kuchukua sehemu ya ardhi yetu.

Usiku ule niliyaona magari ya kijeshi yakipita nje ya nyumba yetu, pale Morocco rd Kinondoni Biafra. Umeme ulikatwa, magari yale yalikuwa yakitokea kambi ya Lugalo kwenda mpakani.

Ndio, nimeishi na kushuhudia kwa macho yangu mwaka ule wa 1979, pale uwanja wa taifa, mbali ya kumpoteza rubani wetu kwenye ndege ya kivita iliyokuwa ituangukie uwanjani, lakini rubani akajitahidi aende akaanguke nayo nje ya uwanja. Nakumbuka Julius Nyerere alibaki amekaa akiwa amekunja miguu na kushika tama. Alionekana kutuli.

Na ilipofika muda wa kuhutubia, Julius alitoa hotuba muhimu yenye kutuandama hadi leo. Aliamua kuacha kuzungumzia ajali ile, bali, alirudia kusema kuwa vita si lelemama, na kwamba Watanzania tujiandae kufunga mikanda kwa miezi kumi na nane. Na hakika imekuwa zaidi ya miaka 18, na hadi leo tuna makovu ya vita. Ni makovu ya kiuchumi.

Naam, ndani ya miaka kumi nchi yetu ilipitia mitihani mitano migumu. Nyerere hakuwa dikteta, alijenga uongozi wa kitaifa uliojenga ushawishi na mshikamano wa kitaifa tukaweza, hata kwa tabu, kuvuka mitihani hiyo mitano na tukabaki salama kama taifa.

Ndio maana leo, inashangaza, wakati tumepoteza ndugu zetu kupambana na kumng'oa dikteta Idd Amin, tunajadili hamu ya kuwa na rais dikteta. Ndio, Historia ni mwalimu mzuri, tuipitie historia yetu. Uganda wamekuwa na dikteta Idd Amin kwa miaka 8, lakini, hata Amin hakumaliza rushwa kwa vifaru vyake vya jeshi. Badala yake alisambaza hofu kwa Waganda na kuwaandama na hata kuwapoteza wapinzani wake.

Na kwa vile , kama taifa, tumepigana na kumshinda dikteta, basi, tusikubali kumkaribisha wenyewe dikteta ndani ya ua wetu...
Maggid Mjengwa.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company