Watu 58 wauawa katika shambulio dhidi ya makao makuu ya UN Sudani Kusini

Raia Sudani Kusini wakipewa hifadhi, baada ya kuyakimbia mapigano katika mji wa Bor.
Reuters  Na RFI
Watu wasiopungua 58 wameuawa na wengine zaidi ya 100 wamejeruhiwa wakati makao makuu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudani Kusini yaliposhambuliwa. Maelfu ya raia wa Sudani Kusini walikua wamepewa hifadhi kwenye kambi moja ilijengwa kwenye makao makuu hayo ya Umoja wa Mataifa, baada tu ya mapigano kuzuka.

“Miili 48 ikiwa ni ya watoto, wanawake na wanaume imekutwa katika katika kambi moja iliyokua imejengwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Miili 10 ya watu waliyoshambulia imekutwa pia kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Watu 58 ndio wanaaminika kuwa wameuawa, lakini idadi hio inaweza ikaongezeka, kwani miongoni mwa watu 100 waliyojeruhiwa, baadhi yao wamejeruhiwa vikali”, mkuu wa shuguli za misaada kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Sudani Kusini, Toby Lanzer amesema wakati alipokua akiongea na AFP.

Magari ya jeshi la Sudani Kusini katika mji wa Bor.REUTERS/James Akena
Shambulio hilo limetokea katika mji wa Bor (mashariki), mji ambao uko chini ya himaya ya serikali ya Sudani Kusini, Idadi watu waliyouawa iliyotolewa mwanzo na balozi wa Marekani Kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power, ilikua ni ya watu 20 na wengine 70 kujeruhiwa.

Wakati huohuo Umoja wa Mataifa umelani shambulio hilo na kusema kusikitishwa na machafuko yanayoendelea nchini Sudan Kusini, baada ya watu waliojihami kwa silaha kuvamia kambi ya wakimbizi ya Umoja wa Mataifa mjini Bor na kuwaua zaidi ya watu 20.

Balozi wa Marekani katika Umoja huo Samantha Power amesema watu hao waliojihami kwa silaha walionekana kama waandamanaji wa kawaida kabla ya kuanza kufyatua risasi ndani ya kambi hiyo inayoaminiwa kuwapa hifadhi wakimbizi wengi kutoka kabila la Nuer la aliyekuwa Makamu wa rais Riek Machar.

Katibu mkuu wa UN, Ban Ki Moon ameonya dhidi ya mashambulizi mengine yatakayoelekezwa kwenye kambi ya Jonglei ambayo inawahifadhi zaidi ya wakimbizi laki 5 wa Sudan Kusini, mji ambao unagombea na pande mbili zinazokinzana nchini humo.

Shambulio hili linajiri wakati huu waasi wanaoongozwa na Riek Machar wakijiandaa kusonga mbele kuelekea mji mkuu Juba kumng'oa rais Salva Kiir.

Amani imetoweka Sudan Kusini kwa miezi kadhaa sasa tangu makabiliano yalipozuka kati ya wanajeshi wa Sudani Kusini na waasi wa makamu wa rais Riek Machar wanaomtaka rais Salva Kiir kuondoka madarakani.

Mazungumzo ya amani jijini Addis Ababa Ethiopia hadi sasa bado hayajazaa matunda kumaliza mzozo huo.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company