PAC yakataa kupokea taarifa ya CAG


NA LEONCE ZIMBANDU
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Gaudence Kayombo

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeshindwa kupokea taarifa ya ukaguzi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), baada ya kugundua baadhi ya miradi haijaonyeshwa kwenye taarifa.

Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo ilitoa agizo kwa ofisi ya CAG kuandaa upya taarifa hiyo kwa kuhusisha miradi yote kwa kushirikiana na katibu wa kamati hiyo ili kuonyesha miradi iliyokaguliwa kutoka Halmashauri za mikoa ya Iringa, Njombe, Kigoma na Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa PAC, Gaudence Kayombo, (pichani) aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi jijini Dar es Salaam jana baada ya kusitisha uwasilishaji wa taarifa ya ujenzi wa daraja la mto Malagarasi.

Alisema taarifu imekuwa na mapungufu ya kutohusisha miradi mingine ikiwa ni pamoja ujenzi wa bandari, Daraja la Kikwete, lakini pia ilipaswa kuonyesha matumizi ya chenji ya rada iliyotumika.

Kayombo alisema taarifa iliyowasilishwa ilizungumzia taarifa ya ujenzi wa daraja la mto Malagarasi.

“Ebu nendeni mkafanye marakebisho ili mtakapowasilisha kwetu taarifa yenu iwe imekamilika na isiwe vipande vipande,” alisema.

Kayombo alishindwa kutoa ufafanuzi wa lini Ofisi ya CAG ilitakiwa kuwasilisha taarifa hiyo mbele ya kamati yake kutokana na muda wa Bunge la Bajeti kukaribia.

Mkaguzi msaidizi kutoka ofisi ya CAG, Robert Cheyo, alisema taarifa zao walizoandaa zilikuwa za kitaalamu na kuwa haikuwa na kipingamizi kwa kuwa kazi yao ni kukagua na kutoa taarifa ya utekelezaji wa mradi na matumizi ya fedha.


CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company