MKOSAMALI: USHINDANI UWE WA HOJA, SIYO MISIMAMO YA VYAMA


Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wametakiwa kushindana kwa hoja badala ya kutumia muda mwingi kujadili mambo ya kichama.
Mjumbe wa Bunge hilo, Felix Mkosamali, alisema katika Kamati Wajumbe wanatakiwa kushindana kwa hoja badala ya kusimamia misimamo waliyojiwekea.

"Inasikitisha kuona watu wazima wanashindwa kujenga hoja na badala yake wamekuwa wakishikilia misimamo yao ya vyama badala ya kujenga hoja," alisema na kuongeza:

"Katiba siyo mali ya chama chochote cha siasa, katiba ni mali ya wananchi wote, lakini inashangaza kuona kuwa wapo watu ambao wanakuja na misimamo yao ambayo inaonyesha wazi kuwa wanatetea masilahi yao binafsi, kinachotakiwa ni lazima kujenga hoja." (J.G)



Hata hivyo, alisema katika Kamati kuna changamoto kubwa kutokana na vyama vyote vya siasa kuwa na misimamo yao.

Alisema changamoto iliyopo ni pale wanapokwenda kujadili mambo nyeti, lakini unakuta kuna wajumbe wamekwenda na misimamo yao ya kutetea maslahi ya vyama vyao.

"Jambo hilo linaweza kutuathiri kwa kiasi kikubwa na kushindwa kufikia mwafaka wa kusaidia taifa kupata katiba ambayo ni nzuri na yenye manufaa kwa taifa na wananchi wote," alisema.

Aliongeza kuwa kutakuwa na shida kubwa katika Kamati kutokana na wajumbe wengi kuja katika Bunge Maalum la Katiba wakiwa na maelekezo ya misimamo ya vyama vyao.

"Kitendo cha watu au kikundi cha watu kuandaa rasimu mbadala kwa ajili ya kupinga rasimu iliyokuwepo..."Sisi tunataka mtu atakayepinga naye atuletee vitabu ambavyo vinaonyesha utafiti wa kina uliofanyika na atuambie alikusanya maoni hayo wapi na kwa muda gani, asije mtu kupinga tu huku akiwa na hoja za hewani hewani hilo hatulitarajii na hatutalikubali," alisema.

Alisema wananchi wanatakiwa kutambua kuwa Tume ya Jaji Joseph Warioba imetumia zaidi ya Sh. bilioni 66 na kama maoni yao watayaona hayana maana basi hapakuwepo haja ya kutumia fedha hizo kukusanya maoni," alisema.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company