Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki akitoa taarifa ya kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) ofisini kwake leo jijini Dar es salaam.
*****************************************
Na. Aron Msigwa –MAELEZO,Dar es salaam.
Jumla ya kata 22 katika manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke zitaingizwa katika mpango wa utengaji wa maeneo maalum (smart area) kwa ajili ya kuboresha usafi wa mazingira jijini Dar es salaam.
Akitoa taarifa ya kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Dar es salaam (RCC) leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amesema uanzishaji wa maeneo maalum ya usafi wa mazingira unalenga kuondoa shughuli zote zinazofanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji kinyume cha sheria na kulifanya jiji la Dar es salaam kuendelea kuwa katika hali isiyoridhisha ya usafi wa mazingira.
Amesema utekelezaji wa mpango huo wa utengaji wa maeneo maalum unazingatia sheria ya mipango miji Na. 8 ya mwaka 2007 na sheria ya mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 na kuzitaja kata zitakazohusika katika mpango huo kuwa ni pamoja Keko, Chang’ombe, Kurasini, Mibulani , Sandali na kata ya Gerezani zote za manispaa ya Temeke.
Kata nyingine ni Mchafukoge, Kariakoo, Mchikichini, Jangwani, Kisutu, Kivukoni,Upanga Mashariki na Upanga Magharibi ambazo ziko manispaa ya Ilala na kata za Hananasif, Kinondoni, Kigogo, Mzimuni na Magomeni zote za manispaa ya Kinondoni.